
Dr. BUDODI
May 17, 2025 at 01:07 PM
KUTOKWA DAMU NYINGI BAADA YA KUTOA MIMBA AU KUJIFUNGUA NI DALILI YA HATARI
Ilikuwa jioni, mwanga wa machweo ukipenya kupitia madirisha ya hospitali. Nilikuwa nikitembea kuelekea chumba cha kubadilishia nguo(Changing room) baada ya siku ndefu ya kuona wagonjwa. Hatimaye, zamu yangu ilikuwa inaisha, na nilikuwa tayari kurejea nyumbani.
Ghafla nilishtushwa na kelele zilizovuruga utulivu wa hospitali nzima.
"PPH!!"
Alikuwa nesi kutoka idara ya dharura(Emergency Department), Kelele hizi hazikua ngeni maskioni mwangu kama ilivo kwa muhudumu yeyote wa afya, kelele hii huashiria swala la uhai na kifo. PPH(Post Partum Haemorhage) ni hali ambapo mwanamke anapoteza damu nyingi baada ya kujifungua au kutoa mimba ambapo huwa ni zaidi ya lita moja ya damu baada ya upasuaji au nusu lita ya damu baada ya kujifungua kawaida. Ni hali inayoweza kusababisha kifo ikiwa haitadhibitiwa haraka.
Niligeuka haraka na kukimbilia chumba cha dharura. Wauguzi walikuwa wakisukuma kitanda cha dharura, na juu yake, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amelala, uso wake umejaa jasho na mikono yake ilikua yabaridi mithiri ya mfu, macho yake yalikua yamejaa hofu na alikua akipumua juujuu.
“Nimetokwa na damu nyingi, daktari,” alisema kwa sauti hafifu aliyotumia nguvu nyingi kuitoa huku akiwa amekamata kwanguvu koti langu jeupe. Nilimjibu kwa sura ya tabasamu “Usihofu utakua salama Sarah”
Nilimchunguza kwa na kutambua kuwa nguo zake zilikuwa zimelowa damu, na mapigo yake ya moyo yalikuwa yanakwenda mbio, ubaridi wa mikono kutokwa jasho na kupumua juu-juu kulitosha kudhibitisha kuwa hii ni PPH na mwanamke huyu alikua na dalili za kuelekea kwenye Shock(mshtuko wa mwili/ kufeli kwa mzunguko wa damu).
CHANZO CHA TATIZO
Nilipochunguza historia yake ya matibabu, niligundua kuwa alikuwa ametumia dawa za mitaani kutoa mimba wiki moja iliyopita. Hakuwa na uhakika kama mimba ilikuwa imetoka yote. Hali hii ilisababisha retained tissue, ambapo mabaki ya mimba hubaki ndani ya kizazi na kusababisha damu kuendelea kutoka.
PPH inaweza pia kusababishwa na:
kutoboka au kuchanika kwa kizazi (tear)
kulegea kwa kizazi (uterine atony)
matatizo ya kuganda kwa damu (coagulopathy)
Katika hali nyingine, daktari anaweza kupendekeza utoaji wa mimba kwa sababu za kiafya, kama vile mimba zabibu (molar pregnancy) au kutapika kupita kiasi (hyperemesis gravidarum). Lakini utoaji wa mimba kiholela huongeza hatari ya madhara makubwa.
HATUA ZA MATIBABU
Kwa haraka mgonjwa alitundikiwa drip ya maji ili kuongeza mzunguko wa damu, tukampa dawa za kusaidia kizazi kujikaza, na tukampeleka chumba cha upasuaji ili kuondoa mabaki ya mimba. Wakati wa upasuaji mdogo, niliona jinsi kizazi chake kilivyokuwa kimelegea—hali inayojulikana kama uterine atony. Tulifanya kila jitihada kuzuia damu kuendelea kutoka.
Baada ya saa mbili za matibabu makini, hali yake ilianza kuimarika. Alifungua macho na kunitazama kwa shukrani. “Nitaweza kuzaa tena?” aliuliza kwa sauti dhaifu.
“Ndio,” nilimjibu kwa tabasamu. “Lakini ni muhimu kupata huduma za afya mapema unapokumbana na changamoto yoyote ya uzazi.”
MADHARA YA PPH IKIWA HAITADHIBITIWA MAPEMA
Kama tusingechukua hatua za haraka, madhara yafuatayo yangetokea:
mshtuko wa mwili (haemorrhagic shock)—Mwanamke hupoteza fahamu, mapigo ya moyo hushuka au kupotea kabisa, na katika hali mbaya zaidi, huweza kusababisha kifo.
kufeli kwa viungo muhimu—Figo, moyo, na ubongo vinaweza kushindwa kufanya kazi ipasavyo, hali inayoweza kusababisha kifo.
UMUHIMU WA KUTAFUTA HUDUMA ZA AFYA
Baada ya siku kadhaa, nilimtembelea wodini. Alikuwa na nguvu zaidi, na alikuwa tayari kurejea nyumbani. Aliniambia kuwa angewaelimisha wanawake wengine kuhusu hatari za utoaji mimba kiholela.
Ni hatari kutoa mimba kiholela. Ikiwa umepitia hali hii, tafuta msaada wa afya haraka ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea.
📞 PIGA SIMU BURE: +255744667759
_ _ _ _