
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
May 26, 2025 at 07:49 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA*
MTUNZI; *GODLOVE KABATI*
KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel*
WhatsApp; 0763204351
-----------------
SEHEMU YA KUMI
*KUMBUKA...*
*Usimpe mwanadamu asilimia zako zote za uaminifu, hasa kila linapofikia suala la pesa.*
*Hapa usishangae sana yule rafiki yako unayemuamini atakapogeuka na kuwa kama mnyamamwitu mkali, aliyetayari kukurarua!*
*Mungu alimuumba mwanadamu,*
*Mwanadamu akaiumba fedha,*
*Ajabu! Fedha iliyoumbwa na mwanadamu, inamchanganya na kumuweusha.*
*Tafsiri kadri ya uelewa wako!*
*Na hii ni sehemu ya kumi...*
Lilikuwa ni anga la saa saba mchana, lililomiliki jua la utosi, jua linalofukuta joto zito linalokera lakini lililozoeleka haswa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Jua hili liliendelea kufanya ukatili wake kwa watu wenye vichwa vyenye mtindo wa nywele aina ya *kipara* , kama tu kipara ni mtindo wa nywele.
Naam, hata kipara kinachong'aa cha Didas Ambrozi kilipokelewa vyema na miale ya jua hili lenye hasira punde tu aliposhuka kutoka kwenye gari lake, nje ya mgahawa aliokubaliana kukutana na Bebe.
Hofu ya masaibu yaliyomkuta ikaungana na ukali wa jua hili, vikamchanganya na kumkasirisha.
Akakunja ndita usoni baada ya kugundua kuwa asingeweza kulitazama jua hili, ili walau alirushie tusi.
"Hili jua limetumwa au?" Akalalamika huku akikihifadhi kipara chake kitukufu ndani ya kofia.
Akapiga hatua ndefu ndefu na kuingia ndani ya mgahawa ule. Haikumchukua sekunde kumi kabla macho yake hayajainasa nafasi kwenye kona kama alivyokuwa ameelekezwa.
Hapa alikuwa ameketi Bebe. Ambaye ameufunika mwili wake gubigubi kwa mtandio, suraye ameipamba kwa miwani kubwa ya jua na kichwa chake kikiwa ndani ya kilemba. Mezani hana chochote kile kinacholika, badala yake ana chupa kubwa ya maji ya kunywa. Ameketi kwa utulivu, mkono wa kushoto umeshika tama na ule wa kulia ukiigonga gonga glasi ile ya kioo iliyojazwa maji.
Alifanana na mwanamke ambaye kama hayuko kwenye maombolezo basi alikuwa na lengo lake binafsi. Na kweli, kwake yeye mavazi yote haya hayakuwa na lengo tofauti zaidi ya kuepuka kujulikana na watu, ama kujiepusha na usumbufu usiohitajika kutoka kwa mashabiki zake.
Bahati iliyoje, muda huu hapakuwa na watu wengi ndani ya mgahawa.
Didas akamfikia na kumsalimia, lakini hakujibiwa.
Hapa akagundua tofauti nyingine ya ziada, ambayo ni kama aliitegemea abadani.
Bebe hakuwa na furaha.
Mhudumu aliyekuwa karibu akaichangamkia meza yao na kumuuliza Disas chakula ambacho anakihitaji kwa mlo.
"Nitakuita!" Jibu fupi lilitosha kuuzima ule uchangamfu wa mhudumu yule, ambaye aliificha hasira yake kwenye tabasamu la uongo.
Kimyakimya Didas akaketi katika kiti mkabala, akamsogelea kwa ukaribu na kumtazama usoni. Bebe akavuta kamasi puani mwake katika namna ya huzuni, hapa akavua miwani na kutazamana na Didas uso kwa uso. Macho ya Bebe yalikuwa yamevimba baada ya kulia kwa muda mrefu.
Walitazamana bila kutamka lolote. Didas akaamua kukohoa kidogo na kuuvunja ukimya,
"Nisikilize Bebe...kila kitu kitakuwa sawa. Hauna haja ya kulia na kuhuzunika wakati mimi nipo. Usijali, nitampatia chochote anachokitaka. Kama anachokitaka ni fedha, hilo sio tatizo kwa-" Didas akakatishwa.
"Ulivyoongea naye mara ya mwisho amekueleza anachokihitaji?" Sauti ya Bebe iliokata tamaa ikatupa swali.
"Uum...yeye nimeongea naye asubuhi hii hii, lakini inaonekana ana kiburi mwanaharamu yule, nitamfanya aju-" Didas aliyeanza kubwata akakatishwa.
"Umeshafahamu anachokitaka?" Bebe akarudia swali lile. Sasa ni mtulivu, haonekani kuwa na wasiwasi na wala hana papara katika kuongea kwake.
Mchirizi mwembamba wa jasho ukamtambaa bwana Didas kutoka kwenye paji la uso wake, akavua kofia yake na kuwahi kuufuta kabla haujafika kwenye shavu lake la kulia.
"Hapana hajaniambia...kanieleza kuwa amekupatia maelekezo yote wewe." Akatamka huku akipambana kupangusa matone yote ya jasho yaliyotia kambi kwenye kipara chake na paji lake la uso.
Bebe akashusha pumzi ndefu na kutamka,
"Ana mahitaji mawili tu. Na kulingana na alivyodai, anataka yatekelezwe ndani ya masaa ishirini nne kuanzia kesho. Kwa maana hiyo mpaka kufikia keshokutwa, kasema lolote litakalotokea tusimlaumu."
Didas akakurupuka na kasi yake ya kupumua ikaongezeka maradufu,
"Ana..anataka nini. Niambie Bebe anataka nini?" Akauliza akiwa amemuinamia Bebe kwa ukaribu zaidi. Macho yamemtoka pima yakikagua huku na huko kama kuna wateja ambao wanayafuatilia maongezi yao kwa ukaribu.
Bebe akaketi vyema na kuendelea,
"Daddy, kama ikitokea hatujamtimizia kile anachokitaka. Basi ujue kuwa huo nd'o mwanzo wa mimi na wewe kupakwa matope.
Akheri yangu mimi nisiye na ndugu, lakini jifikirie wewe mpenzi.
Mke wako, wanao, jamii inayokuzunguka na mbaya zaidi sifa ya kampuni yetu." Alipofika hapa Bebe akabadilika ghafla na kuwa mnyonge....ule ujasiri wake ukayeyuka ghafla na machozi yakachukua nafasi.
"Nisaidie Daddy....naogopa sana. Jina langu limekuwa kubwa! Nafahamika na watu wengi sana. Kama ikitokea akavujisha hizo video, sifa yangu niliyo nayo itakuwa imenajisiwa tayari. Hakuna dili lolote la promotion nitakalolipata!" Akainama chini na kuuficha uso wake ndani ya ule mtandio, akaanza kulia.
Didas akasimama mara moja, akaiacha kiti chake na kuketi sambamba na Bebe. Akamkumbatia kifuani mwake na akachukua jukumu jipya la kumbembeleza.
"Usilie mpenzi...hili ni jambo dogo sana mbona. We niambie anataka nini, nitajie hayo matakwa yake huyo mjinga mmoja. Nina hela nyingi mimi, hata akitaka nimpe benki nampa!" Didas akatamba.
Ni kweli kwake yeye neno fedha halikumtetemesha hata kidogo. Na ni jambo gani kubwa ambalo mtesi huyu angeliomba kama sio fedha? Alijiamini.
Sura yake ikingali bado ndani ya mtandio ule, Mdomo wa Bebe ukawa kwenye mapambano makali na pua, iliyojikita kwenye kuvuta kamasi.
"Anataka milioni mia." Sauti nyepesi yenye kilio ikatamka sentensi ile ambayo kidogo iliufanya moyo wa Didas uruke mapigo kadhaa.
"Milioni mia?!" Haikueleweka kama Didas anauliza kwa kutosikia vyema au anakishangaa kiasi kilichotajwa.
Lakini Bebe hakuwa na muda wa kumjibu, yeye akaendelea kuwasilisha.
"Kingi...kingineee..." Akarejea upya kwenye kilio. Tena safari hii akalia kwa nguvu zaidi ya mwanzo.
Baadhi ya watu waliokuwa karibu na meza yao wakawatazama kwa udadisi. Kijana mmojawapo miongoni mwa wateja akasogea kwenye meza yao na kuuliza,
"Aiseee kiongozi, habari yako bwana. Vipi shemeji ana tatizo lolote?"
"Ha-hapana kaka...ni kichwa tu kinamsumbua, si unajua tena wanavyodeka hawa heheheh." Didas akajichekesha ili kuonesha kuwa lile halikuwa jambo kubwa.
Kijana naye akajichekesha na kuondoka kishingo upande.
"Niambie jambo la pili Bebe,niambie..." akamnong'oneza.
"Anataka uuvunje mkataba wangu na kampuni yako!"
Hali ya hewa ikambadilika Didas ghafla, mijongeo ya viumbe kama vipepeo...ikaanza kupepea tumboni mwake, akahisi utumbo mdogo umechanganyikana na utumbo mkubwa. Taratibu akamuachia Bebe, akakikamata kitambaa chake na kujipangusa jasho lililokuwa likitambaa shingoni mwake.
Alichoka!
Bebe akajipangusa machozi na kuuibua uso wake uliokuwa umetota kwa machozi. Akamtazama Didas ambaye alionekana waziwazi kuwa amechanganyikiwa.
Huenda hoja ya milioni mia haikumbambaisha, lakini hili takwa la pili lilikuwa kama ngumi ya tumbo kwake.
"Hivi huyu mshenzi ni nani?!" Didas akanong'ona huku akikiuma kidole chake kwa hasira.
"Hawezi kuwa mmoja kati ya wafanyakazi wa ile hoteli kweli?" Aliongeza swali ambalo halikujibiwa moja kwa moja na Bebe.
Akashusha pumzi ndefu na kumtazama Bebe. Macho lake safari hii yalivaa utu mpya, hayakuwa yake ya huruma na wala hayakubeba huba. Alimtazama Bebe kwa macho ya tofauti na Bebe akaligundua hilo.
"Ni kwa nini kakupatia wewe haya maelekezo na sio mimi? Au kuna kitu unanificha Bebe."
Akiwa na macho yanayoonesha wasiwasi, Didas akatupa swali kwa Bebe.
"Unataka kumaanisha nini? Kwamba hauniamini ama?" Bebe akajitetea, sauti yake ikapata nguvu kiasi.
"Simaanishi hivyo...lakini huenda ikawa hivyo. Hii ni dhania yangu tu." Didas akakoroma.
"Dhahania? Didas...hili ni tatizo letu sote. Kwa hio unataka kusema kuwa nimekula njama na huyu mtu, nikatega kamera pale chumbani? Serious..?" Bebe naye akapandisha sauti...ndita zimeuvamia uso wake mdogo.
Kitendo cha kuitwa kwa jina lake la kwanza, *Didas*. Kikamshtua sana Bwana Didas, haikuwa kawaida kwa Bebe kumuita jina hili moja kwa moja.
Ikawa ni kama wanapandishiana sauti na kuwavutia wateja waliokuwapo mule ndani. Waama walionekana kama watu wa kushangaza sana. Ni dakika moja tu iliyopita, walikuwa wanabembelezana lakini sasa wanalumbana.
Didas akainamisha kichwa chake kwa kukiegamiza kwenye viganja vya mikono yake akisikitika. Aliuona uzito wa dunia ukimuinamia moja kwa moja na kumzidia.
Hakutegemea kama video ile ama zile kama tu ziko nyinginge nyingi, kuwa zimgharimu kiasi cha milioni mia moja. Hili kwake angelihesabu kama hasara ya kununua kipande cha jiwe kwa kubadilishana na almasi kubwa inayong'ara.
Alikuwa tayari kuipokea hasara hii, sio mara yake ya kwanza kukutana na hasara abadani. Japo hii ilikuwa imemtazama moja kwa moja usoni.
Lakini hili suala la kukatisha mkataba wake na Bebe, aliliona kama mpango ambao umekaa kimtego. Akiwa na wasiwasi kuwa labda Bebe amemchoka na amekula njama ili akapate malisho mapya katika sehemu nyingine. Wasiwasi wake bado ulikuwa palepale kwenye dhahania.
"Nataka kumjua huyu mtu!" Didas akakoroma.
"Umjue? Huo muda wa kusubiri mjuane utautoa wapi Daddy? Tuna siku moja tu. Only one day." Kidole chake kimoja cha shahada kinaelea hewani kuashiria namba ya siku iliyobaki na sauti yake nzuri ya kubembeleza inatangaza hofu yake.
Vyote kwa Didas wakati huu havikuwa na nguvu yoyote ile. Kidole kile alikiona kama mdomo wa bunduki iliyoshikwa na gaidi. Na sauti ile aliiona kama sauti ya msaliti.
"Bebe umenisaliti!" Didas akatamka huku macho yake yakionekana kung'aa kwa machozi yanayolengalenga. Bebe akaonekana kubabaika, hajui amjibu nini.
"Sawa nimekubali!" Sauti tatanishi ikakitoroka kinywa cha Didas.
"We si unawasiliana naye huyo jamaa sio? Wewe nd'o anayekupa maelekezo yote au sio? Haya mwambie hivi, na mimi nina matakwa yangu hapa. Mwambie nataka nionane naye uso kwa uso. Atapata noti zake anazotaka na mkataba nitauchana mbele yake! Shwaini!" Akasimama kwa ghadhabu na kuivaa kofia yake. Kisha upesi akaondoka hotelini pale akiwa amevimba kwa hasira.
Akamuacha Bebe ambaye alichagua kubaki kwenye utulivu. Utulivu ambao huenda aliuhitaji mno kwa wakati huu.
Kuondoka kwa Didas kukapishana na hatua za yule yule kijana aliyesogea mezani pale kuwajulia hali wakati ule.
Muda huu hakuja kumjulia mtu hali, bali aliketi moja kwa moja kwenye kiti kilekile alichopishwa na Didas.
Moja kwa moja akatazamana na Bebe.
"Vipi amekubali?" Likawa swali lake la kwanza.
"Mh...hapana, bado hajakubali moja kwa moja. Inaonekana ameushtukia mpango wetu, hasa huu wa kuvunja mkataba." Bebe akamjibu kwa utulivu. Sauti yake ikiwa na nidhamu ya hali ya juu.
---------------------------
Namna gani hapa!
Ina maana Bebe anahusika kwenye hili dili?Na huyu kijana ni nani?
Hebu ngoja tuone, ni nini kalamu ya mwandishi itatupatia.
Reaction! Reaction! Reaction!.....reaction zenu ni muhimu jama.
Bila kusahau maoni kwenye namba 0763204351.
Hii itaendelea...
❤️
🔥
❤🔥
🥹
11