Kalamu House
Kalamu House
June 1, 2025 at 02:04 PM
```SIMULIZI: MALAIKA 2``` ```SEHEMU: YA TATU``` Malaika alibaki mahali pale kwa muda kabla ya kuondoka na kuamua kurudi nyumbani akijua mpango aliokuwa nao siku hiyo haukufanikiwa. Aliingia katika hali ya unyonge kutokufanikiwa ila bado aliweka uso wa furaha usoni mwake ili kuondoa maswali yeyote kwa baba yake. “Vipi umefanikiwa kuonana na huyo mtu!?” alimdadisi baada ya Malaika kuingia ndani. “Naweza kusema nimefanikiwa japo sijamuona!” alijibu akitabasamu. “Oooh… angalau kama jambo limefanikiwa!” alifurahi kusikia hivyo kuwa binti yake ameonesha kufanikiwa. “Angelina!” aliita baba yake Malaika huku Malaika akijiuliza ni nani aliyeitwa. “Abee!” sauti ya kike iliitika kutoka jikoni. “Unamfahamu!?” alimuuliza baada ya kufika sebuleni pale walipokuwa. “Hapana!” alijibu akitikisa kihwa kuweka msisitizo. “Huyu ndiye Malaika!” alimtambulisha kwake Malaika aliyekuwa akitabasamu pale kwenye kochi alipokuwa ameketi. “Malaika, huyu ndiye anaenilea angalau umenikuta katika afya nzuri!” alimgeukia Malaika na kumtambulisha. “Oooh… nakuona hata umezidi kunawiri!” alimsifu muonekano wake. “Basiii, hiyo ndio kazi ya Angelina na kwa bahati nzuri anajina kama lako tu, wote ni Malaika wangu!” alijibu akitabasamu kuonesha thamani ya wanawake wale. “Nashukuru kukufahamu dada!” Angelina alizungumza akimtazama Malaika kwa tabasamu. “Na mimi pia, nashukuru kukufahamu!” alijibu Malaika akirudisha tabasamu kwake. “So Malaika, umerudi moja kwa moja, si ndio!?” aliuliza baba yake akitaka kujua ujio huwa wa ghafla wa binti yake ni ule wa moja kwa moja au wa dharura. “Nimerudi moja kwa moja, baba!” alijibu Malaika wakati Angelina akiwa tayari ameondoka. “Nadhani nichukue likizo yangu kabla ya kustaafu kabisa!” bila kupoteza muda aliweka wazi hitaji la moyo wake kwa mwanae. “Mmmh… baba, bado mapema; kampuni inakuhitaji!” “Mapema ndio vizuri!” alijibu akionesha tayari kuamua. “Nahitaji muda kidogo lakini!” Malaika bado alionesha kipingamizi cha kuchukua nafasi ya baba yake. “Muda ndio haupo!” Bado baba yake alisimamia maamuzi yake akinyanyuka kwenye kochi lile akielekea chumbani. Malaika nae alipanda chumbani kwake akienda kubadilisha na kuoga kabisa kisha baada ya kutoka bafuni na kuvaa mavazi ya kulalia, alijilaza kitandani akiwaza namna anaweza kumpata Amon. Alijiuliza ni mangapi yamempita wakati hayupo na Mzee yule alimaanisha nini kumwambia ataonana nae kwao; na ni maeneo yapi ambayo wanakutana! Maswali yalimtatiza akiwaza kama Mzee yule alikuwa akimdanganya au kumueleza ukweli. “Dada, chakula tayari!” aligongewa akiwa chumbani kwake. “Ahsante!” aliitika akiendelea kuwazua namna anaweza akampata Amon. Mawasiliano alionesha kupoteza ikiwa hata namba zake hakuwa nazo huku yeye mwenyewe akiwa bado hana namba ya mawasiliano ya mtandao wa simu wa nchini akitumia mtandao wa kijamii na intaneti (Wi-Fi). Mpango aliokuwa nao ni kusajili namba mpya ya mawasiliano kwake atakayokuwa akiitumia siku ikipambazuka haswa baada ya muda huo kiza kutanda. Aliteremka chini kwenda kupata chakula na baba yake akiwa na Angelina ambao wote walikaa meza moja kitu ambacho kidogo kilimfanya Malaika ajiulize ila kushindwa kusema neno au kuonesha utofauti wowote. Katika meza iliyo ndefu yenye viti nane, vitatu kila upande wa urefu na kimoja katika kila mapana. Kiti cha mapana alikalia baba yake wakati upande wa kushoto akiwa Angelina na kulia kwake kwenda kuketi Malaika akiwa anatazamana na Angelina. Ni muda sana tangu kuwa hivyo wakipata chakula pamoja, hata katika uwepo wake hapo nyuma, hakuwa akiketi na baba yake; labda ni kwa ajili ya ujio wake. “Unaonekana unafuraha sana baba!” Malaika alimdadisi baba yake akimtazama. “Lazima nifurahi, binti yangu upo hapa; kwanini nisijawe na furaha!?” alijibu. “Aaah… hii furaha sio ya siku moja, hata nilipokuwa nikiongea na wewe; sauti yako ilijawa na furaha!” aliendelea kumdadisi akimtazama Angelina aliyekuwa ameinamisha kichwa chake kwenye sahani yake wakati baba yake akitazama mwisho wa meza ile kwenye kiti kilichomuangalia. “Usipojawa na furaha katika haya maisha, utafurahi lini!?” alijibu akigeuza shingo kumtazama Malaika akitabasamu. “Haya bhana!” alijibu akiamua kuyamaliza mazungumzo hayo. “Mmmh, chakula kitamu sana; nilikumbuka sana ladha ya chakula cha nyumbani!” alikisifia chakula baada ya kula kijiko kimoja tu. “Kazi ya Angel hiyo, mpishi mzuri sana; hii nayo ni sababu ya kuwa na furaha!” alijibu Baba yake akimsifia Angelina. Malaika alihisi jambo lisiloeleweka, furaha ya baba yake na hali aliyomkuta ya uchangamfu, afya iliyonawiri; ilioneshwa alipata matunzo mazuri. Mara ya mwisho Baba yake kuwa katika hali nzuri ni kipindi cha uhai wa mama yake ndio alikuwa hivyo na furaha pamoja na kunawiri, ila baada ya Mama yake kufariki, hakuwahi kuuona uchangamfu wa baba yake mara kwa mara, na hata alipokuwa akirudi nyumbani kutoka masomoni bado hakuwa na furaha hiyo; labda ni kweli kwasababu yake kwakuwa alichukua muda sana nje bila kurudi nyumbani; atatambua mbeleni, uzuri yupo hapo kuishi.
Image from Kalamu House: ```SIMULIZI: MALAIKA 2```  ```SEHEMU: YA TATU```  Malaika alibaki maha...
❤️ 1

Comments