KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
June 10, 2025 at 05:34 PM
*HATIMA YA KIMUNGU* *Hadithi ya Unabii na Kifo Cha Mfalme Ahabu* _”Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.“_ Moja ya sehemu muhimu sana katika ‘Sala Ya Bwana’.. Hatima ya mwanadamu inategemea sana mapenzi ya Mungu ‘God’s Will’, na ingawa mara nyingi sisi wanadamu huangalia ulimwengu na yaliyomo katika macho yetu ya kianadamu, nachelea kusema kuwa kuna mengi nyuma ya hatima zetu.. Leo kuna stori moja huwa naipenda sana inamhusu moja wa wafalme wakorofi na watukutu kuwahi kutokea katika falme ya Israel.. Hapo zamani za kale, katika ufalme wa Israeli, kulikuwa na mfalme aitwaye *Ahabu mtoto wa Omri*. Ahabu alikuwa ni mfalme mtukutu ambaye alipenda kufanya mambo mengi kwa njia zake mwenyewe. Aliitawala nchi kwa mkono wa chuma na huku akiwapa heka heka za hapa na pale manabii wa Mungu akiwemo Eliya. Siku moja, *Ahabu akiwa na mkwe wake Jehoshaphat aliyekuwa mfalme wa Juda* katika porojo zao kifalme akamwambia mkwewe “ Poti nataka nikampige *Ben Hadadi niichukue Ramoth-Gileadi unasemaje?.* “Mimi sina tatizo mkwe, si unajua tena watu wangu watu wako na farasi wangu farasi wako. Imeisha hiyo poti.” akajibu Jehoshafati Lakini sababu mfalme huyu wa Juda alikuwa ni mtu mwenye tahadhari sana, akaona itakuwa wazo zuri kuuliza manabii kwanza, wawape ubashiri kabla ya kwenda vitani. Kwa ufahamu tu, tabia ya kuomba ubashiri wa kiroho/kupiga ramli kutoka kwa manabii, mizimu, wasoma nyota, au wabashiri kabla ya kwenda vitani imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na kuna mifano mingi kuhusu tamaduni hiyo kuanzia enzi za kale hadi miaka ya karibuni. Hivyo Jehoshafati akamwambia Ahabu _“lakini nilikuwa nawaza hapa tungepata unabii kuhusu jambo letu kabla tujaenda ingekuwa vyema zaidi”_ Ahabu akaafiki. Ndipo Ahabu aliwaita manabii wake karibu 400 ambao walipenda kumsifu kuliko kusema ukweli, sijajua aina hiyo ya watu enzi hizo waliitwaje ila kizazi chetu wanaitwa machawa. Akawauliza _“je niende kushambulia Ramoth-Gileadi au lah?”_ Manabii wale waliopenda kumjaza mfalme ujinga aliotaka kusikia bila kuwaza mara mbili, walipiga kelele kwa pamoja, _“Nenda vitani, Ee Mfalme! Ushindi utakuwa wako!”_ Yehoshafati, mfalme wa Yuda kutokana ule umakini wake hakuwa ameridhishwa kabisa. _“Poti, hakuna nabii wa Bwana ambaye tunaweza kumwuliza, hawa jamaa sijawaamini sana?”_ aliuliza, akiwa na shaka kidogo. Ahabu aliminya macho kidogo na kutoa pumzi ndefu kisha akajibu _“Yupo Mikaia mwana wa Imla, lakini namchukia huyu jamaa. Yaani siku zote hanitolei unabii mwema, ila ubaya ubwela tu.”_ Licha ya kusitasita kwake, Ahabu aliamua kumwita Mikaia. Yule Mjumbe aliyemchukua Mikaia wakiwa njiani alijaribu kumwelekeza aseme nini, lakini Mikaia, akiwa nabii makini, aliahidi kusema tu kile Bwana atakachomwambia. Mikaia alipowasili, mfalme akampokea kwa kijembe _“ umekuja eeh mwana wa Imla usiyependa mazuri juu yangu”_ Mikaya akajibu kwa utani _“ hapana mkuu mi nipo kwa ajili yako, nini shida?”_ Ndipo mfalme akauliza _“Mikaya nilikuwa na mpango wa kwenda kuvamia Ramoth-Gilead kurudisha ardhi ambayo Ben Hadadi mkubwa alichukua huko nyuma, vipi tuende vitani au tutulie?”_ Awali nabii huyu kutokana na upepo aliokuwa kauona hapo alimpa Ahabu ujumbe wa matumaini kama manabii wengine, lakini alisema kwa kuipamba na kuzidisha mno kitu ambacho hata Ahabu akahisi ni kejeli. Alimwambia _“enenda ukashinde,”_ Mikaia alisema kwa tabasamu pana, _“kwa maana Bwana ataitia mikononi Ramoth-Gileadi mikononi mwako mfalme.”_ Ahabu akakunja uso akimfokea kwa ghadhabu _“Hivi we Mikaya ni mara ngapi nimekufanya uape ili uniambie ukweli kwa jina la Bwana?”_ Tabasamu la Mikaia likafifia, basi akaamua kutoa unabii wa kweli. Akasema _“niliona Israeli wote wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Bwana akasema, ‘Watu hawa hawana Kiongozi. Kila mmoja na aende nyumbani kwa amani.’”_ Ahabu akamgeukia Yehoshafati huku akisikitika na ghadhabu _“sikukuambia! huyu jamaa hajawahi kunitolea unabii mwema hata siku moja?”_ Hayo ndio yaliyokuwa yakiendelea pale Israel katika hekalu la mfalme. Lakini shughuli nzima ilifanyika katika viunga vya mbinguni. Muda huo Mungu alikuwa akifanya baraza mahsusi na jeshi lake la mbinguni. Lusifa, akiwa katika ‘mood’ yake ya utani, aliingia katika mkutano huo kwa mikogo huku akijiimbisha nyimbo zake za hapa na pale. Mwenye Enzi akajiegemeza kwenye kiti chake cha enzi na kuhutubia mkutano akasema _“Ahabu ameshakuwa pasua kichwa mno. Nilimsamehe wakati ule wa Naboth kuhusu kuangamiza nyumba yake yote ila naona ni muda muafaka apumzishwe”._ _“Mpango wangu ni akafie katika uwanja wa vita, nani ataweza kumrubuni Ahabu ili akapigane Ramoth-Gileadi na afie huko?”_ alimalizia Mungu Mwenye enzi kwa sauti ya kutetemesha iriyorindima ukumbi mzima. Malaika wa majeshi mbalimbali wakatoa maoni yao ya hapa na pale, lakini hakuna aliyekuja na plan nzuri iliyonyooka. Ndipo Lusifa, mjanja wa mjini akaona asipitwe na nafasi hii adhimu kabisa, akasogea kwa mbele akiwa na tabasamu lake la hila. _“Mwenye enzi mimi nina mbinu moja uhakika mno, jamaa hawezi toboa”_ alisema kwa kujiamini sana …_”ni rahisi sana nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote, sababu ninamjua Ahabu ana aleji kali na ukweli”_ alijibu, huku akifurahia ishu nzima ilivyokuwa inaenda . _“Si unakumbuka hata wakati wa Eliya, huyu jamaa huwa anapenda kuambiwa vitu anavyopenda kusikia tu, hivyo hapo hapo ndio mimi nitakapomwangusha”_ Mungu akainuka na kusema. _“Vizuri sana, natumai utafanikiwa kumdanganya. Nenda ukafanye hivyo.”_ _“Imeisha hiyo, Mwenye Enzi”_ alisema huku akinesa na kutembea kwa madaha, Lusifa alitoweka kwenda kufanya kazi yake, na kuliacha baraza la mbinguni likiongea kwa kicheko kuhusu jinsi Ahabu anavyoenda kudanganywa na tamaa yake ya kusikia habari nzuri pekee. Lakini sababu haki ya kiungu huwa imenyooka na inatenda haki pasipo kupinda.. Kutokana na hili basi Mungu akasema sababu mimi ni mwenye haki na siku zote haki yangu ni nyoofu lazima nimpe Ahabu nafasi. Basi ili hilo kutimia, roho wa Mungu akashuka kwa Mikaya na kuhakikisha kuwa ingawa kulikuwa na manabii 400 ambao waliingiwa na roho wa uongo, bado kulikuwa na nafasi ya kuokolewa iwapo Ahabu ataamua kusikia sauti ya Mungu ndani ya nabii mmoja. Haya turudi duniani.. Sasa baada ya Mikaya kuwaambia kwa kina unabii huo, baadhi ya manabii wakawa wakali na hadi kuanza kumshambulia. Basi akiwa amechukizwa na unabii huo wa Mikaya, Ahabu akawaambia walinzi wake _“hebu mfungeni huyu jamaa na unabii wake wa ajabu ajabu hadi nitakaporudi. Hakikisheni mnamnyoosha, chakula na maji apewe kidogo akili imkae sawa.”_ Mikaya akisikiliza maelekezo hayo akadakia _“ukirudi mzima labda sio Bwana aliyeongea na mimi. Nimekaa palee, hutoboi wewe”_ Akiongozwa na ukaidi wake Ahabu, akaamua kuusikiliza unabii wa roho ya uongo, akapanga kwenda vitani. Huku akijaribu kuipiga chenga hatima kwa kujificha, na kubadilisha mavazi yake asionekane mfalme na kumwambia Jehoshaphat pekee avae kifalme bado haikutosha. Katikati ya mapambano makali mshale uliopigwa bahati mbaya ukampata, kuthibitisha kuwa huwezi kuikwepa hatima, hasa ikiwa imeamriwa na Mungu. Mshale huo ukampa jeraha kubwa Ahabu hivyo akamwamrisha dereva wa chariot yake kugeuza na kutoka kwenye uwanja wa mapambano ili akajiuguze lakini jioni ile ile kutokana na jeraha lile hali yake ikawa mbaya hatimaye umauti ukamkuta. Nilikuwa najaribu kuwaza muda ule Ahabu alipolala kuelekea kufa katika chariot yake, huenda alijiuliza jinsi mambo yote yalivyokwenda kombo na jinsi ukaidi wake ulivyomponza wakati Mikaia labda alicheka peke yake huko alipofungwa, akijua kuwa alikuwa amesema ukweli usio na doa. Huku nae Mungu akiwa anasema shughuli imeisha na Lusifa akitikisa mguu na kujipiga kifua kuhusu umahiri wake. Hivyo, hadithi ya Ahabu inamalizika kwa mtindo huo huku tukiona kuwa unabii wa Mungu huwa haukimbiwi. MAFUNZO Hadithi nyingi huwa na mafunzo, mengine ni ya wakati inatokea na nyingine ni kwa ajili ya kizazi cha mbele.. Tuseme tu waisraeli walikuwa vichwa ngumu hivyo mafunzo ya wakati wao sidhani kama walizingatia sana, lakini sisi wa kizazi hichi tuna la kujifunza.. 1. Hatima ya Kiungu haikimbiwi, ni wazi kuwa lile neno la mapenzi ya Mungu yatimizwe ni zito na lenye maana kubwa sana.Maisha ya mwanadamu yanahitaji sana hii God’s will. Hatima ya mwanadamu iko ndani ya mikono ya Mungu lakini amempa mwanadamu uwezo wa kusikiliza sauti ya ndani yenye kweli.. Ingawa mara nyingi inaonesha wengi huwa hawasikilizi sauti hii na kuipuuza. 2. Haki ya Kiungu ni ya ajabu ni iko fair mno, unaweza ona kuwa pamoja na kwamba roho wa uongo aliingia kati ya manabii 400 , bado mwenyezi Mungu aliruhusu mtu mmoja kuwa na ukweli ili kama Ahabu angefungua sikio lake la kiroho basi angesikia. Hii inaweza pigilia msumari kuwa huwezi pewa jaribu pasipo mlango wa kutokea. 3. Kumbe uchawa upo muda mrefu, na kuna viongozi wana asili ya kupenda kuambiwa vitu wanavyotaka kusikia tu hata kama vina madhara. Hii imesababisha watu wote wasio na ujasiri wa kusema ukweli kukaa kimya na kuitikia kile ambacho kiongozi anataka. Na kibaya zaidi ni kwamba wale wachache wenye ujasiri wa kuwaambia viongozi ukweli jinsi ulivyo wamekutana na madhila makubwa kuanzia kutengwa,kuteswa hadi kuuwawa. Hivyo ni vyema viongozi wetu kujenga tamaduni ya kuwapa nafasi akina Mikaya ili wawaambie ukweli hata kama unauma vipi maana inawezekana ukweli ndio ukombozi wao na inaweza kuwaepusha maanguko makubwa.. Nini kingine umejifunza!? Cogito, ergo sum *Mjombaako* *©️BantuKwanza*
Image from KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets: *HATIMA YA KIMUNGU*  *Hadithi ya Unabii na Kifo Cha Mfalme Ahabu*  _”M...

Comments