
Kalamu House
June 4, 2025 at 03:34 PM
```SIMULIZI:THE FORBIDDEN LOVE```
```SEHEMU: YA PILI```
Mama aliendelea kutembea na safari hii mwendo ukiongezeka kulifikia geti na kabla ya kuona nje baada ya kufika; Damian aliingia ndani na kuwaona wakiwa mahali pale.
“Amefika!” aliwavunjia habari hiyo akicheka kuonesha furaha huku wadogo zake wakirukaruka na kukumbatiana wakati mke wake akicheka pembeni na mama akionesha kutaka kumuona mwanae kuweza kuridhika.
Aidan alimsogelea mama yake alipomuona na kumkumbatia wakati mama yake akiangua kilio kilichowafanya wengine wote kulalama wakimlaumu kwanini alie badala ya kufurahi.
Mama hakujali. Mama alihitaji muda na mwanae wa pili baada ya muda mchache kudhani amepatwa na jambo baya lakini muda huo alikuwa mbeke yake tena akionesha kuwa mzima wa afya japo hakupata kumuona vizuri. Alimkumbatia akilia mikononi mwake huku Aidan akishangaa taharuki hiyo na kum’bembeleza Mama yake akicheka kwa mshangao ule alioupata nyumbani kwao.
Baada ya kumtuliza Mama yake, alisalimiana na wadogo zake wawili wakike akikumbatiana nao vile ile wao wakiwa na furaha zaidi kumuona kuliko kilio.
Aliingia ndani, gari lake likiwa eneo lile lile la getini wakati Damian tayari alirudisha gari lake sehemu ya maegesho.
Aliporudi kufunga geti, aliliona gari la Aidan likiwa nje pale bado likimulika mwanga taa na wakati huo tayari ameingia ndani ya nyumba na wengine wote. Alisogea mpaka kwenye gari lile na kufungua mlango upande wa kulia wa dereva na kupanda kwenye gari hilo. Alitazama nyuma na kuona mizigo katika mifuko kadhaa na kutabasamu kisha kutoa gia kwenye maegesho akiweka kwenye gia ya kuendesha ‘D’ na kuliingiza ndani usawa mdogo mbele ya geti lile na kusimamisha gari kisha kuteremka na kurudi kufunga geti lile na ndipo kulipeleka gari lile kwenye maegesho ya magari, pembeni ya gari lake.
“Umetutisha sana aisee, ilikuwa twende polisi hivi!” alizungumza Baba yake baada ya simanzi iliyotanda nyumbani hapo kupotea na furaha kurudi.
“Aaah… sasa mlikuwa mnaenda kuwaeleza nini?” aliwadadisi akicheka wakati Damian akiingia sebuleni pale mkononi mwake akiwa na funguo mbili za magari.
“Mimi nilikuwa nawaambia atakuja ila unawajua wazee wako!” alizungumza Damian akimkabidhi ufunguo wake wa gari uliokuwa katika muundo wa rimoti.
“Aaah, wakati yeye ndiye aliyetuhamasisha tutoke!” Familia nzima ilicheka baada ya Baba kumfanya Damian kuwa ndiye aliyekuwa na wasiwasi kuliko wote.
Mke wa Damian aliketi pembeni akiishia kucheka na kutazama familia ile furaha yao ikirudi kama ilivyokuwa awali kabla ya mumewe kwenda kuketi pembeni yake na kuushika mkono wake kulia katika kochi lile.
“Aaah… daaah, shem!” alizungumza Aidan akinyanyuka kwenye kochi lile alilokua amekaa ambalo pembeni yake upande wa kulia akiwepo mama yake na upande wa kushoto mdogo wake wa mwisho.
“Samahani aisee, mapokezi yamekuwa makubwa na taharuki ilinifanya tusionane vizuri aisee!” alisogea akimpatia mkono wake.
“Hamna shida shem, karibu!” alijibu Mke wa Damian akitabasamu.
“Ahsante, karibu na wewe katika familia!”
“Ahsante sana!” alijibu wakiachiana mikono yao na Aidan kurudi alipokuwa ameketi.
“Naam huyu ndio Aidan, kwa bahati mbaya sana kwenye harusi yetu hakuwepo, tangu andoke miaka kama saba iliyopita, leo ndio anarudi nyumbani!” alimueleza mke wake.
“Nashukuru kukufahamu shem!” alizungumza kuonesha uchangamfu wake.
“Eeh bhana, Bro! Huyu ndio wa ubavu; shemeji yako anaitwa Consolata!” alimueleza Aidan akiwa tayari amerudi alipokuwa ameketi.
“Kwa mara nyingine, karibu kwenye familia, shem; nimefurahi kukuona!” alijibu.
“Haya na wewe yuko wapi mwenza wako!?” Mama alimgeukia Aidan akimdadisi.
“Yupo nje hapo hamjamuona!” aliwaeleza na kuwafanya wote wapate taharuki na kumshangaa.
“Yupo wapi!?” waliuliza kwa pamoja.
“Aaah, eti Kaka, hujauona!?” alimuuliza kaka yake akicheka.
“Aaah… usiniuzie kesi; sijamuona!” alikataa akijitoa katika matatizo yanayoweza kujitokeza.
Nyumba nzima walitoka nje na Aidan akiwaongoza mpaka kwenye maegesho ya magari.
“Si huyu hapa!” aliwaeleza.
“Yupo wapi!?” wote walidadisi wakikosa kuona mtu pale nje zaidi ya gari.
“Aaah, jamani kwa uzuri wote huu alionao bado hamumuoni, au kwakuwa ni usiku!” alilalama akizidi kuwachanganya wao wakikosa kuona mtu.
“Usiniambie anazungumzia kuhusu gari!?” Consolata alinong’ona kwa mume wake baada ya kuonesha kumuelewa Aidan alichomaanisha.
“Sidhani!” alimpinga mke wake na yeye akiwa pamoja na familia yake kuendelea kumuangalia huyo anaezungumziwa.
“Fortuner, eeh!?” alizungumza Consolata kwa sauti kumuuliza Aidan.
“Naaam! Na sio tu Fortuner, sema Fortuner SRV, V6!” Alijibu akitaja muundo wa gari hilo.
“… na naona wakwe mtapatana sana!”
Wote walimgeukia Consolata aliyesimama pembeni ya mume wake na kumrudia Aidan.
“Yaani una maanisha gari!?” Baba alimuuliza Aidan.
“Sio tu gari, ni mwenza wangu huyu” alijibu na kufanya familia yake kurudi ndani wakimuacha mahali pale peke yake huku Consolata akicheka.
Ghafla waliomsherehekea walimuacha mwenyewe, hakukuwa na mtu mahali pale wote wakirudi ndani na kubaki akishangaa. Ugeni uliisha mapema kabisa, haukudumu hata nusu saa ya kuwasili kwake.

❤️
1