
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
June 6, 2025 at 02:19 PM
*HAKUNA ‘FREELUNCH’ IKULU YA MAREKANI*
*Maisha ya Rais wa Taifa Tajiri Zaidi Duniani Hayana Mtelezo Unavyodhani*
Ilikuwa ni mwaka 2009, Michelle Obama akiwa bado mgeni kabisa ndani ya White House. Wiki chache tu baada ya kuhamia, alipokea kile alichodhani ni bahasha ya taarifa kutoka kwa wahudumu wa jumba hilo. Lakini alipofungua, akakutana na bill iliyoshiba, ndefu, tena iliyochambua hadi vipande vya peanut butter vilivyotumika kwenye mkate wa binti yake Sasha.
Bila maelezo mengi, alichopewa ilikuwa ni orodha ya gharama za chakula na matumizi mengine walizotumia kama familia, akiwa na wajibu wa kulipa kutoka kwenye mshahara wa mumewe, na bill hii ilikuwa ni ya kwanz kati ya nyingi ambazo angeendelea kupata kila mwezi..
Michelle alishtuka, hakujua kabisa kwamba hata ukiwa mke wa Rais wa Marekani, nchi tajiri zaidi duniani hakuna mtelezo. Kwa haraka unaweza kuimagine jinsi alivyoenda kuwaambia wanae kuishi kwa bajeti.
Rais wa Marekani analipwa kama *dola 400,000 (sawa na pesa za kitanzania billioni 1)* kwa mwaka kiasi ambacho kwa hapa nchini kwetu kinaonekana kuwa kikubwa sana. Lakini ukishajua namna ambavyo analazimika kutumia fedha hiyo, utaanza kuelewa kwamba kuwa rais siyo tiketi ya kuishi kama mfalme, hasa hasa nchi za wenzetu.
Kwa maadili ya kisiasa na uongozi ya Marekani, serikali inagharamia yale tu yanayohusiana na majukumu rasmi ya rais kwa taifa (official government business). Mengine yote hasa ya familia na matumizi binafsi yanaachwa kwa rais mwenyewe, si analipwa mshahara bwana.
Chakula mkuu jilipie, hii sio kazi ya kodi za wananchi, ingawa ndani ya White House, kuna wapishi wa kimataifa (ambao mshahara wao huwa inalipa serikali), meza za kifalme, na huduma ya hali ya juu ambayo ni classic kweli kweli, lakini ukila lasagna au fleur burger ujiandae kulipa bill.
Rais analipia kila kitu kinachohusu mlo wa familia yake. Kuanzia kifungua kinywa cha mtoto wake hadi dessert ya usiku, anawajibika. Bila kujali hadhi, serikali ya Marekani haitumii senti ya kodi ya raia kwa mambo binafsi ya mtu anayeshikilia ofisi ya juu zaidi.
Kwa watanzania wengi waliokulia kwenye dhana ya “mheshimiwa akifika, kila kitu ni bure,” hili ni jambo linalotia mshangao. Lakini huko, ndiyo msingi wa utawala madaraka si leseni ya kutumia pesa ya wananchi hovyo.
Unaweza kuwa interested kutaka kujua kuhusu ishu za ada za watoto maana ni jambo ambalo kawaida huwapa wazazi kijipresha cha hapa na pale. Labda nikuambie tu kama Rais wa Marekani akiamua mwanae asome shule ya kifahari kama *Sidwell Friends School* moja ya shule bora zaidi Marekani au labda IST ( yenye hadhi hizo hapa bongo), ambapo ada inavuka *dola 50,000* kwa mwaka, mzazi wake ambaye ni Rais hulipa kama mzazi mwingine yeyote. Hakuna habari ya serikali italipa..
Hakuna posho za elimu wala “voucher” kutoka Ikulu. Hii ni sehemu ya kudumisha kanuni kwamba cheo cha baba yako hakiwezi kuwa mzigo kwa umma. Na hii si hadithi ya rais mmoja tu; kuanzia *Clinton, Obama hadi Biden*, jambo hili limekuwa ni kanuni isikiukwa.
Vipi mambo yake binafsi inakuwaje analipiwa au? Nchini Marekani Rais na familia yake hujiendesha kama raia mwingine wa kawaida.
Matumizi kwenye vitu kama:
1. Nguo anazovaa au gharama za dry cleaning analipia mwenyewe.
2. Huduma za saluni, kukatwa nywele, au kufanyiwa makeup pia ni gharama zake.
3. Safari binafsi (kama vacation au matembezi ya kifamilia) familia yake hulipa sehemu inayolingana na gharama za usafiri kwenye ndege za commercial (first class equivalent), hata kama wamesafiri kwa Air Force One (ambayo kwa sababu za usalama ni lazima atumie).
Ingawa wengi hudhani kuishi White House ni kama kushinda bahati nasibu ya maisha, ukweli ni kwamba baadhi ya marais wameondoka Ikulu wakiwa wameelemewa na madeni si kwa sababu ya ufujaji, bali kwa sababu ya mfumo unaowatwika mzigo wa gharama binafsi huku wakiumizwa na mtazamo wa hadhi yao.
Kwa mfano, familia ya Ronald Reagan iliondoka White House mwaka 1989 ikiwa kwenye hali ngumu kifedha, baada ya kutumia mamilioni katika mapambo ya nyumba, hafla zisizo rasmi, na maisha ya heshima yaliyowalazimu kuchukua mikopo na kufanya mikataba ya hotuba mara tu walipotoka madarakani ili kujiokoa kifedha.
Kiasi kwamba, licha ya Reagan kuwa Rais wa taifa lenye nguvu zaidi duniani, alihitaji kufanya matangazo ya umma na kuuza haki za hotuba zake ili kufidia gharama za kuishi Ikulu.
Upande mwingine familia ya Bill Clinton, baada ya drama nzito ya Monica Lewinsky, waliondoka madarakani wakiwa na deni la zaidi ya dola milioni 16! Yap, kesi za kisheria, fidia kwa akina Paula Jones, na mawakili waliomsaidia kupambana na impeachment vilimkosesha usingizi. Maana yake ni kwamba matatizo yako binafsi utasolve wewe na familia yako. Kwa kifupi, jamaa alitoka White House akiwa na suti nadhifu lakini wallet imechakaa..
Hata wakati wa kampeni za mwaka 2020 Trump alipotumia ndege ile ya serikali kwa sababu alikuwa bado Rais alilipia karibu *dola milioni 4.7* kama gharama za safari hizo. Uzuri huyu jamaa ni milionea hivyo haikuwa tabu sana!
Kuonyesha kuwa wenzetu wanaheshimu hela ya mlipa kodi ikitokea mmoja wa wanafamilia amepiga simu binafsi kwa kutumia line ya serikali, bili hutolewa, na kulipwa. Unashangaa eeh, ndio maanake simu zako binafsi tumia smartphone.
*Kwa Nini Wenzetu Wanazingatia Haya?*
Kwa Wamarekani, hoja kuu ni uwajibikaji wa matumizi ya fedha ya umma. Wanatambua kwamba kodi zinazokusanywa kutoka kwa madereva wa malori, wauguzi, walimu, wakulima na watu wengine wa hali za kawaida kabisa si kwa ajili ya maisha binafsi ya kiongozi even if ni Rais.
Hii ndiyo sababu Marekani imejenga mfumo wa kiutawala unaotenganisha mamlaka na starehe. Ni dhana muhimu kwamba madaraka ya juu yanapaswa kuwa mfano wa nidhamu, si kivuli cha anasa.
Hii ni tofauti kabisa na kwetu Afrika ambapo kiongozi ni kama mwana wa mfalme kama sio mfalme kabisa.. Katika mataifa mengi ya Afrika, picha ni tofauti sana. Mara nyingi, tunashuhudia viongozi wakitumia magari ya kifahari kwa shughuli binafsi, wakisafiri na misafara ya magari zaidi ya 15 kwa hafla isiyo ya kitaifa, au hata familia zao kusomea nje ya nchi kwa kodi za wananchi bila aibu. Kiongozi anapofiwa, serikali inalipa. Mtoto wake anapofunga ndoa, kampuni za umma zinatoa michango ya kifahari. Kuna wengine hata mtoto wa kiongozi anapojifungua, msafara unapelekwa kutoa hongera.
Huko Marekani na nchi nyingi za Ulaya hakuna hizo habari. Kifo cha ndugu wa rais? Serikali inaweza kutoa rambirambi ya kidiplomasia, lakini gharama ni zake binafsi.
Ndoa ya mtoto wa Rais huwa ni jambo la kifamilia na halihusishi kodi ya mlipa ushuru.
Moja ya kitu cha kujifunza hapa ni kwamba uongozi ni heshima ya kutumikia, si fursa ya kula. Kwa viongozi wetu barani Afrika, watendaji wa serikali, kwa mashirika ya umma hili si somo la kuangalia kwa kejeli, bali la kuiga. Mataifa yanayoendelea hayawezi kujinasua kiuchumi kama viongozi wake wataendelea kuishi kama wafalme, huku raia wakihangaika na bei za unga na mafuta ya kula.
So kila unapomuona POTUS akiwa White House, usidanganyike na uzuri wa mjumba ule. Ndiyo jumba ni zuri na lina historia ya aina yake na lina ulinzi wa hali ya juu lakini ukivuka mlangoni, na kuingia maisha ya ndani, utagundua kwamba hata rais wa taifa lenye nguvu zaidi duniani lazima awe na bajeti..
Hakuna mlo wa bure, wala suti za bure au sijui vacation ya bure. Kwa wenzetu Ikulu siyo kasri la kifalme bali ni ofisi ya taifa.
Na pengine, kwa kujifunza kutoka kwao, sisi pia tunaweza kujenga nchi ambayo viongozi wake hawakai juu ya kodi, bali upande wa wananchi.
Kwa mfumo huu wa Marekani, hata ukiwa Rais, ukisahau wallet unaweza kukosa lunch Ikulu… tofauti na huku ambapo ukivaa tai tu, unaweza kula mpaka posho ya chai ya watumishi wengine. 😌
*Mjombaako*
*©️BantuKwanza*

❤️
1