DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
June 11, 2025 at 08:41 PM
*MASOMO YA MISA, JUNI 12 2025.* *ALHAMISI YA JUMA LA KUMI, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA C(I).* *RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI💚* *SOMO LA KWANZA* Mungu ameng’ara mioyoni mwetu ili kutupa nuru ya ufahamu wa utukufu wake. *Somo katika barua ya pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (2 WAKORINTHO 3: 15 — 4: 1, 3 — 6)* Ndugu: Hadi leo hii, kila mara maandiko ya Musa yanaposomwa, pazia linakuwa juu ya akili za Waisraeli; lakini pale mtu anapomgeukia Bwana, pazia hilo linaondolewa. Sasa, Bwana ni Roho, na penye Roho wa Bwana, ndipo penye uhuru. Sisi sote tusio na pazia usoni tunaouona utukufu wa Bwana, tunafananishwa na sura yake, tunaongezewa utukufu baada ya utukufu; kwa maana utukufu huu unatoka kwa Bwana aliye Roho. Kwa hiyo, sisi tuliyokabidhiwa huduma hii kwa huruma ya Mungu, tusife moyo. Ingawaje injili yetu si dhahiri, si dhahiri kwa wale tu wenye kupotea, kwa maana mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili za watu wasiosadiki, ili wasiweze kuiona nuru ya injili ya utukufu wa Kristo, aliye sura ya Mungu. Kwa maana hatutangazi habari zetu sisi wenyewe, bali tunatangaza habari za Kristo Yesu aliye Bwana, na sisi ni watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. Kwani Mungu aliyesema, “Mwanga ung’ae kutoka gizani,” ndiye yeye anayeng’aa mioyoni mwetu tupate kwa mwanga wake kuutambua utukufu wa Mungu uliopo usoni mwa Yesu Kristo. *Neno la Bwana…....* *Tumshukuru Mungu.* *ZABURI YA KUITIKIZANA* Zaburi 85: 9ab, na 10, 11 — 12, 13 — 14 (K) 10b *K. Utukufu wake utakaa katika nchi yetu.* Nitasikiliza anayonena Bwana Mungu; hakika, ananena kuhusu amani. Wokovu wake ni karibu nao wenye kumcha, utukufu wake utakaa katika nchi yetu. *K.* Upendo na uaminifu vimekutana; haki na amani zimebusiana. Uaminifu utachipuka katika nchi, na haki itachungulia kutoka mbinguni. *K.* Naam, Bwana atatoa yaliyo mema, na nchi yetu itatoa mazao yake. Haki aitatangulia mbele ya Bwana, na kuziongoza hatua zake njiani. *K.* *SHANGILIO LA INJILI* Yohane 13: 34 *K. Aleluya. W. Aleluya.* K. Amri mpya nawapeni, asema Bwana, mpendane, kama mimi nilivyowapenda. *W. Aleluya.* *INJILI* Mtu anayemkasirikia ndugu yake anastahili kushtakiwa. *† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo (MATHAYO 5: 20 — 26)* Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Nawaambieni, uadilifu wenu usipozidi ule wa Waandishi na wa Mafarisayo, hamtaingia katika ufalme wa mbingu. Mmesikia ya kuwa watu wa kale waliambiwa ‘Usiue; na mtu akiua, astahili kustakiwa.’ Mimi nawaambieni, hata mtu anayemkasirikia ndugu yake anastahili kushtakiwa. Amwambiaye ndugu yake, ‘Raka,’ astahili kesi katika baraza kuu la wazee. Amwambiaye ‘Mjinga,’ anastahili moto wa Jehanamu. Basi, ukipeleka sadaka yako kwenye altare, na hapo ukakumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno nawe, acha sadaka yako hapo mbele ya altare, nenda kwanza ukapatane na ndugu yako. Kisha rudi kutoa sadaka yako. Usikawie kupatana na mshitaki wako uwapo bado njiani naye, asije akakutoa kwa hakimu, na hakimu akutoe kwa tarishi, naye akakutupa gerezani. Amin, nakuambia, hutoki humo hadi utakapokuwa umelipa senti ya mwisho. *INJILI YA BWANA…...* *Sifa Kwako Ee Kristo*
Image from DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS: *MASOMO YA MISA, JUNI 12 2025.*  *ALHAMISI YA JUMA LA KUMI, KIPINDI CH...

Comments