Dr. BUDODI
Dr. BUDODI
June 8, 2025 at 01:00 PM
*PID HUSABABISHWA NA NINI?* PID ni maambukizi yabakteria kwenye kizazi cha mwanamke ambapo viungo kama mji wa mimba, mirija ya uzazi, na mayai huathiriwa. Maambukizi haya mara nyingi husababishwa na vimelea wa magonjwa ya zinaa kama klamidia au kisonono(Gonorrhea). Maambukizi haya huanza kwenye mirija ya uzazi au mlango wa kizazi na kuenea hadi kwenye mayai na mji wa mimba ikiwa hayajatibiwa. Bakteria husababisha uvimbe na michubuko, ambayo huacha makovu yanayoziba au kuharibu mirija ya uzazi, ikifanya iwe vigumu kwa yai na mbegu za kiume kukutana. PID inaweza pia kusababisha hydrosalpinx, hali ambapo mirija inajaa maji. Tabia hatarishi ni pamoja na ngono isiyo salama, kuwa na wenza wengi, kuingiza vidole ukeni(douching) au historia ya magonjwa ya zinaa. Dalili zinaweza kujumuisha maumivu ya tumbo chini ya kitovu, homa, uchafu usio wa kawaida kutoka ukeni, au maumivu wakati wa tendo, lakini si kila mgonjwa wa PID hupata dalili hizi kwa wengine dalili hazionekani hadi wanaposhindwa kupata ujauzito. PID mara nyingi hugunduliwa kwa wanawake wa miaka 20 hadi 30. *JINSI PID INAVYOSABABISHA UTASA.* Mirija ya uzazi iliyoziba na makovu kutokana na PID inazuia mbegu za kiume kukutana na yai, ikifanya urutubishaji kutowezekana. Hata kama moja ya mirija iko wazi, makovu yanaweza kuzuia kijusi(yai lililorutubishwa) kusafiri hadi kwenye mji wa mimba, na kuongeza hatari ya mimba kutunga nje ya kizazi(Ectopic pregnancy), hali hatari inayohitaji matibabu ya haraka. Michubuko na uvimbe unaosababishwa na PID unaweza kuharibu ubora wa mayai au mji wa mimba, ikipunguza uwezekano wa mwanamke kuzaa kawaida. *NJIA SALAMA NA BORA ZA KUMSAIDIA MWANAMKE MWENYE MIRIJA ILIYOZOBA KUTOKANA NA PID* . Hakuna njia ya uhakika ya kuzibua mirija ikiwa imeziba, badala yake mgonjwa anashauriwa kuingia kwenye njia za upandikizaji ikiwa anahitaji mtoto * _In Vitro Fertilization (IVF),_ inachukua mayai moja kwa moja kutoka kwenye ovari, kuyarutubisha kwenye maabara, na kupandikiza mtoto aliepatikana kwenye uterasi, hii inaepuka changamoto ya mirija kuziba. *USHAURI WA KITAALAMU.* Ikiwa una historia ya magonjwa ya zinaa, maumivu ya chini ya tumbo, au mimba ya nje ya kizazi (ectopicl, wasiliana mapema na Daktari ambapo atapendekeza kipimo cha hysterosalpingogram (HSG) ili kuangalia mirija yako ya uzazi. IVF ni chaguo bora kwa mirija iliyoziba kabisa, hasa ikiwa kuna hydrosalpinx(mirija kujaa maji), ambayo inaweza kuhitaji kuondolewa kabla ya IVF. Usichelewe, kwani umri zaidi ya 35 hupunguza ufanisi wa njia hii. Jikinge na magonjwa ya zinaa kwa kufanya ngono salama, kutumia kondomu, na kutibu maambukizi haraka. Ni muhimu pia kufanya vipimo vya mbegu za mume wako ili kuhakikisha ubora wake. Daktari atakupa Ushauri wa kisaikolojia utakaokusaidia kukabiliana na msongo wa mawazo wakati wa matibabu. Kula chakula chenye virutubisho kama vitamini C ili kuimarisha kinga yako ya mwili. Kwa kuzingatia taratibu zote za matibabu bila shaka utaitwa mama.

Comments