KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
June 2, 2025 at 10:11 AM
*ELIMU ILIYOTUKIMBIZA NYUMBANI* _Kizazi Kilichodharau Shamba, Kikakimbilia Ajira Isiyolipa Kodi_ _“Wanangu, someni muajiriwe… msije mkaishia kuwa kama mimi na baba yenu… Kulima ni kugumu mno, si unaona leo? Tokea asubuhi tuko shambani hadi sasa hivi ndo tunarudi.”_ Maneno haya yaliingia na kuandikwa kwenye mioyo ya watoto wake *Amani, Roja, na Milembe* kama alama ya udhalili isiyoonekana. *Bi Nuru, mama yao,* aliwaambia akiwa amejifunga khanga kiunoni, miguu na mikono vikiwa vimejaa mavumbi ya Mkalaini, kijiji kidogo kilichojificha chini ya jua la Kwimba, mkoani Mwanza. Siku hiyo walikuwa wanarudi kutoka shambani, majani ya viazi (malando) yakiwa bado yananing’inia kwenye matoroli ya miti waliyokuwa nayo. Wakati huo huo, mamia ya kilomita kusini, huko *Njombe, kijiji cha Ukalawa, Bi Ndelwa* naye alikuwa anabeba mapipa ya pombe ya kienyeji na kuwapakia watoto wake: *Luhuvilo, Penensia, Daudi, na Faraja.* Waliibeba hadi kilabu cha pombe cha karibu ambako ndio walipopatikana wateja waliokuwa wanafurahia na kushikilia glasi zilizojaa pombe hizo. Bi Ndelwa alinyanyua uso, akawatazama wanawe kwa simanzi na kuwaambia: _“Wanangu chonde chonde msome kwa bidii mkaajiriwe., msije mkaishia kuwa kama mimi. Hii kazi ya kuuza pombe imeniletea fedheha nyingi, msije ishi haya maisha.”_ Familia mbili tofauti, kazi mbili tofauti, kulima na kutengeneza pombe za kienyeji. Lakini sauti zao zilifanana, ujumbe wao ulikuwa mmoja: elimu ndio njia pekee ya kutoroka fedheha ya maisha waliyoyapitia. Na kweli, kwa juhudi na jasho la hizo kazi walizoziona kama adhabu, waliwasomesha watoto wao. Amani alisomea Kilimo na Mifugo, Roja na Milembe walichukua masomo ya Masoko. Kwa upande wa Bi Ndelwa: Luhuvilo na Penensia walihitimu digrii ya sheria. Daudi akajikita kwenye Chemical Processing, Faraja akamaliza Business Administration na Masoko. Wazazi wakafurahi, watoto ni wasomi na wanajua kuongea kiingereza na hadi walitambiana na wazazi wengine kule kijijini. Vijana wakatunukiwa vyeti, wakavaa nadhifu, wakabeba CV zao na kuanza matembezi kupita maofisini kutoka Wizara moja hadi kampuni binafsi nyingine. Wengine walifanikiwa, Amani alipata ajira Kigoma kama Bwana Shamba, Daudi akaajiriwa Tanzania Breweries, akihusika na kutengeneza pombe kiwandani pale. Faraja akaingia Vodacom; kama afisa masoko akitangaza na kusambaza vifurushi. Huku Roja, Milembe, Penensia na Luhuvilo wakitembea na bahasha bila mafanikio hadi miguu ikaanza kuota sugu. Miaka ikazidi kukatika, huzuni na simanzi zikatawala kwa vijana wale na wakati mwingine walishindwa kuwaambia wazazi wao uhalisia kwa kuogopa kuwavunja moyo. Maana hebu fikiria matarajio ni kuwa ukisoma kuna kazi, ila leo hii msomi anamwambiaje mama yake wa kijijini kuwa kakosa hela ya kula? Wapi tulipokosea ? Kwa macho ya kawaida, tunaweza kusema: “Elimu ni njia ya kutoka kwenye umasikini.” Lakini hebu tujiulize… je, elimu yetu ilitufundisha namna ya KUONA thamani ya tulikotoka? Au ilitutenganisha kabisa na mzizi wa mafanikio yetu halisi? Wazazi hawa wawili, Bi Nuru na Bi Ndelwa walikuwa na _‘micro-enterprises’_ za maana tu. Kilimo na utengenezaji wa pombe vilisomesha watoto hadi chuo kikuu! Hii ni proof of concept kwamba walichokuwa nacho kilikuwa sustainable, shida haikuwa kwenye aina ya shughuli, bali tatizo lilikuwa ni *scale na structure.* Shida ilianzia pale walipoanza kuichukia kazi yao mbele ya watoto wao. Kilio cha _“msije mkaishia kuwa kama mimi”_ kilipandikiza mbegu ya aibu na kujikataa ndani ya watoto hawa. Badala ya kuona kazi za wazazi wao kama urithi, waliiona kama adhabu. Waliamini maisha mazuri yapo ofisini, si shambani au kwenye chupa za pombe ya kienyeji. Roja na Milembe walienda chuoni kusoma elimu ya masoko, wakitazamia mbeleni kuwa maofisa masoko na matangazo, wakikaa kwenye ofisi zenye kiyoyozi, huku wakinywa kahawa za bure. Hawakuwahi kufikiria kwamba walizaliwa nyumbani penye chakula tele kilichotoka shambani, na mama yao alikuwa na viazi na mahindi ya kutosha kula na kuuza. Kama elimu yao ya masoko ingeunganishwa na uzalishaji wa Bi Nuru, pengine leo wangekuwa na organic farm brand yenye label: “RoMi Organics – Mazao Bora kutoka Mkalaini.” Faraja alisoma masoko na biashara. Alitamani kuajiriwa Vodacom na ofcoz aliweza. Lakini je, aliwahi kujiuliza: kama mama yangu aliweza kutengeneza pombe ya kienyeji hadi akanisomesha, kwanini nisitafute kibali, nifanye branding ya hiyo pombe, nipate nembo ya TBS, niuze katika mahoteli ya kitalii kama authentic Tanzanian spirit na kila mtu akaonja ufundi wa Bi Ndelwa katika ubora wa kisasa. Daudi, kwa kejeli ya circle ya ulimwengu, now anafanya kazi TBL akitengeneza pombe kwa teknolojia ya kisasa; wakati alikua akibeba pombe ya mama yake kwenye ndoo, leo hii anatumia elimu yake kuendeleza kile alichokikataa. Ni kama historia imejirudia kutoka Ukalawa hadi Dar es Salaam, akiwa amerudi katika wimbo ule ule wa Bi Ndelwa, lakini kwa jina tofauti: Industrial Alcohol Processing. Elimu Bila Mizizi ni Kiatu Bila Mguu Ukweli wa kusikitisha ni kwamba mfumo wetu wa elimu haukuwahi kutufundisha kuheshimu tulipotoka bali ulitutenganisha. Ukatufundisha kwamba maisha ya mashambani ni fedheha, kazi za mikono ni adhabu, na ustaarabu unapatikana tu unapokalia kiti cha matairi na kuvaa tai. Kwa bahati mbaya, kizazi kilichoamini hivyo leo kimegundua ukweli mchungu: ajira hazipo, mishahara ni midogo, maisha yamekuwa magumu na zaidi, zile “kazi za aibu” zilizowalisha na kuwasomesha ndizo zinazowapa watu uhuru wa kifedha leo. Mfumo huu uliasisiwa makusudi kwa ajili ya kutengeneza subordinates ambao ni rahisi kufuata amri na sio kufanya ‘ground breaking changes’ katika maisha yao ya kila siku au walipotokea. Kilichofanyika ni kana kwamba, vijana wetu walipewa jembe kisha waanze kuzunguka kwenye mashamba ya jirani kutafuta vibarua vya kulima, ilhali nyumbani kuna shamba lililohitaji tu kufyekwa na kupanuliwa. Elimu yao ingetumika kuboresha mfumo, kuongeza tija, kuongeza soko si kukimbia kabisa na kutafuta ajira kwa wengine. Tunaishi katika wakati ambapo vijana wanazunguka mjini na maofisini wakiwa na vyeti makini kabisa na wasifu mrefu kama soksi za wanafunzi wa unesi, lakini hawana pa kuvitumia. Wazazi wao walilima, wakafanya biashara, wakauza mkaa, pombe za kienyeji na walikuwa na mtaji wa maisha ambao walidhani ni “aibu.” Leo hii tuna shahada za biashara lakini hatuwezi hata kuuza vitumbua mtaani. *Suluhisho* Maisha ni zaidi ya ajira za ofisini tu wala kuajiriwa na kuvaa tai kwenye kiyoyozi sio ukombozi. Elimu ya kweli ni ile inayoweza kutafsiri tulichosomea ili iweze kuboresha kile kilichotulea. Kwa mfano: *Sheria:* Penensia na Luhuvilo wangeweza kusaidia mama yao kupata kibali halali cha kuuza pombe na kulinda biashara ndogo ndogo. *Biashara:* Faraja angeweza kutengeneza kampuni ya local brews na kuingia sokoni . *Kiwanda:* Daudi angeweza kuungana na ndugu zake kutengeneza kiwanda cha kuzaliwa pombe kwa kutumia mbinu za kisasa kabisa wanazotumia TBL. *Kilimo:* Amani angeweza kuanzisha shule ya wakulima vijijini na kuandika mwongozo wa agriculture for wealth. *Masoko:* Roja na Milembe wangeweza kufanyia rebranding bidhaa za kijijini chao na kuzipeleka sokoni kupitia mitandao. Ukweli mchungu ni kwamba Elimu isiyo na connection na maisha yako ya kila siku ni sawa tu na bomu linalosubiri kulipuka. Lazima unachosoma kiweze kutafsirika katika vile ambavyo walifanya wazazi wako hadi ukafika ulipofika. Moja ya sababu kubwa Wabantu kuwa na familia ambazo ni legelege (kulinganisha na waarabu na wahindi) ni kutoweka nguvu katika kuboresha legacy ya familia hizo. Sababu kila kizazi ni kama kinaanza upya na kuona shughuli iliyofanikisha mafanikio yake kama ushamba. Kuna mashujaa wengi wa maisha wanaojulikana kwa jina la wazazi. Ingawa walikosa vyeti lakini walihakikisha watoto wao wanahitimu elimu za juu. Waliuza mihogo, pombe, mkaa na walijinyima ili sisi tupate elimu. Iweje leo tumwone mama aliyelima mahindi ili usome kama mtu aliyeshindwa? Iweje tumwone baba aliyekuwa fundi seremala ukapata hela ya kujikimu kama aibu?Au iweje udharau shughuli hizo? Kujiendeleza haina maana ya kujikana, mafanikio halisi ni pale unapoweza kurudi kwenye chanzo, ukakitumia kama msingi wa ujenzi mpya. Sio kutupa kila kitu na kuanza upya ugenini bila mizizi. Usiione kazi ya mzazi wako kama aibu. Inawezekana ndicho kitu pekee kilichofanya uwe hapo ulipo leo. Badala ya kutafuta ajira tu, tafuta namna ya kufanya yale waliyoanza kuwa rasmi, kuwa ya kisasa na kuwa endelevu. Kwa sababu mwisho wa siku, ajira siyo ofisi. Ajira ni uwezo wa kutumia maarifa kujiletea kipato halali iwe ni kwa jembe, kwa mdomo, au kwa kichwa. Na pale ambapo historia yako imekupa mbegu usiikatae, ioteshe, ikuze, na itumike kuwainua wengine. Kama kuna kisasi kizuri tunachoweza kulipa kwa wazazi wetu basi ni hiki: Kuwafanya wajivunie kazi walizozifanya… kwa kuona kwamba kile walichodhani ni fedheha, kimetusaidia kujenga maisha yenye heshima na faida. _Mimi ni mjumbe tu..nisiuwawe._ *Mjombaako* *©️BantuKwanza.*

Comments