
KitaaCtics: Where the Elite Meets The Streets
June 11, 2025 at 04:23 AM
*SI MBAYA KUJUA*
*Nanasi Pambo La Kitajiri*
Wakati leo hii ukifika msimu wake tunanunua hadi kwa shillingi mia tano, na kama ukienda Stereo pale Temeke unaweza shangazwa na urahisi wa bei za tunda hili, mambo hayakuwa hivi miaka kama 300 tu iliyopita barani ulaya.
Katika *miaka ya 1700*, mananasi yanayojulikana kwa jina lake la kitaalamu *Ananas comosus* hayakuwa tu matunda yaliyopatikana kirahisi kama sasa, yalikuwa ni kilele cha anasa na upekee barani Ulaya.
Uadimu wake na asili yake ya kigeni yaliyafanya kuwa na thamani kubwa sana miongoni mwa matajiri. Tofauti na leo, ambapo mananasi yanapatikana kwa urahisi kwenye supermarkets na masoko mengine, safari ya nanasi moja kutoka shambani hadi Ulaya ilikuwa ni ndefu na yenye gharama kubwa.
Mananasi kwa asili yalitoka Amerika Kusini na Carribean na yalilimwa kwa mara ya kwanza na jamii wazawa kama Tupi-Guarani waliokuwa wakikaa kusini mwa Brazili na Paraguay wenyeji hawa waliliita tunda hilo kwa jina la *“nana,” likimaanisha “tunda bora.”*
Mananasi yalikutana na wapelelezi (explorers ultimately have wasoma kwenye historia) wa kutoka Ulaya mwishoni mwa karne ya 15. Ni nyakati hizi hitaji kubwa ya mananasi ilianza baada ya exploration ya wazungu barani Amerika. Tunda hili kwa mara ya kwanza liliripotiwa katika visiwa vya Carribean na kisha baadae Amerika Kusini, na ukisoma barua pamoja na shajara zao zilizoelezea tunda hilo zilijaa sifa za kupindukia kama za kijana aliyepagawa na mapenzi.
Chukua, kwa mfano, maelezo yaliyoandikwa na Gonzalo Fernández de Oviedo y Valdés mwaka 1535. Aliandika kwamba nanasi lilikuwa halijawahi kushuhudiwa kwa “uzuri wa mwonekano, harufu mwanana, ladha isiyosemeka,” na kwamba, “kati ya hisia tano za mwili, zile tatu zinazoweza kutumika kwa matunda na hata ya nne, ile ya kugusa, linazidi matunda yote
Upo!?
Jitihada za mwanzo za kubeba mbegu na kupanda ziligonga mwamba na hivyo njia pekee ya kulipata tunda hilo ilikuwa ni kulisafirisha. Hata hivyo kusafirisha tunda hilo kuvuka bahari ya Atlantiki bila kuharibika ilikuwa mchakato mahsusi na wenye wa gharama kubwa.
Ili kuhifadhi ubichi wake, mananasi yalikuwa yakisafirishwa katika ‘conditions’ zilizotengenezwa kwa uangalifu mkubwa, na mara nyingi maandalizi hayo yalisababisha tunda hilo kugharimu kiasi kikubwa cha pesa—wakati mwingine sawa na maelfu ya dola za leo. Inasemwa nanasi enzi hizo lilifika hadi dola 8000 (takribani Tsh 20m) kwa pesa ya leo.
Kwa sababu hizo, mananasi yakawa zaidi ya chakula; yalikuwa alama ya hadhi. Familia tajiri zilionyesha mananasi kwenye karamu za kifahari au hata kukodisha mananasi kuonyesha kwenye sherehe. Ndiyo, umesoma sawa—kukodisha nanasi ilikuwa ilikuwa ni big deal nyakati hizo! Wamiliki walihakikisha tunda hilo halijaguswa ili liweze kurudishwa na kutumika tena kwa maonyesho ya baadaye.
Mananasi pia yaliathiri usanifu na sanaa. Muonekano wake wa kipekee uliashiria ukarimu na utajiri, na kuathiri miundo kama vile “Pineapple Finial” maarufu juu ya Kanisa Kuu la St. Paul huko London na sanamu mbalimbali za mananasi.
Upekee wa nanasi ulipungua katika karne ya 19 kutokana na maendeleo ya mifumo ya usafirishaji,ugunduzi wa friji na mbinu za kilimo, na kufanya tunda hilo liweze kupatikana kwa urahisi zaidi.
Leo hii matumizi ya nanasi kama alama ya anasa na ufahari inabaki kuwa kipande cha kuvutia cha historia!Na kama hukujua basi leo nimekusanua.
So wakati unapanga kwenye New Year hii kupata Pinacolada, hebu waza kwanza miaka 300 iliyopita ingakuwaje.
*Mjombaako*
*©️BantuKwanza*
