WIZARA YA MAMBO YA NJE
May 24, 2025 at 08:35 PM
Rais Mbeki: “Ili kuiadhimisha Siku ya Afrika, ni lazima tuijadili kwanza Afrika”
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Mhe. Thabo Mbeki amewataka viongozi wa Afrika kusimamia vyema utekelezaji wa sera za nchi na Afrika kwa ujumla ili kutatua changamoto zinazowakabili Waafrika na kufikia maendeleo ambayo Afrika inayakusudia kuyapata.
Rais Mbeki ameyasema hayo akifungua Mhadhara wa Siku ya Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki na kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam Mei 24, 2025.
Mhe. Mbeki katika hotuba hiyo ya ufunguzi, amesisitiza umuhimu wa nafasi ya kizazi cha sasa katika kuendeleza mapambano ya kuiendeleza Afrika yenye umoja, iliyoanzishwa na viongozi waliotangulia.
Pia, ameeleza kuwa katika kuiadhimisha Siku ya Afrika Duniani inayoadhimishwa kila Mei 25, ni vyema kujadili changamoto zinazoikumba Afrika na kuzitekeleza sera zinazowekwa ili kufikia malengo ya maendeleo Afrika. “Tumepitisha sera nyingi na nzuri kwa mustakabali wa Afrika, changamoto kubwa ni kwamba watu wachache ndio wanatekeleza sera hizo… Ili kuiadhimisha Siku ya Afrika, ni lazima tuijadili kwanza Afrika” amesema Rais Mbeki.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Mhadhara wa mwaka 2025 kufanyika Tanzania na kutambua mchango mkubwa wa Tanzania katika kuiunganisha Afrika na uongozi imara akiongeza kuwa mbali na Afrika Kusini, Tanzania ndio nchi pekee Afrika ambayo imekuwa mwenyeji wa Mhadhara wa Siku ya Afrika mara tatu hadi sasa.
👍
🙏
❤️
😮
27