
Kalamu House
June 6, 2025 at 05:14 PM
```SIMULIZI: MALAIKA 2```
```SEHEMU: YA NNE```
Waliendelea kula na baada ya kumaliza aliketi sebuleni na baba yake kuzungumza machache kabla ya kwenda kulala.
“Kesho nitaenda kusajili namba mpya ya mawasiliano!” alieleza Malaika kuweka wazi ratiba aliyokuwa nayo siku iliyofuata.
“Ooh, sawa sawa; au nikuletee!?” alimuuliza akitaka kujua kama anaweza kumsaidia.
“Sawa!” alijibu Malaika akionesha pia ndio alilokuwa anataka ila hakuweza kumuagiza baba yake.
“Sawa, utavumilia kiasi, nikirudi jioni nitarudi nayo!” alimueleza.
“Na kingine unachohitaji?” alimdadisi binti yake baada ya la mawasiliano kumalizana nalo.
“Hapana!” alijibu Malaika.
“Salio unalo la kutosha!?” alimuuliza kama ana pesa za matumizi.
“Ndio baba, ninazo!” alijibu akitabasamu.
“Sawa; kesho fundi atakuja kulifanyia ukaguzi gari lako na kuona kama kila kitu kipo sawa!” alimueleza.
“Na kuhusu gari; leseni yako haijapita muda wake?”
“Leseni ninayo ya kimataifa!” alijibu.
“Ila ya nchini imemalizika muda wake muda sana!”
“Sawa, ila itabidi tukaifungue!”
“Sawa baba!”
“Sawa, kesho alfajiri nina kikao, naona nikapumzike mapema!” alimuaga binti yake.
“Sawa baba na mimi naelekea kupumzika!”
“Sawa, usiku mwema!” alimauga akinyanyuka kuelekea chumbani kwake.
“Na kwako pia baba!” Alibaki sebuleni pale licha ya kusema na yeye anaelekea kupumzika.
Dakika chache na yeye alinyanyuka kwenye kochi lile kuelekea chumbani kwake. Kabla ya kupanda ngazi alisikia vyombo vikipangwa jikoni na kujua kuwa Angelina atakuwa huko. Moja kwa moja alielekea jikoni na kumkuta Angelina kama alivyotegemea akimalizia kuvifuta vyombo na kuvipanga katika makabati yake husika baada ya kuviosha.
“Umemaliza tayari, hakuna cha kukusaidia!” alizungumza Malaika alipoingia jikoni mule.
“Aaah, usijali; tayari nimemaliza!” alimjibu akitabasamu.
“Haya sawa kama hutaki nikusaidie!”
“Hamna dada, tayari nimemaliza!” alijibu Agelina.
“Haya sawa, usiku mwema!” alimuaga akiamua kutoka jikoni humo.
“Na kwako pia!” alimjibu na kabla hajatoka, Malaika alikumbuka jambo na kugeuka kumtazama Angelina aliyekuwa akiendelea na kazi yake.
“Dada!” alimuita na kumfanya ageuke kumtazama.
“Nashukuru sana kwa kumjali Baba, inaonesha umekuwa mtu wa muhimu sana maishani mwake, nakushukuru sana!” alimueleza na kumfanya Angelina akose cha kujibu akiishia kumtazama akiinama chini kama mwenye kuona aibu na Malaika kutoka jikoni mule.
Angelina aliacha kufuta vyombo vile akitafakari maneno yale pasipo kujua maana ya Malaika ilikuwa ni ipi na kama yalikuwa maneno aliyomaanisha japo alionekana kumaanisha kila alilolisema na kujikuta akitabasamu.
Malaika alipandisha chumbani kwake na kujilaza kitandani kwake akijiona rasmi amerudi nyumbani ambako hakuwepo kwa miaka mingi. Nyumbani palimpendeza ikiwa licha ya kutokuonana na Amon alijona kuwa na amani na furaha, katika jambo lolote hakuacha kutabasamu.
Alipitiwa na usingizi na kutokana na uchovu aliokuwa nao hakutambua na kujikuta akiamka pakiwa tayari pamepambazuka. Baba yake tayari alikuwa ametoka kuelekea ila akimuachia maelezo kwenye karatasi aliyoipitisha chini ya mlango wa chumba chake na kuwa mbele ya mlango. Malaika aliiokota na kuisoma karatasi hiyo.
‘Samahani nimetoka bila kukusemesha, ila nadhani lilikuwa jambo la maana kwa uchovu ulipkuwa nao; tutaonana baadae na mpaka hapo Angelina atakuhudumia, kwa mahitaji yeyote usisite kumuambia!’ Ilisomeka hivyo karatasi hiyo aliyoisoma kabla ya kufungua mlango kutoka nje na kuamua kurudi kufungua dirisha lililomtoa nje katika baraza iliyokuwa nje ya chumba hicho, ghorofani (Balkoni).

❤️
1