
Kalamu House
May 31, 2025 at 01:20 PM
```SIMULIZI: MALAIKA 2```
```SEHEMU: YA PILI```
Mwanamke wa miaka thelathini na tatu (33) sasa, hakuwa yule Malaika wa miaka ishirini na sita (26).
Kimuonekano alizidi kupendeza, umbo la namba nane, kiuno chembamba kilichoshikiliwa katika na miguu ya umbo la bia na mapaja yaliyotanuka pembeni kuzidisha mvuto kwake kwa kila aliyemuona. Urefu wa wastani katika rangi yake ya kahawia kuonesha asili yake ya watu weusi. Nje na muonekano aliokuwa nao, mtazamo wake wa maisha ulibadilika sana na vitu vingi alijifunza kipindi ambacho hakuwepo nyumbani, vitu vilivyomfanya ajione kuwa vingi hakuwa akijua au kutambua kuhusu maisha.
Kila alipopita mtaani kule watu walishangaa kuliona gari la aina ile maeneo yale, hayakuwa maeneo ambayo gari la aina ile kuonekana; hivyo iliwafanya kila mmoja kutoka kulitazama; likiwa la muonekano wa tofauti, lilivutia wengi walioliona na kutamani kumjua aliyekuwa akiendesha.
Alifika mpaka nje ya nyumba ile na kuteremka kwenye gari kila mmoja akitazama ni nani aliyekuwa akishuka huku ukitangulia mguu wa kulia kuteremka, mguu uliovutia kuashiria aliyeteremka alikuwa mlimbwende. Katika gauni fupi la kitambaa chepesi lililoishia magotini likiwa la maua, mguu ule ulionekana. Alifunga mlango wa gari na kusogea mlangoni mwa nyumba ile kila mmoja aliyemuona akijiuliza kama mwanamke huyo amepotea njia au kuwa mahali sahihi.
Alishusha pumzi akitambua kuwa watu wanamtazama na kutokuwajali akisogea mlangoni pale na kabla kubisha hodi alitoka mwanamke mmoja.
“Habari yako dada!” alimsalimu mwanamke huyo.
“Nzuri!” alijibu akimtazama kutoka juu mpaka chini na kurudia tena mara ya pili akimshangaa.
“Samahani; kuna mtu namuulizia!” alianza kueleza hitaji lake.
“Humu ndani?” alijibu mwanamke yule kuonesha katika hali ya kutokuamini mwanamke kama yeye amuulizie mtu wa maeneo yale.
“Ndio!” alijibu Malaika.
“Nani!?” alimuuliza akimtazama kwa shauku jubwa ya kutaka kujua.
“Anaitwa Amon!” alijibu Malaika mapiga yake ya moyo yakienda mbio.
“Amon??” aliuliza mara ya pili akionesha kutokumuelewa.
“Ndio!” alithibitisha.
“Mmmh… hakuna mtu anaitwa Amon hapa!” alijibu wakati huo majirani kadhaa walioshindwa kuvumilia walisogea karibu na nyumba ile.
“Wee, mama Zuu, anamuulizia nani?” jirani mmoja aliuliza.
“Anamuulizia, nani vile umesema!?” alimgeukia tena kumuuliza ikiwa tayari alisahau jina alilotajiwa.
“Amon, namuulizia Amon!” alijibu akiwaeleza kwa sauti na wale waliofika karibu yao.
“Mmmh, mbona hatumjui!” Alijibu yule jirani aliyesogea kuuliza.
“Hamuwezi kumjua, alihama zamani sana!” sauti moja ya Mzee aliyekuwa anapita njia ilisikika ikiwaeleza.
“Mmmh… mzee Bakari na wewe hupitwi!” alizungumza yule aliyekuwa akizungumza na Malaika mlangoni pale.
“Samahani mzee wangu!” Malaika aliondoka pale upesi akimfuata baada ya kuona nuru ambapo tayari alipoteza matumaini.
“Unaweza kujua alipohamia!?” alimdadisi.
“Sijui, miaka mingi imepita bila kusikia lolote wala kumuona!” alijibu akizidi kupoteza matumaini yeyote aliyokuwa nayo Malaika.
“Naomba unisaidie mzee wangu, tafadhali!” alijaribu kum’bembeleza.
“Mmmh… sijui, jaribu kuulizia ulizia, ila sio huku mtaani!” maelezo hayo yalimfanya akose kujua pa kuanzia zoezi likizidi kuwa gumu zaidi ya lilivyokuwa.
“Nitamuulizia wapi?” aliuliza ikiwa ndio swali lililokuwa kichwani mwake.
Mzee yule alimtazama akimuona amekosa matumaini na kumhurumia.
“Twende nikupeleke!” alimueleza akimpa wazo alilokuwa nalo.
“Sawa, twende!” bila kufikiria zaidi, Malaika aliona hana cha kupoteza.
Mzee yule aliingia kwenye gari na Malaika kuzunguka upande wa pili kisha akiwasha gari na kuondoka mahali pale akiongozana na mzee yule huku wale waliosogea katika nyumba ile wakibaki kushangaa na kuangusha kicheko cha umbea na unafiki. Walitoka nje ya mitaa ile na kurudi maeneo ya mjini.
“Egesha gari hapo pembeni!” alimuagiza Malaika na Malaika kufuata maagizo hayo.
“Wewe ni mgeni!?” alimdadisi baada ya kusimamisha gari.
“Ni muda tangu niondoke huku, ndio nimerejea!” alijibu Malaika.
“Ndio maana!” alijibu.
“Kwanza kabisa, hutakiwi kumuamini mtu haswa kwa mwanamke kama wewe!” alizungumza Mzee yule maneno yaliyoanza kumpa wasiwasi Malaika.
“Kwanini!?” alidadisi huku akiwa na hofu.
“Maisha tofauti na yalivyokuwa zamani, pale tayari watu walikuwa wakupangie njama na nilichokusaidia ni kukuokoa; mitaa kama ile wenzako hawathubutu kusogea kabisa!” alimueleza akimtisha sana Malaika.
“Sasa nawezaje kumpata Amon!?” alimdadisi akirudi kwenye hitaji lake.
“Nilipata habari kuwa maisha yake yamebadilika sana hivyo huwezi kumpata uswahilini!” alimueleza.
“Nitampata wapi!?”
“Kuna uwezekano ukaonana nae huko huko kwenu, maeneo ambayo nyie hukutana, ndio maeneo unaweza kumkuta na yeye au angalau kumuulizia!” alimjibu akimpa namna nyingine ambayo haikuingia akilini.
“Mmmh…!” alikosa cha kusema maneno yakimuisha na kubaki kujiona amefika ukingo wa kuonana na Amon.
“Ila kuwa makini sana, kuwa makini na maeneo yale; nakuomba sana!” alimueleza akifungua mlango wa gari lile kutaka kuteremka.
“Samahani Baba!” alimsimamisha kabla hajateremka na kumfanya afunge mlango.
“Chukua hii nauli ya kurudia, na ahsante sana!” alimpatia shilingi elfu hamsini kutoka kwenye pochi yake.
“Ahsante sana!” aliipokea pesa ile akitabasamu na kuteremka kwenye gari lile.

❤️
1