WIZARA YA MAMBO YA NJE

WIZARA YA MAMBO YA NJE

162.9K subscribers

Verified Channel
WIZARA YA MAMBO YA NJE
WIZARA YA MAMBO YA NJE
May 15, 2025 at 08:55 PM
FINLAND YAKARIBISHWA KUWEKEZA KATIKA MIRADI YA MAWASILIANO NCHINI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Finland katika sekta ya mawasiliano kwa lengo la kukuza teknolojia na kuendeleza miundombinu ya kisasa nchini. Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, wakati wa kikao na Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjälä, kilichofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam. Balozi Shelukindo ameeleza kuwa Tanzania inatambua nafasi muhimu ya sekta ya mawasiliano katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Amesisitiza kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Finland, hususan kampuni zilizobobea katika teknolojia ya mawasiliano kama Nokia, ili kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za mawasiliano nchini. “Tunaamini kuwa ushirikiano wa kimkakati katika sekta ya mawasiliano utasaidia kuongeza tija katika sekta za biashara, elimu, na huduma za kijamii,” alisema Balozi Shelukindo. Akiwa amembatana na ujumbe wa wawakilishi wa sekta binafsi kutoka Finland, wakiwemo wawakilishi wa Kampuni ya Nokia, Mhe. Syrjälä ameeleza kuwa Finland imejipanga kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika maeneo ya maendeleo. Amebainisha kuwa kampuni za teknolojia kutoka Finland, ikiwemo Nokia, zipo tayari kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya mawasiliano nchini. Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa , Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), ambao wameeleza utayari wa kushirikiana na Finland katika kukuza sekta ya mawasiliano kama kichocheo cha maendeleo endelevu.
Image from WIZARA YA MAMBO YA NJE: FINLAND YAKARIBISHWA KUWEKEZA KATIKA MIRADI YA MAWASILIANO NCHINI  Ser...
👍 ❤️ 😂 😢 😮 🙏 8

Comments