Kalamu House
Kalamu House
May 30, 2025 at 01:54 PM
```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA KWANZA``` Ndege ikiwa inakaribia kutua, mhuduma aliwatangazia waweze kuwa na utulivu wafunge mikanda na kuwa tayari kwa mitikisiko na ukosaji wa utulivu kwa muda mchache wanapotua chini. Dirishani Malaika alitazama nje kuliona jua likizama wakati maelezo hayo yakitolewa, mawazo yake yakiwa mbali na mahali pale akitamani kile kilichomrudisha kifanikiwe. Miaka saba tangu aondoke, miaka saba ametumia kugundua uhitaji wa moyo wake, miaka saba ya kugundua kuwa bado anampenda Amon, miaka saba ya kuwa tayari kuishi na Amon bila kujali hadhi yake wala daraja alilokuwepo la maisha, miaka saba ya kutambua kuwa anaweza kumtengeneza Amon kuwa yeyote anayetaka yeye kuwa baada ya miaka saba ya kuteseka na mapenzi! Alishituliwa na mtikiso wa ndege ilipogusa ardhi lakini haikumletea shida yeyote; alipata kutambua tayari wametua kuonesha alikuwa hatua chache karibu na ndoto yake. Katika muonekano wa tofauti zaidi na miaka saba iliyopita, akionekana mwanamke mwenye kujielewa zaidi na mtu mzima; urembo ukiwa zaidi ya ulivyokuwa mwanzo. Mavazi yake yalitambulisha hadhi yake ya maisha, mkoba alioshika, begi aliloburuza akitoka katika milango ya kiwanja kile cha ndege. Tofauti na mara nyingine ambazo alikuwa akirudi nyumbani kutoka nchi nyingine, siku hiyo hakuja kuchukuliwa na baba yake, hata uwepo wake pale haukutambuliwa akiwashitukiza wote wanaomfahamu kuhusu kurudi kwake nchini. Alifika eneo la maegesho ya magari na kukuta gari nyingi za usafiri lakini hakuna aliyemkimbilia. Kila mtu alikuwa makini kwenye gari lake kama waliokuwa wakisubiri taarifa fulani kabla ya kuondoka kufuata wateja. Hakuelewa kilichoendelea na kumfanya asogelee gari moja aliyekuwa nje ya gari lake kumuuliza. “Mambo kaka!” alimsalimu akivua miwani aliyokuwa amevaa kuzungumza nae. “Poa!” alijibu dereva yule akimtazama kumsikiliza shida yake. “Hizi sio gari za biashara!?” alimuuliza. “Ni za biashara!” alijibu. “Unaweza kunipeleka…!” kabla ya kumaliza aliulizwa. “Umeagizia usafiri!?” “Kuagiza!? Kuagiza!?” alibaki kushangaa. “Hizi zote ni gari za mtandaoni, ukitaka usafiri lazima uagize katika mtandao!” alimfafanulia. “Hee… na huku pia mna huo mfumo!” alishangaa akitabasamu. “Ndio!” “Sawa, huo mtandao unaitwaje!?” alimuuliza akitoa simu yake huku akijiuliza ni vingapi vimebadilika ndani ya miaka saba hiyo. “A&N” alimjibu akiandika kwenye simu yake kupakua mtandao huo. “Ndio hii?” alimuonesha kuthibitisha kwenye simu yake kama ndio hiyo. “Ndio!” alimjibu na kubonyeza kitufe cha kupakua. Alijisajili na kufanikiwa kuagiza usafiri akiondoka na gari lile lile moja kwa moja akiandika eneo la kupelekwa akioneshwa gharama na jina la dereva wake, namba ya usajili wa gari na muda watakaotumia. Alitabasamu kuona maendelea yaliyotokea nyumbani kwao. Alihitaji kufika nyumbani kwao kisha kutoka kumtafuta Amon; hakupanga kutulia, hakuwa na mpango wa kupoteza siku bila kukutana na Amon. Ulikuwa ujio wa kushitukiza kwa baba yake ambae hakumtegemea Malaika kurudi, tena sio siku hiyo; bila taarifa. Licha ya kuwa tukio ambalo hakulitegemea, bado lilijaza furaha nafsini mwake kumuona mwanae wa pekee. Walisalimiana lakini Malaika alionesha kuwa na haraka ambayo baba yake hakuijua ni ya nini. “Unaelekea wapi tena!?” alimhoji kumuona akiteremka kutoka ghorofani kilipo chumba chake akiwa katika hali ya kuonekana anaetoka. “Kuna ntu naenda kumuona kisha narudi baba, mara moja!” alijibu Malaika akitabasamu na kusogea mpaka sehemu wanapoweka funguo za gari. “Huwezi kumsubirisha mpaka kesho angalau!?” alimdadisi akitamani angepata kupumzika baada ya safari. “Nadhani ni mimi ndiye nisiyeweza kutulia!” alijibu akiendelea kutafuta ufunguo wa gari lake. “Aaah…!” alikosa cha kuongea akisikitika. “Hivi ufunguo wa gari….!” “Ooh… chukua huo wa gari langu hapo, wa duara huo wa Audi!” alimjibu. “Gari lako sidhani kama liko tayari kutembelewa, sijalifanyia ukaguzi haswa baada ya kukaa eneo la maegesho kwa muda mrefu!” alimueleza sababu. “Sawa!” aliuchukua ufunguo ule alioambiwa. Alifika alipo baba yake na kum’busu kwenye paji la uso kisha kutoka nje akitupa macho kwenye maegesho ya magari na kuona kukiwa na magari matatu; mawili yakionekana wazi na moja kufunikwa. Katika mawili yale aliliona Audi RS7 la kijivu ambalo funguo yake alikuwa nayo na kubinya kitufe kwenye kidude kile cha duara na gari kujitoa loki za mlango akisogea lilipo. Pasipo kupoteza muda aliingia ndani ya gari lile na kuliwasha, likiunguruma kwa sekunde chache kabla ya kuwa kimya kiasi cha kushindwa kutambua kama limewashwa. Alikanyaga mafuta huku gia ikiwa kwenye sehemu ya maegesho na injini kunguruma tena na kumfanya atabasamu akitikisa kichwa. “Baba kapata wapi ladha za magari haya!” alijisemea mwenyewe akicheka na kulitoa gari mahali pale. Kwakuwa mlinzi alimuona akitoka na kuingia kwenye gari, tayari alifungua geti na Malaika kutoka getini na gari lile. Safari kuelekea alipokuwa akiishi Amon, njiani aliwaza kama atapakumbuka lakini kwa namna maeneo yalivyokuwa ilimuaminisha kuwa atapakumbuka. Aliposhika njia iliyompeleka mpaka nyumba ile aliyokuwa akiishi Amon, mapigo ya moyo yalimuenda mbio akitafakari itakavyokuwa atakavyoonana nae. Aliwaza kuwa muwazi na kumuomba msamaha akikiri kuwa alikosea kutokumpa nafasi. Moyoni mwake aliamini kueleweka akiwa tayari kumthibitishia kwa chochote kile kuwa amebadilika.
Image from Kalamu House: ```SIMULIZI: MALAIKA 2```  ```SEHEMU: YA KWANZA```  Ndege ikiwa inakar...
❤️ 1

Comments