
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
May 22, 2025 at 08:43 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA*
MTUNZI; *GODLOVE KABATI*
KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel*
WhatsApp; 0763204351
-----------------
SEHEMU YA TISA
*Usijidaganye...*
*Siri ni ya mtu mmoja tu.*
*Ikiwa ya wawili hiyo siyo siri tena, itatambaa kwa kasi ya ajabu...ikiwa na onyo lilelile la "Usimwambie mtu, hata mimi nimeambiwa nisiseme."*
*Hii ni sehemu ya tisa.*
TAHARUKI!
Aliyafikicha macho yake kwa viganja vya mikono yake ili ajihakikishie kuwa ile sio ndoto. Kisha akaigeuza ile simu ili aone kama ni ya kwake au labda ni ya mtu mwingine. Nayo ikawa ni kama inamwonya kuwa chondechonde, asiikane. Akaitambua kuwa ni simu yake.
Hayo hayakutosha.
Akaitazama video ile kwa mara nyingine. Mara ya nne.
Akajihakikishia kuwa hawa viumbe wanaopinduana kwenye video hii anawatambua. Huyu wa kiume hakumtambua kwa sura na majina tu, alimtambua mpaka kiroho na kimwili.
Alikuwa ni yeye mwenyewe.
Didas akajipapasa mfukoni mwake na kutoa leso. Huku akiitazama simu yake, akajipangusa matone ya jasho yaliyokuwa yameanza kuota kimafungu kwenye paji la uso wake. Yakatengeneza michirizi kwenye shingo lake.
Simu ikamponyoka na kuanguka sakafuni. Hapa akagundua kuwa hata mwili wake ulimtetemeka sana, ni kama ulioshtushwa na video hii ya ajabu.
Akainama na kuikota upesi akichelea kuonekana na mtu yeyote eneo lile licha ya kwamba alikuwa peke yake eneo hili.
Asubuhi hii ya saa tatu kasoro, joto la mwili likamzidia. Koti la suti yake nadhifu akaliona kama mzigo mkubwa wa kilo hamsini juu ya mwili wake, akalivua.
Tai yake shingoni akaiona kama kitanzi kilicho tayari kumpa mkataba wa kuiaga dunia, akailegeza katika namna ya haraka mpaka akaichomoa katika fundo lake.
Didas alibabaika.
Eneo lile ambalo dakika kadhaa nyuma aliliamini kama eneo lake bora kwa ajili ya mapumziko, akaliona sio salama tena.
Simu yake akaiona kama bomu ambalo muda wowote linaweza kulipuka kama tu ikiwa mkononi mwa watu wengine. Akaitia kwenye mfuko wa suruali lake kwa umakini mkubwa kisha akapiga hatua kubwa kubwa kukitafuta chumba cha ofisi yake.
Njia nzima kuelekea ofisini mwake, macho yake ni kama yametiwa kiwi. Hakuona wala kutambua mtu au kitu chochote.
Wafanyakazi wakamshangaa,
"Bosi amekuwaje tena?" Waliulizana na hakuna aliyekuwa na majibu.
Siku hii Didas alionekana kuwa wa tofauti kwao kuanzia asubuhi.
Aliwahi mapema kabla yao, alikuwa mwenye tabasamu na bashasha tele usoni na alikuwa mchangamfu mno kuliko walivyomzoea.
Lakini ajabu ndani ya kipimo cha masaa mawili kama sio moja, Bosi wao Didas huyu hapa amebadilika.
Miguu yake inapishana kwa kasi koridoni. Anahema juu juu, koti mkononi, tai imemlegea shingoni.
Didas amepagawa!
"Sipokei simu wala mtu yeyote kuanzia muda huu. Nina kazi ya maana sana naifanya ofisini, sitaki usumbufu!" Yalikuwa ni maagizo yaliyotolewa na sauti inayoamrisha kutoka kwa Didas kwenda kwa karani wake.
"Sawa bo-" Hakusubiri jibu. Upesi akauvamia mlango wa ofisi yake na kuzama ndani, kisha akaubamiza mlango kwa nguvu na kitasa kikasikika kikitekenywa na ufunguo kwa ndani.
"Kha! Kulikoni tena?" Karani huyu mrembo wa kike ,akapigwa na butwaa.
Huko ndani, Didas akazima kila kifaa cha umeme alichokiona kwa hofu ya kuvujisha kile anachotaka kukifanya, safari hii hakutaka kufanya makosa.
Akaikagua ofisi yake kwa umakini akihofia kuwa labda kuna vinasa sauti vilivyotegwa, visije vikamtia upya majaribuni.
Aliogopa sana. Akamuogopa sana yule mtu aliyempigia simu na kumpa maelekezo kama haya yaliyoambatana na hii video ya aibu.
"Ameturekodi muda gani huyu hayawani?" Akajiuliza yeye na nafsi yake.
Kabla hajaanza kugawanya lawama, akajipa dakika chache za kukaa na kutafakari.
Akiwa ameketi juu ya kiti chake kikubwa kinachonesa qmbacho muda huu kilikiwa kigumu kama chuma, akavua shati na kubaki na fulana.
"Labda pale hotelini walitufanyia uhuni? Au...walitega kamera kwenye koti langu? Au Bebe...hebu ngoja!"
Akaipekua orodha ya namba za mawasiliano kwenye simu yake, akitafuta namba ya Bebe. Akampigia, simu yake haikupokelewa. Akampigia mara ya pili, ya tatu na ya nne bila mafanikio.
"Shit!"
Akasonya na kupiga ngumi juu ya meza yake kwa nguvu. Akiwa kwenye taharuki, akajikuna kidevu chake kilichosheni ndevu nyingi.
Fikra zake zikapaa na kumuonesha kila rangi ya hatari ambayo hakuwahi kuomba imkute maishani mwake.
*"Hiki ni kipande kidogo tu cha keki nzima."* akausoma upya ule ujumbe ulioambatana na video ile. Safari hii aliuona ni kama umeandikwa kwa mwandiko wa kishetani, na aliyeuandika anamcheka kwa dharau.
Didaa akatetemeka kwa hofu.
"Ni kipande cha keki. Labda ipo au zipo ndefu zaidi ya hapa. Labda huyu jamaa video zangu za siku nyingi, hata kabla ya hii ya jana." Akatamka kwa huzuni.
"Vipi...vipi kama akizitundika video zote mitandaoni na watu wa rika zote wazione. Nitaweka wapi sura yangu mimi Dida?!" Akahamishia mikono yake kichwani. Kumbukumbu zake zikamsulubu, zikimkumbusha matukio na matendo yake yote maovu aliyoyafanya na Bebe.
Chozi likamdondoka!
Akafikiria namna atakavyoaibika, namna atakavyoichafua sura ya kampuni. Akaona waziwazi atakavyoporomosha soko la bidhaa zao, atakavyouangusha ufalme wa biashara uliojengwa kwa muda mrefu tena kwa jasho, machozi na damu.
"Eeh Mungu wangu!" Macho yake yakawa ya moto kwa machozi. Alikuwa na muda mrefu tangu ametoa machozi, lakini leo hii hofu ya matokeo ya kumbukumbu ya dhambi zake za nyuma, inamtoa machozi.
Alipokumbuka kuwa hata mwanaye mkubwa Junior ana simu janja aliyompatia kama zawadi, Didas Ambrozi akahama kutoka kwenye kiti na kuchutama sakafuni.
"Shenzi kabisa!" Akafoka kimyakimya.
"Mtoto mdogo kama yule anamiliki vipi simu ya mkononi?" Haikujulikana kama anamlaumu mwanaye aua anajilaumu yeye mwenyewe aliyempatia. Mwanaye ambaye nd'o kwanza yuko elimu ya msingi, darasa la sita.
Tena ni mjuvi na mtundu wa kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii. Hakuna kurasa yoyote ya watu maarufu ambayo hakuijua.
Didas siku zote alichekelea na kudai kuwa hiki ni kizazi kipya, kizazi cha teknolojia, hivyo haoni kosa la mtoto mdogo kuijua mitandao na kuitumia.
Alichoka!
Fikra hii ikaambatana moja kwa moja na matokeo baada ya mkewe kuiona video hii ambayo aliitafsiri kuwa ni video chafu. Kwa nini hakukifikiria kitendo kile alichokifanya kuwa kichafu na badala yake aichafue video? Alijua mwenyewe.
Kwa mara nyingine akaona kuwa huenda hii ikawa hoja kubwa na yenye mashiko kwa mkewe anayelumbana naye kila uchwao.
Akaifikiria heshima aliyojijengea katika kanisa lake la kiinjili analoabudia, heshima na busara zake vikampatia cheo cha kuitwa *mzee wa kanisa*.
Hamadi!
"Nitapoteza kila kitu!" Akatamka kwa sauti ya chini huku akipambana kulifuta jasho usoni mwake.
"Kwamba magazeti yataaandika, SAKATA LA MREMBO FROLA NA BOSI WAKE LAITETEMESHA DAR." Akawaza.
Hakutaka kusubiri mashambulizi haya ya kushtukiza yamfuate alipo...
Akaamua kujihami kwa silaha alizo nazo. Na silaha yake kubwa aliyoitegemea muda huu ni pesa.
"Anataka fedha huyu. Aseme kiasi chochotekile anachokitaka nitampatia! Ili mradi tu, aniondolee hii aibu!"
Akaamua aipigie namba ya mtu yule asiyemfahamu.
Ikapokelewa upesi.
Akaanza kujitetea mara moja,
"Nakusikiliza wewe. Niambie unataka nikulipe sh'ngapi? Nitajie kiasi unachokitaka tuyamalize." Akatamka kwa jazba iliyochanganyikana na woga.
"Kunilipa? Kiasi? Sielewi unaongelea nini mzee wangu." Katika namna isiyotegemewa sauti ile ikajibu kwa utulivu.
"Come on! Nisikilize kijana...usitake kushupaza shingo yako bwana. Ni matarajio yangu kuwa unaelewa ni nini namaanisha. Tafadhali, niambie unataka kiasi gani tuimalize hii kesi." Didas akirejea taratibu juu ya kiti chake akarusha karata yake nyingine.
"Mzee...mimi nimebahatika kukufahamu japo kwa jina, lakini wewe hunijui. Nimefanya wema wa kukutumia kipande cha keki tufaidi pamoja. Na nikakueleza kuwa uniafute ili tujadiliane juu ya ladha yake, hivyo tu!" Akamalizia sentensi yake akiwa na cheko la dharau.
Didas akazidi kuchanganyikiwa, akatoka kwenye kiti chake kwa mara nyingine, akaanza kutembea akizunguka zunguka mule ndani. Alitamani amjibu kwa kumrushia matusi mazito lakini wakati huu alihitajika awe mjinga na mnyonge, akachagua kubaki kimya.
"Nisikilize mzee wangu..." sauti ile ikatangaza ubabe.
"Maelekezo yote atakupatia huyo malaya wako. Ni maelekezo yanayohitaji utekelezaji wa haraka, mna siku moja tu. Ama sivyo vyombo vya habari na mitandao vitapata habari mpya inayovutia!" Sauti ile ya kukoroma ikaweka kituo na simu ikakatwa!
Moyo wa Didas ukaruka mapigo kadhaa baada ya kusikia maneno yale. Kwa mara ya kwanza maishani mwake akamuweka Bebe katika orodha ya viumbe hatarishi wa kuogopwa. Akawa na asilimia zilizotosha kuvunja imani yake kwake.
"Kumbe anahusika!" Donge kubwa la hasira likajiunda kifuani mwake.
Akiwa harakati za kuvaa upya mavazi yake ili aondoke ofisini mule, simu yake ikaita.
Mpigaji sio mwingine bali ni Bebe. Akashusha pumzi na kuitazama simu ile. Akaipokea akiwa anatukana matusi mengi kimoyomoyo.
Lakini ajabu!
Akapokelewa na sauti ya kilio na malalamiko.
"Daddy...tuna siku moja tu Daddy!" Bee alikuwa analia na kuomboleza. Achana na kilio chake wala maombolezo yake. Kilichomzuzua Didas ni ile sauti nzuri na tamu ya Bebe, hasa akiwa kwenye kilio.
Hata kama angekuwa anaigiza, kilio chake kingetosha kabisa kumpa msamaha na akauepuka moto wa milele.
"Kuna nini Bebe? Mbo..mbona unalia eh?" Didas anazuga haelewi kinachoendelea, amevaa ujasiri bandia wa kiume.
"Ametupa siku moja tu mpenzi wangu...siku moja tu!" Kitendo cha kuitwa *mpenzi* kikawa kama msumari wa moto kwenye kifua cha ujasiri wa Didas.
Akasahau hasira yake yote aliyokuwa nayo dhidi ya Bebe. Akachukua jukumu la kumbembeleza na kumuondoloea hofu.
"Usijali kipenzi...kila kitu kitakuwa sawa. Hili nitalimaliza mimi mwenyewe dear. Huyu nyang'au nitamtia adabu, hatatuchezea michezo yake tena! Uko wapi sasa hivi?" Didas akajitutumua na kuonyesha uanaume wake.
Bebe akamueleza kuwa yuko nyumbani kwake. Wakapanga mahali pa kukutana ili wachore ramani ya kuokoa kwenye msitu huu mpya walioingia na kupotea ndani yake.
Didas akiwa na huruma tani mia kwa Bebe.
"Huyu dogo atanitambua mimi ni nani!" Akaweka nia yakumuangamiza huyo aliyewachezea mchezo huu.
Hakujua! Hakujua!
---------------------------
Itaendelea Jumamosi
Tuendelee kusambaza link ya chaneli na kutoa maoni yetu kupitia 0763205351.
❤️
❤🔥
4