
Kalamu House
June 2, 2025 at 02:02 PM
```SIMULIZI: THE FORBIDDEN LOVE```
```SEHEMU: YA KWANZA```
Aidan bado hajaingia!?” Aliuliza Baba yao baada ya kutoka dukani alikokwenda kuchukua baadhi ya vitu.
“Nadhani hata chukua muda sana!” Alijibu mwanae wa kiume, kaka yake na Aidan aliyetazama saa yake ya mkononi iliyokuwa katika mfuko wake wa suruali na kuona ni karibu na majira aliyosema.
“Saa ngapi?” Alimuuliza akitaka kujua ni muda gani wa kumtarajia.
“Sasa ni saa kumi kasoro, kwa maelezo yake; saa kumi kamili mpaka narobo hivi atakuwa hapa!” Alimjibu baba yake.
“Sawa!”
“Mbuzi tayari umeshammaliza!?” Alimuuliza mwanae huyo ambae alikuwa na jukumu la kumtengeneza mbuzi.
“Naelekea kwenda kumuandaa sasa hivi, tayari nimeshamaliza kuchuna ngozi!” alijibu akiirudisha mfukoni alipoitoa na kuchukua mizigo ile aliyokuja nayo baba yake na kuelekea nayo mpaka jikoni akiweka chupa zile za vinywaji mbalimbali katika jokofu.
Wanawake walikuwa nje wakishughulika na mapishi huko; siku hiyo jiko la ndani halikutumika kutokana na ukubwa wa siku na umuhimu wake.
Baada ya kuweka vinywaji vile, alifungua mlango wa jikoni wa nyuma na kuwaona wanawake wakiwa huko na hekaheka nzima ya mapishi. Ndugu zake wawili wa kike, mama pamoja na mke wake.
Aliwapita bila kuwasemesha neno kuzunguka nyuma ambako zoezi zima la uchomaji wa nyama ulifanyika.
“Kaka Damian…!” mdogo wake mpenzi mkubwa wa nyama alimuita.
“Bado!” alijibu bila kugeuka akikijua kinachomfanya amuite.
Watu wote mahali pale walicheka hata mdogo yule aliyemuita kaka yake. Kila mmoja moyoni mwake alijawa na furaha moyoni, amani ilitawala katika familia hiyo.
Katika dakika zile alizotegemewa kufika Aidan, zilipita na masaa kusogea pasipo kuingia kwake mgeni mtarajiwa. Wasiwasi uliwashika baada ya kujaribu kupiga simu yake na kutokupatikana kabisa.
Mawazo yalijaa kwa ndugu wale haswa kwa mama na watoto wake wakike walioonesha kuhofia usalama wake. Baba na kaka yao Damian walionesha utulivu wa hali ya juu labda ili kuweka utulivu na huenda walikuwa na udhaifu kwa ndani lakini hali yao ya nje iliwafanya wawe na imani kiasi.
Muda ulivyozidi kwenda ndio imani ilizidi kupungua, jua nalo lilianza kuzama; vyakula vikianza kupoa na kuonesha mipango yote kuvurugika.
Baba ya na Damian nao walianza kukubali kupoteza mchezo, eote wakionesha kufikia makubaliano kuwa kuna jambo limemkuta ndugu yao huyo na ni vyema kusikiliza kama kuna habari yeyote ya ajali. Ajali ndio lilikuwa amuzi lao wote kwakuwa alikuwa safarini.
Aidan aliamka usingizini na kutazama saa yake ya mkononi iliyokuwa kwenye meza ndogo pembeni ya kitanda kile baada ya kuona tayari kiza kimetanda katika chumba kile cha nyumba ya kupanga (apartment) aliyofikia.
Mara moja alikurupuka kitandani baada ya kuona ni saa moja jioni na kukimbilia bafuni kwenye chumba hicho cha hoteli.
Simu yake ilikuwa kwenye umeme akiwa anaichaji baada ya kuisha chaji kabisa.
Alipotoka bafuni aliiwasha wakati akijiandaa ili kuweza kutoka huku akisikitika kwa kupitiwa huko baada ya kujilaza kidogo ili simu iingie chaji kidogo baada ya kuisha kabisa lakini kujikuta akipitiwa na usingizi kabisa.
Simu ilimuonesha simu nyingi kutoka kwa wana-familia wake, angalau kila mmoja alijaribu kumpigia ili kujaribu bahati zao.
Aliishia kusikitika akijiandaa haraka haraka ili asichelewe zaidi ya hapo, angalau apate nao chakula cha jioni ikiwa cha mchana alikikosa.
Alivaa pensi yake ya kijivu na sendoz chini, juu akivaa fulana nyepesi yenye mistari meusi na meupe iliyopita kwa aina ya mlalo; akichukua simu yake, waletu pamoja na ufunguo wa gari katika meza ile na kutoka katika nyumba hiyo aliyofikia na moja kwa moja mpaka kwenye maegesho ya magari yaliyopo chini kabisa ya jengo hilo la ghorofa.
Wakiwa wanatoka kwenda polisi, baba na kaka yake; katika gari la kaka yake, Damian; Ford Ranger nyeusi, mbele yao waliona gari lililokuwa likionesha kuingia ndani mule walipokuwa wanatoka wao; geti katikati yao, taa za gari zote zikimulikana, Damian aliteremka kutoka upande wa dereva, kulia, akimuacha baba yake ndani ya gari wakati huo huo, Aidan akiteremka kutoka kwenye gari lake aina ya Toyota Fortuner ya kijivu na kukutana na kaka yake mbele, katikati ya taa za magari hayo mawili.
“Aaah… aaaah… aaah!” alipayuka Damian baada ya kugundua ni ndugu yake aliyekuwa mbele yake.
“Daaah!!!” walikumbatiana kwa furaha ya kuonana.
Mama na mabinti zake wakiwa barazani kwani ndani hapakukalika tena, walijiuliza kwa nini gari la Damian halikusogea getini na wakiona kuna taa zilimulika kuingia ndani kuonesha kulikuwa na gari nje wakati baba yao nae akiteremka kwenye gari lile na kusogea walipo wanae.
Katika hali ya shukrani alifika na kuwakumbatia wote wawili pasipo kujali kama Damian alikuwa nae.
Mama na mabinti zake kuona mume wake ameteremka na kama safari haikuendele walisogea eneo lile la getini na kukaribia kwao waligundua nje kulikuwa na gari.
Binti yake mdogo, aliye wa mwisho kuzaliwa aligundua jambo kabla ya kufika getini na kuona kilichopo.
“Nasikia harufu ya marashi ya Kaka Aidan!” alieleza kuonesha pua zake zilikuwa vizuri kunusa.
“Mmmh…!!” aliguna dada yake wakimfanya wifi yao kucheka akiwa hana cha kusema.

❤️
1