
TRA TANZANIA
June 5, 2025 at 03:00 AM
VILABU VYA MPIRA LIGI KUU TANZANIA VYATAKIWA KULIPA KODI KWA HIARI
Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ligi kuu Tanzania Bw. Almas Kasongo amevitaka vilabu vya Mpira wa Miguu vinavyoshiriki ligi kuu Tanzania kuwa tayari kutii sheria za kodi kwa kulipa kodi zote wanazopaswa kulipa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuimarisha miundo mbinu ya michezo
Bw. Kasongo ametoa rai hiyo tarehe 04.06.2025 katika semina ya kodi iliyoandaliwa na TRA kwa kushirikiana na Bodi ya ligi Kuu Tanzania kwa maafisa watendaji Wakuu wa Vilabu vya Mpira wa Miguu vinavyoshiriki ligi Tanzania Bara na kufunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya ligi Kuu Tanzania Bw. Steven Mnguto
Ameongezea kuwa vilabu vya mpira vinapaswa kulipa kodi ili kuweza kutatua changamoto zinazozikumba tasnia ya mpira wa miguu nchini na kuimarisha miundo mbinu ya kisasa inayokwenda na wakati ikiwemo ujengwaji wa viwanja vya mpira.
"Unaweza ukaona kwamba leo hii kuna changamoto za miundo mbinu ya viwanja pia namna gani mpira wetu unapaswa kuwa lakini ili tuweze kuyafanya haya lazima tulipe kodi."
Nae Afisa mtendaji Mkuu wa klabu ya Kagera Sugar, Bw. Thabit Kandoro amesema kutoka na semina hiyo amejifunza umuhimu wa kushirikiana na TRA katika kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiyari huku akiishauri TRA kuona namna ya kuwakutanisha na maafisa wake ili na wao waweze kuwaelezea namna klabu zao zinavyofanya kazi.
👍
😂
❤️
😢
26