
TRA TANZANIA
June 11, 2025 at 04:34 PM
BAKHRESA AIPONGEZA TRA KWA KUTOA ELIMU NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KODI
Mlipakodi binafsi mwenye hadhi ya juu, Bw. Saidi Salim Bakhresa, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa juhudi zake endelevu za kutoa elimu ya kodi na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini.
Akizungumza leo, Juni 11, 2025, Jijini Dar es Salaam alipotembelewa na timu ya TRA ikiongozwa na Naibu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa, Bw. Gabriel Kimweri, ofisini kwake, Bw. Bakhresa amesisitiza umuhimu wa TRA katika kuwafikia wadau wote wanaostahili kulipa kodi ili kuchangia maendeleo ya taifa.
“Ni hatua nzuri sana TRA kuendelea kutoa elimu na kusaidia wafanyabiashara kushinda changamoto za kodi, Ninawashauri wote wanaostahili kulipa kodi wafuate wajibu wao kikamilifu ili tuweze kujenga taifa bora zaidi. Kila mtu anapaswa kutimiza wajibu wake na pia kupata haki yake kwa usawa.” amesema Bakhresa.
Kwa upande wa TRA, Naibu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa, Bw. Gabriel Kimweri, amesisitiza kuwa TRA itaendelea kuimarisha juhudi za kutoa elimu ya kodi na kutatua changamoto za wadau, hasa katika mwezi wa Juni 2025, ambao ni mwezi wa kampeni maalum ya TRA ya kutoa elimu na kutatua changamoto za kodi.
“Kampeni hii ni sehemu ya juhudi zetu za kuhakikisha wadau wanaelewa vizuri masuala ya kodi na kupata suluhu za haraka kwa changamoto za kikodi zinazowakabili, Tunajitahidi kuwafikia wengi kadri iwezekanavyo,” amesema Bw. Kimweri.
Ameongeza kuwa mtu yeyote mwenye changamoto ya kikodi asisite kuwasiliana na TRA kwa namba za simu 0800 780 078 au 0800 750 075, barua pepe [email protected], au tovuti ya www.tra.go.tz.
Kampeni hii ilizinduliwa rasmi na Kamishna Mkuu wa (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda tarehe 06.06.2025, ikiwa ni mwezi wa mwisho kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Lengo la kampeni hiyo ni kuimarisha uelewa wa wadau kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi na kutoa msaada wa moja kwa moja kwa wafanyabiashara wanaokumbana na changamoto mbalimbali za kikodi.
Mwisho

❤️
👍
🙏
😂
13