MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
May 20, 2025 at 08:14 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA NANE *Yale maovu yote yafanyikayo gizani, huumbuliwa adharani kwenye mwangaza mweupe.* *Ulimwengu umeumbwa katika namna ya ukweli kushinda daima.* *Haijalishi ni kwa wakati gani, kama utachelewa au la.* *Uongo haujawahi kusimama mbele ya ukweli.* *Na hii ni sehemu ya nane* "Naam, kama nilivyokueleza. Tumepokea ofa nyingi za mashirika, kampuni na watu binafsi wanaokuhitaji kwa ajili ya matangazo yao." Bwana Didas akatamka huku akimakinika na baadhi ya nyaraka alizokuwa nazo mkononi. Yeye na Bebe wameshafika nje ya hoteli kuepusha usumbufu wa mashabiki na adha zisizohitajika. "Na kama ujuavyo, wewe sa'hivi ni mtu huru. Unayo maamuzi ya kufanya kitu chochote unachokitaka. Haya, kuna hizi hapa..." akamkabidhi nyaraka zile ili azisome. Bebe akazipekua upesi upesi bila kuzitilia maanani. Akatabasamu na kutikisa kichwa katika namna ya kukubali. "Ni sawa tu Daddy. Sina pingamizi!" Akazipanga na kumrudishia bwana Didas. "Ina...ina maana umekubali au? Ume...umezisoma zote kweli?" Didas akahoji kwa kubabaika. "Sasa kwa nini nikatae? Maana hapo kwenye kila ofa kuna malipo mazuri. Na hili ni suala litakalotufaidisha sisi sote, mimi na kampuni." Bebe akamaliza kwa kutabasamu. Tabasamu lililomuambukiza Didas, naye akatabasamu pia, tabasamu la kuigiza lililoambatana na wasiwasi. Alichokitamka Bebe kilimuonesha waziwazi, faida iliyokuwa mezani mara tu Bebe atakapokodiwa na kampuni nyingine kutoka kwao. Hofu aliyokuwa nayo ni endapo tu Bebe atapata ofa kubwa zaidi itakayomtangazia malipo ya kiwango cha juu kuizidi kampuni yake. Huenda huo ndio ukawa mkono wa kwa heri kwake na akampoteza Bebe moja kwa moja. Tabasamu lake likayeyuka mara moja alipolifikiria hili. Akahamishia macho yake kwenye zile karatasi na barua zilizokuwa mkononi mwake. Akajitia kuzisoma upya...akatishika. Hakika kurasa za mikataba hii zilifoka utajiri wa pesa za kutosha. Pesa zenye uzito wa kupasua mizani. Ni kweli kampuni ingefaidika kama tu Bebe akikubali ofa hizi, lakini kwake yeye hakuwa na hitaji la pesa wala utajiri. Hivi ni vitu alivyojenga navyo urafiki tangu zamani. Anataka nini sasa? Jibu lake likawa jepesi tu...Bebe. Huyu hapa aliye mbele yake. Alitamani amtunze na awe karibu yake daima! Na hapa akayarudisha upya macho yake usoni kwa binti huyu mrembo aliyekuwa bado ana cheche za lile tabasamu lake. Didas akatabasamu upya na kutamka, "Nakupenda sana Bebe!" Zile cheche zikasuguana na kuunda moto mpya wa tabasamu usoni kwa Bebe. "Nakupenda pia!" Akamjibu na kumsogelea karibu zaidi. Wakakumbatiana na papi za midomo yao zikagusana, Zikaruhusu ndimi zao kupinduana, Wakajitahidi kujizuia, si wakashindwa bwana! Joto la miili yao likapanda bila hiyana, Kila mtu na ashiki yake, tayari kupambana, "Si hapa Daddy..." Bebe akamsukuma kwa upole. Huku akiyalegeza macho yake. Jasho lilianza kumvuja Didas akiwa anahema juujuu. Macho yake yanapepesa huku na kule, wasiwasi na aibu vimemvamia kwa nguvu. "Hii si hoteli hii? Ngoja nikalipie chumba." Akajiwahi. Haooo....wakazama ndani ya hoteli ya nyota tano. Ikamlazimu Didas ateketeze mamilioni ya fedha, kwa ajili ya burudani ya usiku mmoja tu akiwa na Bebe. Madaraja ya maisha! ------------- Akiwa mbele ya kompyuta yake ndogo, J4 alikuwa makini sana na kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kwenye skrini ya kompyuta hii. Sikio lake linayanasa mawimbi ya sauti na macho yake yana na umakini mkubwa kuzitazama picha zote anazoweza kuziona mbele yake. Mkono wake wa kushoto ulikuwa na kalamu na kando yake palikuwa na kidaftari kidogo alichokuwa anaandika kila taarifa aliyoipokea na kuipa umuhimu katika shughuli hii. Ni shughuli gani? Anajua mwenyewe. Mara anakunja ndita na kuihamishia kalamu ile mdomoni kwa dakika kadhaa. Kisha anaendelea kuandika. Ghafla simu yake ya mkononi ikaita. Jina la aliyempigia lilisomeka kama D, akatabasamu. Ni yuleyule swahibu wake mkubwa- Dotto. Kabla hajaipokea, akasimamisha shughuli zake kwenye kompyuta, alimuelewa sana huyu rafiki yake. "Kama hana mchongo wa hela ya haraka huko kwenye ulanguzi wake huyu....basi ni wanawake." Akawaza na kuipokea upesi simu ile. Kama kawaida zikaanza salamu zilizoambatana na matusi ambayo daima yalinyimwa uzito wa kuitwa matusi na yakapewa uzito wa salamu ya kawaida. Maongezi yao yakaendelea kisha mara D akauliza swali ambalo lilimrejesha J4 kwenye uso wa kompyuta ile. "Vipi kuhusu yule demu wako mzee...umefikia wapi sasa?" "Duh kaka, kuna ramani moja kali ninaichora hapa, yule atanasa tu. Hutaamini bro, we tulia!" J4 akarekebisha upya video zake alizokuwa akizitazama pale kwenye skrini ya kompyuta yake. "Aah wapi, wewe mzito sana mdogo wangu ile pisi ni ya viwango vya kimataifa!" D akatania huku akitokwa na cheko la dharau. "Hautaamini bro...nitakushangaza!" J4 akamjibu huku akiwa bado anapekua faili ambalo alikuwa liliuvutia umakini wake. "Yule ukimpata nitatembea uchi mitaa yote ya Manzese." D akatamba. "Hebu sikilizia kwanza bro...kata simu chap! Kuna kitu hapa nimekiona!" J4 akamshtua D. "Umeona nini dogo? Umeo-" Alikuwa suala la kusubiri simu ikatwe, akaikata mwenyewe. J4 akainama na kuitazama skrini ya kompyuta ile kwa umakini zaidi, kuliko ule wa awali. Lilikuwepo faili la video ambalo alikuwa analisubiri kwa muda mrefu. Akalifungua. Hamadi! Alichokiona kilimkurupua mara moja kutoka kwenye kiti chake. Akasimama na kutupa ngumi ya ushindi hewani. Huenda huu ulikuwa ni wakati bora zaidi aliokuwa akiusubiri kwa hamu kubwa. Upesi akarejea kwenye kompyuta yake na kucharaza maneno kadhaa ambayo yalilihifadhi faili hili kwa upekee wake peke yake. "Nitawashangaza!" Akatamka na kucheka kwa sauti. Sauti iliyopenya kwenye giza la chumba kile chenye mwanga hafifu, ikadunda kwenye kuta na kuishia mulemule chumbani. Ni siri yake. -------------- Ilikuwa ni siku njema iliyoanza kuonekana tangu asubuhi kama wasemavyo wahenga. Haikuzoeleka hivi kwa Bwana Didas hata kidogo. Asubuhi hii aliamshwa kwa upendo na mke wake wa ndoa, akaandaliwa chai nzito ambayo alishiriki pamoja na familia yake mezani. Mkewe akamkumbusha kuwa bado anampenda. Akambebea briefcase lake mpaka kwenye gari, kisha akamuaga kwa busu zito na kumbato la huba. Ajabu hii! Hivi vitu mara ya mwisho kufanyiwa na mkewe hakumbuki ilikuwa ni lini...ama yeye mwenyewe aliruhusu atendewe hivi lini? Hakumbuki. Alizoea kulumbana na mkewe, hakuwa na muda wa kukaa na familia yake. Daima alidai kuwa amezikumbatia shughuli za ofisini ili ailishe familia yake. Sasa mambo yalikuwa yametakata, madirisha ya neema yamemfungukia na maendeleo yanagombana kuishi naye. Didas akameza funda la mate na kuondoka akiwa mchangamfu mno. "Kuna nini leo?" Alijiuliza. Hata barabarani hakukuwa na foleni kama alivyotarajia. Akafika ofisini mapema, yeye kama mkurugenzi siku hii akawa mfano bora wa kuigwa. Alifika hata kabla ya karani wake. Siku hii hakuwa na mafaili ya kushughulikia zaidi ya kusaini fedha kadha wa kadha zinazoingia kama faida. Ilikuwa ni zaidi ya neema. Bwana Didas akafumba macho yake na kutabasamu. Kila alipoyafikiria mafanikio, jina Bebe likatangulia. Bebe alikuwa ni ufunguo wa kila kitu alichokuwa akihitaji kwenye maisha yake. Akasimama na kutoka nje ya ofisi yake, akahesabu hatua zake akiwa mwingi wa furaha mpaka kwenye roshani iliyokuwa katika ghorofa ile. Hapa aliweza kuyatazama majengo kadhaa ya jiji la Dar es Salaam na pilikapilika zilizokuwa zinaendelea ndani yake. Akaifikiria fahari yake iliyomjia katika namna ya ajabu na haraka tangu amemfahamu Bebe. Akiwa kwenye fikra hii, simu yake ikaita na alipoitazama ilikuwa ni namba ngeni iliyompigia. Akafikiria kuipuuza lakini akachelea kuwa huenda ni mteja ama ofa mpya inabisha hodi. "Namna gani bwana...mbona namba ya simu ya mezani inajulikana? Eboh!" Akasonya na kuipokea akiwa amekunja sura. Hakuzungumza kwanza, akasikilizia upande wa pili uliopiga. "Bwana Didas habari yako!" Ilikuwa sauti ya kiume, iliyojaa ubichi. Angeweza kuidai salamu kama akitaka. "Salama! Naongea na nani?" Akajibu kwa kifupi. "Utanifahamu tu kiongozi wala usiwe na haraka. Nina ujumbe wako tu hapa, ambao-" akakatishwa. "Mimi unanifahamu hongera kwa hilo. Lakini mimi bado sijakufahamu. Kama huwezi kujitambulisha sina haja ya kuzungumza na wewe!" Akataka kukata simu lakini akagundua kuwa hawezi kuikata. "Taratibu kiongozi taratibu...haya maongezi ni yangu mimi na wewe tu. Hakuna mtu anayesikia wala anayeweza kuyafikia, kuwa na amani kabisa." Sauti ile ya kijana wa kiume ikarindima. "Wewe ni nani kijana?" Didas akauliza baada ya kuona jitihada za kukata simu ile zimeshindikana. "Utanifahamu hivi punde tu wala usijali. Hii simu huwezi kuikata, unachotakiwa kufanya sasa hivi ni kufungua mtandao wako wa WhatsApp na kutazama ujumbe niliokutumia. Baada ya hapo nitafute kabla ya adhana ya saa saba! Shime.." Simu ile ikakatwa. "Kelbu!" Didas akarusha tusi. "Hii mihadarati na bange vitakuja kutuharibia taifa." Akaweka nukta. Moyo wake ukadunda kwa nguvu baada ya kukumbuka maelekezo aliyopewa. Upesi akaingia katika mtandao wa WhatsApp na kupekua jumbe kadha wa kadha zilizoingia hivi punde. Kweli, akaona ujumbe kutoka kwa namba ngeni. Akaufungua! Lilikuwa ni faili dogo tu la video lililoambatana na ujumbe, "Hiki ni kipande kidogo tu cha keki nzima!" Akaufungua ujumbe ule. Ilikuwa ni video...mara ghafla zikasikika sauti za miguno ya mahaba! Akapunguza sauti ya simu upesi akihofia sauti ile kusikika na watu. "Kijana mjinga sana huyu, anafikiri kila mtu anapenda hizi video za uchafu?" Akatazama vizuri, ilikuwa ni video iliyounganishwa katika namna isiyoeleweka kamera ilikuwa upande gani. "Kina nani hawa?" Akakaza macho yake. Alikuwa ni yeye na Bebe. ------------- Nimekuwa bize kidogo wakati huu... Lakini hakuna kitakachonizuia kuitumikia fasihi. Tusiache kusambaza link ya chaneli yetu. Itaendelea Alhamisi
Image from MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶: RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU Y...
❤️ 👍 🙏 8

Comments