
Kalamu House
30 subscribers
About Kalamu House
Nyumba Ya Simulizi!
Similar Channels
Swipe to see more
Posts

```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA KWANZA``` Ndege ikiwa inakaribia kutua, mhuduma aliwatangazia waweze kuwa na utulivu wafunge mikanda na kuwa tayari kwa mitikisiko na ukosaji wa utulivu kwa muda mchache wanapotua chini. Dirishani Malaika alitazama nje kuliona jua likizama wakati maelezo hayo yakitolewa, mawazo yake yakiwa mbali na mahali pale akitamani kile kilichomrudisha kifanikiwe. Miaka saba tangu aondoke, miaka saba ametumia kugundua uhitaji wa moyo wake, miaka saba ya kugundua kuwa bado anampenda Amon, miaka saba ya kuwa tayari kuishi na Amon bila kujali hadhi yake wala daraja alilokuwepo la maisha, miaka saba ya kutambua kuwa anaweza kumtengeneza Amon kuwa yeyote anayetaka yeye kuwa baada ya miaka saba ya kuteseka na mapenzi! Alishituliwa na mtikiso wa ndege ilipogusa ardhi lakini haikumletea shida yeyote; alipata kutambua tayari wametua kuonesha alikuwa hatua chache karibu na ndoto yake. Katika muonekano wa tofauti zaidi na miaka saba iliyopita, akionekana mwanamke mwenye kujielewa zaidi na mtu mzima; urembo ukiwa zaidi ya ulivyokuwa mwanzo. Mavazi yake yalitambulisha hadhi yake ya maisha, mkoba alioshika, begi aliloburuza akitoka katika milango ya kiwanja kile cha ndege. Tofauti na mara nyingine ambazo alikuwa akirudi nyumbani kutoka nchi nyingine, siku hiyo hakuja kuchukuliwa na baba yake, hata uwepo wake pale haukutambuliwa akiwashitukiza wote wanaomfahamu kuhusu kurudi kwake nchini. Alifika eneo la maegesho ya magari na kukuta gari nyingi za usafiri lakini hakuna aliyemkimbilia. Kila mtu alikuwa makini kwenye gari lake kama waliokuwa wakisubiri taarifa fulani kabla ya kuondoka kufuata wateja. Hakuelewa kilichoendelea na kumfanya asogelee gari moja aliyekuwa nje ya gari lake kumuuliza. “Mambo kaka!” alimsalimu akivua miwani aliyokuwa amevaa kuzungumza nae. “Poa!” alijibu dereva yule akimtazama kumsikiliza shida yake. “Hizi sio gari za biashara!?” alimuuliza. “Ni za biashara!” alijibu. “Unaweza kunipeleka…!” kabla ya kumaliza aliulizwa. “Umeagizia usafiri!?” “Kuagiza!? Kuagiza!?” alibaki kushangaa. “Hizi zote ni gari za mtandaoni, ukitaka usafiri lazima uagize katika mtandao!” alimfafanulia. “Hee… na huku pia mna huo mfumo!” alishangaa akitabasamu. “Ndio!” “Sawa, huo mtandao unaitwaje!?” alimuuliza akitoa simu yake huku akijiuliza ni vingapi vimebadilika ndani ya miaka saba hiyo. “A&N” alimjibu akiandika kwenye simu yake kupakua mtandao huo. “Ndio hii?” alimuonesha kuthibitisha kwenye simu yake kama ndio hiyo. “Ndio!” alimjibu na kubonyeza kitufe cha kupakua. Alijisajili na kufanikiwa kuagiza usafiri akiondoka na gari lile lile moja kwa moja akiandika eneo la kupelekwa akioneshwa gharama na jina la dereva wake, namba ya usajili wa gari na muda watakaotumia. Alitabasamu kuona maendelea yaliyotokea nyumbani kwao. Alihitaji kufika nyumbani kwao kisha kutoka kumtafuta Amon; hakupanga kutulia, hakuwa na mpango wa kupoteza siku bila kukutana na Amon. Ulikuwa ujio wa kushitukiza kwa baba yake ambae hakumtegemea Malaika kurudi, tena sio siku hiyo; bila taarifa. Licha ya kuwa tukio ambalo hakulitegemea, bado lilijaza furaha nafsini mwake kumuona mwanae wa pekee. Walisalimiana lakini Malaika alionesha kuwa na haraka ambayo baba yake hakuijua ni ya nini. “Unaelekea wapi tena!?” alimhoji kumuona akiteremka kutoka ghorofani kilipo chumba chake akiwa katika hali ya kuonekana anaetoka. “Kuna ntu naenda kumuona kisha narudi baba, mara moja!” alijibu Malaika akitabasamu na kusogea mpaka sehemu wanapoweka funguo za gari. “Huwezi kumsubirisha mpaka kesho angalau!?” alimdadisi akitamani angepata kupumzika baada ya safari. “Nadhani ni mimi ndiye nisiyeweza kutulia!” alijibu akiendelea kutafuta ufunguo wa gari lake. “Aaah…!” alikosa cha kuongea akisikitika. “Hivi ufunguo wa gari….!” “Ooh… chukua huo wa gari langu hapo, wa duara huo wa Audi!” alimjibu. “Gari lako sidhani kama liko tayari kutembelewa, sijalifanyia ukaguzi haswa baada ya kukaa eneo la maegesho kwa muda mrefu!” alimueleza sababu. “Sawa!” aliuchukua ufunguo ule alioambiwa. Alifika alipo baba yake na kum’busu kwenye paji la uso kisha kutoka nje akitupa macho kwenye maegesho ya magari na kuona kukiwa na magari matatu; mawili yakionekana wazi na moja kufunikwa. Katika mawili yale aliliona Audi RS7 la kijivu ambalo funguo yake alikuwa nayo na kubinya kitufe kwenye kidude kile cha duara na gari kujitoa loki za mlango akisogea lilipo. Pasipo kupoteza muda aliingia ndani ya gari lile na kuliwasha, likiunguruma kwa sekunde chache kabla ya kuwa kimya kiasi cha kushindwa kutambua kama limewashwa. Alikanyaga mafuta huku gia ikiwa kwenye sehemu ya maegesho na injini kunguruma tena na kumfanya atabasamu akitikisa kichwa. “Baba kapata wapi ladha za magari haya!” alijisemea mwenyewe akicheka na kulitoa gari mahali pale. Kwakuwa mlinzi alimuona akitoka na kuingia kwenye gari, tayari alifungua geti na Malaika kutoka getini na gari lile. Safari kuelekea alipokuwa akiishi Amon, njiani aliwaza kama atapakumbuka lakini kwa namna maeneo yalivyokuwa ilimuaminisha kuwa atapakumbuka. Aliposhika njia iliyompeleka mpaka nyumba ile aliyokuwa akiishi Amon, mapigo ya moyo yalimuenda mbio akitafakari itakavyokuwa atakavyoonana nae. Aliwaza kuwa muwazi na kumuomba msamaha akikiri kuwa alikosea kutokumpa nafasi. Moyoni mwake aliamini kueleweka akiwa tayari kumthibitishia kwa chochote kile kuwa amebadilika.


```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA PILI``` Mwanamke wa miaka thelathini na tatu (33) sasa, hakuwa yule Malaika wa miaka ishirini na sita (26). Kimuonekano alizidi kupendeza, umbo la namba nane, kiuno chembamba kilichoshikiliwa katika na miguu ya umbo la bia na mapaja yaliyotanuka pembeni kuzidisha mvuto kwake kwa kila aliyemuona. Urefu wa wastani katika rangi yake ya kahawia kuonesha asili yake ya watu weusi. Nje na muonekano aliokuwa nao, mtazamo wake wa maisha ulibadilika sana na vitu vingi alijifunza kipindi ambacho hakuwepo nyumbani, vitu vilivyomfanya ajione kuwa vingi hakuwa akijua au kutambua kuhusu maisha. Kila alipopita mtaani kule watu walishangaa kuliona gari la aina ile maeneo yale, hayakuwa maeneo ambayo gari la aina ile kuonekana; hivyo iliwafanya kila mmoja kutoka kulitazama; likiwa la muonekano wa tofauti, lilivutia wengi walioliona na kutamani kumjua aliyekuwa akiendesha. Alifika mpaka nje ya nyumba ile na kuteremka kwenye gari kila mmoja akitazama ni nani aliyekuwa akishuka huku ukitangulia mguu wa kulia kuteremka, mguu uliovutia kuashiria aliyeteremka alikuwa mlimbwende. Katika gauni fupi la kitambaa chepesi lililoishia magotini likiwa la maua, mguu ule ulionekana. Alifunga mlango wa gari na kusogea mlangoni mwa nyumba ile kila mmoja aliyemuona akijiuliza kama mwanamke huyo amepotea njia au kuwa mahali sahihi. Alishusha pumzi akitambua kuwa watu wanamtazama na kutokuwajali akisogea mlangoni pale na kabla kubisha hodi alitoka mwanamke mmoja. “Habari yako dada!” alimsalimu mwanamke huyo. “Nzuri!” alijibu akimtazama kutoka juu mpaka chini na kurudia tena mara ya pili akimshangaa. “Samahani; kuna mtu namuulizia!” alianza kueleza hitaji lake. “Humu ndani?” alijibu mwanamke yule kuonesha katika hali ya kutokuamini mwanamke kama yeye amuulizie mtu wa maeneo yale. “Ndio!” alijibu Malaika. “Nani!?” alimuuliza akimtazama kwa shauku jubwa ya kutaka kujua. “Anaitwa Amon!” alijibu Malaika mapiga yake ya moyo yakienda mbio. “Amon??” aliuliza mara ya pili akionesha kutokumuelewa. “Ndio!” alithibitisha. “Mmmh… hakuna mtu anaitwa Amon hapa!” alijibu wakati huo majirani kadhaa walioshindwa kuvumilia walisogea karibu na nyumba ile. “Wee, mama Zuu, anamuulizia nani?” jirani mmoja aliuliza. “Anamuulizia, nani vile umesema!?” alimgeukia tena kumuuliza ikiwa tayari alisahau jina alilotajiwa. “Amon, namuulizia Amon!” alijibu akiwaeleza kwa sauti na wale waliofika karibu yao. “Mmmh, mbona hatumjui!” Alijibu yule jirani aliyesogea kuuliza. “Hamuwezi kumjua, alihama zamani sana!” sauti moja ya Mzee aliyekuwa anapita njia ilisikika ikiwaeleza. “Mmmh… mzee Bakari na wewe hupitwi!” alizungumza yule aliyekuwa akizungumza na Malaika mlangoni pale. “Samahani mzee wangu!” Malaika aliondoka pale upesi akimfuata baada ya kuona nuru ambapo tayari alipoteza matumaini. “Unaweza kujua alipohamia!?” alimdadisi. “Sijui, miaka mingi imepita bila kusikia lolote wala kumuona!” alijibu akizidi kupoteza matumaini yeyote aliyokuwa nayo Malaika. “Naomba unisaidie mzee wangu, tafadhali!” alijaribu kum’bembeleza. “Mmmh… sijui, jaribu kuulizia ulizia, ila sio huku mtaani!” maelezo hayo yalimfanya akose kujua pa kuanzia zoezi likizidi kuwa gumu zaidi ya lilivyokuwa. “Nitamuulizia wapi?” aliuliza ikiwa ndio swali lililokuwa kichwani mwake. Mzee yule alimtazama akimuona amekosa matumaini na kumhurumia. “Twende nikupeleke!” alimueleza akimpa wazo alilokuwa nalo. “Sawa, twende!” bila kufikiria zaidi, Malaika aliona hana cha kupoteza. Mzee yule aliingia kwenye gari na Malaika kuzunguka upande wa pili kisha akiwasha gari na kuondoka mahali pale akiongozana na mzee yule huku wale waliosogea katika nyumba ile wakibaki kushangaa na kuangusha kicheko cha umbea na unafiki. Walitoka nje ya mitaa ile na kurudi maeneo ya mjini. “Egesha gari hapo pembeni!” alimuagiza Malaika na Malaika kufuata maagizo hayo. “Wewe ni mgeni!?” alimdadisi baada ya kusimamisha gari. “Ni muda tangu niondoke huku, ndio nimerejea!” alijibu Malaika. “Ndio maana!” alijibu. “Kwanza kabisa, hutakiwi kumuamini mtu haswa kwa mwanamke kama wewe!” alizungumza Mzee yule maneno yaliyoanza kumpa wasiwasi Malaika. “Kwanini!?” alidadisi huku akiwa na hofu. “Maisha tofauti na yalivyokuwa zamani, pale tayari watu walikuwa wakupangie njama na nilichokusaidia ni kukuokoa; mitaa kama ile wenzako hawathubutu kusogea kabisa!” alimueleza akimtisha sana Malaika. “Sasa nawezaje kumpata Amon!?” alimdadisi akirudi kwenye hitaji lake. “Nilipata habari kuwa maisha yake yamebadilika sana hivyo huwezi kumpata uswahilini!” alimueleza. “Nitampata wapi!?” “Kuna uwezekano ukaonana nae huko huko kwenu, maeneo ambayo nyie hukutana, ndio maeneo unaweza kumkuta na yeye au angalau kumuulizia!” alimjibu akimpa namna nyingine ambayo haikuingia akilini. “Mmmh…!” alikosa cha kusema maneno yakimuisha na kubaki kujiona amefika ukingo wa kuonana na Amon. “Ila kuwa makini sana, kuwa makini na maeneo yale; nakuomba sana!” alimueleza akifungua mlango wa gari lile kutaka kuteremka. “Samahani Baba!” alimsimamisha kabla hajateremka na kumfanya afunge mlango. “Chukua hii nauli ya kurudia, na ahsante sana!” alimpatia shilingi elfu hamsini kutoka kwenye pochi yake. “Ahsante sana!” aliipokea pesa ile akitabasamu na kuteremka kwenye gari lile.


```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA TATU``` Malaika alibaki mahali pale kwa muda kabla ya kuondoka na kuamua kurudi nyumbani akijua mpango aliokuwa nao siku hiyo haukufanikiwa. Aliingia katika hali ya unyonge kutokufanikiwa ila bado aliweka uso wa furaha usoni mwake ili kuondoa maswali yeyote kwa baba yake. “Vipi umefanikiwa kuonana na huyo mtu!?” alimdadisi baada ya Malaika kuingia ndani. “Naweza kusema nimefanikiwa japo sijamuona!” alijibu akitabasamu. “Oooh… angalau kama jambo limefanikiwa!” alifurahi kusikia hivyo kuwa binti yake ameonesha kufanikiwa. “Angelina!” aliita baba yake Malaika huku Malaika akijiuliza ni nani aliyeitwa. “Abee!” sauti ya kike iliitika kutoka jikoni. “Unamfahamu!?” alimuuliza baada ya kufika sebuleni pale walipokuwa. “Hapana!” alijibu akitikisa kihwa kuweka msisitizo. “Huyu ndiye Malaika!” alimtambulisha kwake Malaika aliyekuwa akitabasamu pale kwenye kochi alipokuwa ameketi. “Malaika, huyu ndiye anaenilea angalau umenikuta katika afya nzuri!” alimgeukia Malaika na kumtambulisha. “Oooh… nakuona hata umezidi kunawiri!” alimsifu muonekano wake. “Basiii, hiyo ndio kazi ya Angelina na kwa bahati nzuri anajina kama lako tu, wote ni Malaika wangu!” alijibu akitabasamu kuonesha thamani ya wanawake wale. “Nashukuru kukufahamu dada!” Angelina alizungumza akimtazama Malaika kwa tabasamu. “Na mimi pia, nashukuru kukufahamu!” alijibu Malaika akirudisha tabasamu kwake. “So Malaika, umerudi moja kwa moja, si ndio!?” aliuliza baba yake akitaka kujua ujio huwa wa ghafla wa binti yake ni ule wa moja kwa moja au wa dharura. “Nimerudi moja kwa moja, baba!” alijibu Malaika wakati Angelina akiwa tayari ameondoka. “Nadhani nichukue likizo yangu kabla ya kustaafu kabisa!” bila kupoteza muda aliweka wazi hitaji la moyo wake kwa mwanae. “Mmmh… baba, bado mapema; kampuni inakuhitaji!” “Mapema ndio vizuri!” alijibu akionesha tayari kuamua. “Nahitaji muda kidogo lakini!” Malaika bado alionesha kipingamizi cha kuchukua nafasi ya baba yake. “Muda ndio haupo!” Bado baba yake alisimamia maamuzi yake akinyanyuka kwenye kochi lile akielekea chumbani. Malaika nae alipanda chumbani kwake akienda kubadilisha na kuoga kabisa kisha baada ya kutoka bafuni na kuvaa mavazi ya kulalia, alijilaza kitandani akiwaza namna anaweza kumpata Amon. Alijiuliza ni mangapi yamempita wakati hayupo na Mzee yule alimaanisha nini kumwambia ataonana nae kwao; na ni maeneo yapi ambayo wanakutana! Maswali yalimtatiza akiwaza kama Mzee yule alikuwa akimdanganya au kumueleza ukweli. “Dada, chakula tayari!” aligongewa akiwa chumbani kwake. “Ahsante!” aliitika akiendelea kuwazua namna anaweza akampata Amon. Mawasiliano alionesha kupoteza ikiwa hata namba zake hakuwa nazo huku yeye mwenyewe akiwa bado hana namba ya mawasiliano ya mtandao wa simu wa nchini akitumia mtandao wa kijamii na intaneti (Wi-Fi). Mpango aliokuwa nao ni kusajili namba mpya ya mawasiliano kwake atakayokuwa akiitumia siku ikipambazuka haswa baada ya muda huo kiza kutanda. Aliteremka chini kwenda kupata chakula na baba yake akiwa na Angelina ambao wote walikaa meza moja kitu ambacho kidogo kilimfanya Malaika ajiulize ila kushindwa kusema neno au kuonesha utofauti wowote. Katika meza iliyo ndefu yenye viti nane, vitatu kila upande wa urefu na kimoja katika kila mapana. Kiti cha mapana alikalia baba yake wakati upande wa kushoto akiwa Angelina na kulia kwake kwenda kuketi Malaika akiwa anatazamana na Angelina. Ni muda sana tangu kuwa hivyo wakipata chakula pamoja, hata katika uwepo wake hapo nyuma, hakuwa akiketi na baba yake; labda ni kwa ajili ya ujio wake. “Unaonekana unafuraha sana baba!” Malaika alimdadisi baba yake akimtazama. “Lazima nifurahi, binti yangu upo hapa; kwanini nisijawe na furaha!?” alijibu. “Aaah… hii furaha sio ya siku moja, hata nilipokuwa nikiongea na wewe; sauti yako ilijawa na furaha!” aliendelea kumdadisi akimtazama Angelina aliyekuwa ameinamisha kichwa chake kwenye sahani yake wakati baba yake akitazama mwisho wa meza ile kwenye kiti kilichomuangalia. “Usipojawa na furaha katika haya maisha, utafurahi lini!?” alijibu akigeuza shingo kumtazama Malaika akitabasamu. “Haya bhana!” alijibu akiamua kuyamaliza mazungumzo hayo. “Mmmh, chakula kitamu sana; nilikumbuka sana ladha ya chakula cha nyumbani!” alikisifia chakula baada ya kula kijiko kimoja tu. “Kazi ya Angel hiyo, mpishi mzuri sana; hii nayo ni sababu ya kuwa na furaha!” alijibu Baba yake akimsifia Angelina. Malaika alihisi jambo lisiloeleweka, furaha ya baba yake na hali aliyomkuta ya uchangamfu, afya iliyonawiri; ilioneshwa alipata matunzo mazuri. Mara ya mwisho Baba yake kuwa katika hali nzuri ni kipindi cha uhai wa mama yake ndio alikuwa hivyo na furaha pamoja na kunawiri, ila baada ya Mama yake kufariki, hakuwahi kuuona uchangamfu wa baba yake mara kwa mara, na hata alipokuwa akirudi nyumbani kutoka masomoni bado hakuwa na furaha hiyo; labda ni kweli kwasababu yake kwakuwa alichukua muda sana nje bila kurudi nyumbani; atatambua mbeleni, uzuri yupo hapo kuishi.


```SIMULIZI: THE FORBIDDEN LOVE``` ```SEHEMU: YA KWANZA``` Aidan bado hajaingia!?” Aliuliza Baba yao baada ya kutoka dukani alikokwenda kuchukua baadhi ya vitu. “Nadhani hata chukua muda sana!” Alijibu mwanae wa kiume, kaka yake na Aidan aliyetazama saa yake ya mkononi iliyokuwa katika mfuko wake wa suruali na kuona ni karibu na majira aliyosema. “Saa ngapi?” Alimuuliza akitaka kujua ni muda gani wa kumtarajia. “Sasa ni saa kumi kasoro, kwa maelezo yake; saa kumi kamili mpaka narobo hivi atakuwa hapa!” Alimjibu baba yake. “Sawa!” “Mbuzi tayari umeshammaliza!?” Alimuuliza mwanae huyo ambae alikuwa na jukumu la kumtengeneza mbuzi. “Naelekea kwenda kumuandaa sasa hivi, tayari nimeshamaliza kuchuna ngozi!” alijibu akiirudisha mfukoni alipoitoa na kuchukua mizigo ile aliyokuja nayo baba yake na kuelekea nayo mpaka jikoni akiweka chupa zile za vinywaji mbalimbali katika jokofu. Wanawake walikuwa nje wakishughulika na mapishi huko; siku hiyo jiko la ndani halikutumika kutokana na ukubwa wa siku na umuhimu wake. Baada ya kuweka vinywaji vile, alifungua mlango wa jikoni wa nyuma na kuwaona wanawake wakiwa huko na hekaheka nzima ya mapishi. Ndugu zake wawili wa kike, mama pamoja na mke wake. Aliwapita bila kuwasemesha neno kuzunguka nyuma ambako zoezi zima la uchomaji wa nyama ulifanyika. “Kaka Damian…!” mdogo wake mpenzi mkubwa wa nyama alimuita. “Bado!” alijibu bila kugeuka akikijua kinachomfanya amuite. Watu wote mahali pale walicheka hata mdogo yule aliyemuita kaka yake. Kila mmoja moyoni mwake alijawa na furaha moyoni, amani ilitawala katika familia hiyo. Katika dakika zile alizotegemewa kufika Aidan, zilipita na masaa kusogea pasipo kuingia kwake mgeni mtarajiwa. Wasiwasi uliwashika baada ya kujaribu kupiga simu yake na kutokupatikana kabisa. Mawazo yalijaa kwa ndugu wale haswa kwa mama na watoto wake wakike walioonesha kuhofia usalama wake. Baba na kaka yao Damian walionesha utulivu wa hali ya juu labda ili kuweka utulivu na huenda walikuwa na udhaifu kwa ndani lakini hali yao ya nje iliwafanya wawe na imani kiasi. Muda ulivyozidi kwenda ndio imani ilizidi kupungua, jua nalo lilianza kuzama; vyakula vikianza kupoa na kuonesha mipango yote kuvurugika. Baba ya na Damian nao walianza kukubali kupoteza mchezo, eote wakionesha kufikia makubaliano kuwa kuna jambo limemkuta ndugu yao huyo na ni vyema kusikiliza kama kuna habari yeyote ya ajali. Ajali ndio lilikuwa amuzi lao wote kwakuwa alikuwa safarini. Aidan aliamka usingizini na kutazama saa yake ya mkononi iliyokuwa kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda kile baada ya kuona tayari kiza kimetanda katika chumba kile cha nyumba ya kupanga (apartment) aliyofikia. Mara moja alikurupuka kitandani baada ya kuona ni saa moja jioni na kukimbilia bafuni kwenye chumba hicho cha hoteli. Simu yake ilikuwa kwenye umeme akiwa anaichaji baada ya kuisha chaji kabisa. Alipotoka bafuni aliiwasha wakati akijiandaa ili kuweza kutoka huku akisikitika kwa kupitiwa huko baada ya kujilaza kidogo ili simu iingie chaji kidogo baada ya kuisha kabisa lakini kujikuta akipitiwa na usingizi kabisa. Simu ilimuonesha simu nyingi kutoka kwa wana-familia wake, angalau kila mmoja alijaribu kumpigia ili kujaribu bahati zao. Aliishia kusikitika akijiandaa haraka haraka ili asichelewe zaidi ya hapo, angalau apate nao chakula cha jioni ikiwa cha mchana alikikosa. Alivaa pensi yake ya kijivu na sendoz chini, juu akivaa fulana nyepesi yenye mistari meusi na meupe iliyopita kwa aina ya mlalo; akichukua simu yake, waletu pamoja na ufunguo wa gari katika meza ile na kutoka katika nyumba hiyo aliyofikia na moja kwa moja mpaka kwenye maegesho ya magari yaliyopo chini kabisa ya jengo hilo la ghorofa. Wakiwa wanatoka kwenda polisi, baba na kaka yake; katika gari la kaka yake, Damian; Ford Ranger nyeusi, mbele yao waliona gari lililokuwa likionesha kuingia ndani mule walipokuwa wanatoka wao; geti katikati yao, taa za gari zote zikimulikana, Damian aliteremka kutoka upande wa dereva, kulia, akimuacha baba yake ndani ya gari wakati huo huo, Aidan akiteremka kutoka kwenye gari lake aina ya Toyota Fortuner ya kijivu na kukutana na kaka yake mbele, katikati ya taa za magari hayo mawili. “Aaah… aaaah… aaah!” alipayuka Damian baada ya kugundua ni ndugu yake aliyekuwa mbele yake. “Daaah!!!” walikumbatiana kwa furaha ya kuonana. Mama na mabinti zake wakiwa barazani kwani ndani hapakukalika tena, walijiuliza kwa nini gari la Damian halikusogea getini na wakiona kuna taa zilimulika kuingia ndani kuonesha kulikuwa na gari nje wakati baba yao nae akiteremka kwenye gari lile na kusogea walipo wanae. Katika hali ya shukrani alifika na kuwakumbatia wote wawili pasipo kujali kama Damian alikuwa nae. Mama na mabinti zake kuona mume wake ameteremka na kama safari haikuendele walisogea eneo lile la getini na kukaribia kwao waligundua nje kulikuwa na gari. Binti yake mdogo, aliye wa mwisho kuzaliwa aligundua jambo kabla ya kufika getini na kuona kilichopo. “Nasikia harufu ya marashi ya Kaka Aidan!” alieleza kuonesha pua zake zilikuwa vizuri kunusa. “Mmmh…!!” aliguna dada yake wakimfanya wifi yao kucheka akiwa hana cha kusema.


```SIMULIZI:THE FORBIDDEN LOVE``` ```SEHEMU: YA PILI``` Mama aliendelea kutembea na safari hii mwendo ukiongezeka kulifikia geti na kabla ya kuona nje baada ya kufika; Damian aliingia ndani na kuwaona wakiwa mahali pale. “Amefika!” aliwavunjia habari hiyo akicheka kuonesha furaha huku wadogo zake wakirukaruka na kukumbatiana wakati mke wake akicheka pembeni na mama akionesha kutaka kumuona mwanae kuweza kuridhika. Aidan alimsogelea mama yake alipomuona na kumkumbatia wakati mama yake akiangua kilio kilichowafanya wengine wote kulalama wakimlaumu kwanini alie badala ya kufurahi. Mama hakujali. Mama alihitaji muda na mwanae wa pili baada ya muda mchache kudhani amepatwa na jambo baya lakini muda huo alikuwa mbeke yake tena akionesha kuwa mzima wa afya japo hakupata kumuona vizuri. Alimkumbatia akilia mikononi mwake huku Aidan akishangaa taharuki hiyo na kum’bembeleza Mama yake akicheka kwa mshangao ule alioupata nyumbani kwao. Baada ya kumtuliza Mama yake, alisalimiana na wadogo zake wawili wakike akikumbatiana nao vile ile wao wakiwa na furaha zaidi kumuona kuliko kilio. Aliingia ndani, gari lake likiwa eneo lile lile la getini wakati Damian tayari alirudisha gari lake sehemu ya maegesho. Aliporudi kufunga geti, aliliona gari la Aidan likiwa nje pale bado likimulika mwanga taa na wakati huo tayari ameingia ndani ya nyumba na wengine wote. Alisogea mpaka kwenye gari lile na kufungua mlango upande wa kulia wa dereva na kupanda kwenye gari hilo. Alitazama nyuma na kuona mizigo katika mifuko kadhaa na kutabasamu kisha kutoa gia kwenye maegesho akiweka kwenye gia ya kuendesha ‘D’ na kuliingiza ndani usawa mdogo mbele ya geti lile na kusimamisha gari kisha kuteremka na kurudi kufunga geti lile na ndipo kulipeleka gari lile kwenye maegesho ya magari, pembeni ya gari lake. “Umetutisha sana aisee, ilikuwa twende polisi hivi!” alizungumza Baba yake baada ya simanzi iliyotanda nyumbani hapo kupotea na furaha kurudi. “Aaah… sasa mlikuwa mnaenda kuwaeleza nini?” aliwadadisi akicheka wakati Damian akiingia sebuleni pale mkononi mwake akiwa na funguo mbili za magari. “Mimi nilikuwa nawaambia atakuja ila unawajua wazee wako!” alizungumza Damian akimkabidhi ufunguo wake wa gari uliokuwa katika muundo wa rimoti. “Aaah, wakati yeye ndiye aliyetuhamasisha tutoke!” Familia nzima ilicheka baada ya Baba kumfanya Damian kuwa ndiye aliyekuwa na wasiwasi kuliko wote. Mke wa Damian aliketi pembeni akiishia kucheka na kutazama familia ile furaha yao ikirudi kama ilivyokuwa awali kabla ya mumewe kwenda kuketi pembeni yake na kuushika mkono wake kulia katika kochi lile. “Aaah… daaah, shem!” alizungumza Aidan akinyanyuka kwenye kochi lile alilokua amekaa ambalo pembeni yake upande wa kulia akiwepo mama yake na upande wa kushoto mdogo wake wa mwisho. “Samahani aisee, mapokezi yamekuwa makubwa na taharuki ilinifanya tusionane vizuri aisee!” alisogea akimpatia mkono wake. “Hamna shida shem, karibu!” alijibu Mke wa Damian akitabasamu. “Ahsante, karibu na wewe katika familia!” “Ahsante sana!” alijibu wakiachiana mikono yao na Aidan kurudi alipokuwa ameketi. “Naam huyu ndio Aidan, kwa bahati mbaya sana kwenye harusi yetu hakuwepo, tangu andoke miaka kama saba iliyopita, leo ndio anarudi nyumbani!” alimueleza mke wake. “Nashukuru kukufahamu shem!” alizungumza kuonesha uchangamfu wake. “Eeh bhana, Bro! Huyu ndio wa ubavu; shemeji yako anaitwa Consolata!” alimueleza Aidan akiwa tayari amerudi alipokuwa ameketi. “Kwa mara nyingine, karibu kwenye familia, shem; nimefurahi kukuona!” alijibu. “Haya na wewe yuko wapi mwenza wako!?” Mama alimgeukia Aidan akimdadisi. “Yupo nje hapo hamjamuona!” aliwaeleza na kuwafanya wote wapate taharuki na kumshangaa. “Yupo wapi!?” waliuliza kwa pamoja. “Aaah, eti Kaka, hujauona!?” alimuuliza kaka yake akicheka. “Aaah… usiniuzie kesi; sijamuona!” alikataa akijitoa katika matatizo yanayoweza kujitokeza. Nyumba nzima walitoka nje na Aidan akiwaongoza mpaka kwenye maegesho ya magari. “Si huyu hapa!” aliwaeleza. “Yupo wapi!?” wote walidadisi wakikosa kuona mtu pale nje zaidi ya gari. “Aaah, jamani kwa uzuri wote huu alionao bado hamumuoni, au kwakuwa ni usiku!” alilalama akizidi kuwachanganya wao wakikosa kuona mtu. “Usiniambie anazungumzia kuhusu gari!?” Consolata alinong’ona kwa mume wake baada ya kuonesha kumuelewa Aidan alichomaanisha. “Sidhani!” alimpinga mke wake na yeye akiwa pamoja na familia yake kuendelea kumuangalia huyo anaezungumziwa. “Fortuner, eeh!?” alizungumza Consolata kwa sauti kumuuliza Aidan. “Naaam! Na sio tu Fortuner, sema Fortuner SRV, V6!” Alijibu akitaja muundo wa gari hilo. “… na naona wakwe mtapatana sana!” Wote walimgeukia Consolata aliyesimama pembeni ya mume wake na kumrudia Aidan. “Yaani una maanisha gari!?” Baba alimuuliza Aidan. “Sio tu gari, ni mwenza wangu huyu” alijibu na kufanya familia yake kurudi ndani wakimuacha mahali pale peke yake huku Consolata akicheka. Ghafla waliomsherehekea walimuacha mwenyewe, hakukuwa na mtu mahali pale wote wakirudi ndani na kubaki akishangaa. Ugeni uliisha mapema kabisa, haukudumu hata nusu saa ya kuwasili kwake.


```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA NNE``` Waliendelea kula na baada ya kumaliza aliketi sebuleni na baba yake kuzungumza machache kabla ya kwenda kulala. “Kesho nitaenda kusajili namba mpya ya mawasiliano!” alieleza Malaika kuweka wazi ratiba aliyokuwa nayo siku iliyofuata. “Ooh, sawa sawa; au nikuletee!?” alimuuliza akitaka kujua kama anaweza kumsaidia. “Sawa!” alijibu Malaika akionesha pia ndio alilokuwa anataka ila hakuweza kumuagiza baba yake. “Sawa, utavumilia kiasi, nikirudi jioni nitarudi nayo!” alimueleza. “Na kingine unachohitaji?” alimdadisi binti yake baada ya la mawasiliano kumalizana nalo. “Hapana!” alijibu Malaika. “Salio unalo la kutosha!?” alimuuliza kama ana pesa za matumizi. “Ndio baba, ninazo!” alijibu akitabasamu. “Sawa; kesho fundi atakuja kulifanyia ukaguzi gari lako na kuona kama kila kitu kipo sawa!” alimueleza. “Na kuhusu gari; leseni yako haijapita muda wake?” “Leseni ninayo ya kimataifa!” alijibu. “Ila ya nchini imemalizika muda wake muda sana!” “Sawa, ila itabidi tukaifungue!” “Sawa baba!” “Sawa, kesho alfajiri nina kikao, naona nikapumzike mapema!” alimuaga binti yake. “Sawa baba na mimi naelekea kupumzika!” “Sawa, usiku mwema!” alimauga akinyanyuka kuelekea chumbani kwake. “Na kwako pia baba!” Alibaki sebuleni pale licha ya kusema na yeye anaelekea kupumzika. Dakika chache na yeye alinyanyuka kwenye kochi lile kuelekea chumbani kwake. Kabla ya kupanda ngazi alisikia vyombo vikipangwa jikoni na kujua kuwa Angelina atakuwa huko. Moja kwa moja alielekea jikoni na kumkuta Angelina kama alivyotegemea akimalizia kuvifuta vyombo na kuvipanga katika makabati yake husika baada ya kuviosha. “Umemaliza tayari, hakuna cha kukusaidia!” alizungumza Malaika alipoingia jikoni mule. “Aaah, usijali; tayari nimemaliza!” alimjibu akitabasamu. “Haya sawa kama hutaki nikusaidie!” “Hamna dada, tayari nimemaliza!” alijibu Agelina. “Haya sawa, usiku mwema!” alimuaga akiamua kutoka jikoni humo. “Na kwako pia!” alimjibu na kabla hajatoka, Malaika alikumbuka jambo na kugeuka kumtazama Angelina aliyekuwa akiendelea na kazi yake. “Dada!” alimuita na kumfanya ageuke kumtazama. “Nashukuru sana kwa kumjali Baba, inaonesha umekuwa mtu wa muhimu sana maishani mwake, nakushukuru sana!” alimueleza na kumfanya Angelina akose cha kujibu akiishia kumtazama akiinama chini kama mwenye kuona aibu na Malaika kutoka jikoni mule. Angelina aliacha kufuta vyombo vile akitafakari maneno yale pasipo kujua maana ya Malaika ilikuwa ni ipi na kama yalikuwa maneno aliyomaanisha japo alionekana kumaanisha kila alilolisema na kujikuta akitabasamu. Malaika alipandisha chumbani kwake na kujilaza kitandani kwake akijiona rasmi amerudi nyumbani ambako hakuwepo kwa miaka mingi. Nyumbani palimpendeza ikiwa licha ya kutokuonana na Amon alijona kuwa na amani na furaha, katika jambo lolote hakuacha kutabasamu. Alipitiwa na usingizi na kutokana na uchovu aliokuwa nao hakutambua na kujikuta akiamka pakiwa tayari pamepambazuka. Baba yake tayari alikuwa ametoka kuelekea ila akimuachia maelezo kwenye karatasi aliyoipitisha chini ya mlango wa chumba chake na kuwa mbele ya mlango. Malaika aliiokota na kuisoma karatasi hiyo. ‘Samahani nimetoka bila kukusemesha, ila nadhani lilikuwa jambo la maana kwa uchovu ulipkuwa nao; tutaonana baadae na mpaka hapo Angelina atakuhudumia, kwa mahitaji yeyote usisite kumuambia!’ Ilisomeka hivyo karatasi hiyo aliyoisoma kabla ya kufungua mlango kutoka nje na kuamua kurudi kufungua dirisha lililomtoa nje katika baraza iliyokuwa nje ya chumba hicho, ghorofani (Balkoni).
