MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
May 31, 2025 at 11:11 PM
*`PAZIA LA FILAMU`* 📽🎬 *FREDDY* (2022) Mungu alimbariki sana Freddy Ginwala, Akamuumbia moyo wa dhahabu, moyo wenye utajiri wa adili na ibada. Akamjaalia tabia njema zilizoambatana na adabu iliyotukuka. Mungu akamuongezea na mali za kumtosha alizoridhika nazo hakika. Unadhani Mungu wetu ana kikomo kwenye kumimina neema zake? La hasha! Freddy Ginwala, alikuwa na kazi nzuri ya udaktari wa vinywa na meno. Kazi hii ikampa umaarufu mkubwa kwenye jamii yake. Ikampa heshima na jina bora sana miongoni mwa vinywa vya watu. Freddy angedai nini kingine? Lakini hakika Mungu wetu hatupi vyote! Maadamu sio kila kitu kinatufaa. Na hata kikitufaa, huenda kina muda wake maalumu. Mungu hutupatia vitu hivi kwa muda wake, na muda wake daima ni sahihi! Naam, Freddy Ginwala hakuwa na mwenza wa maisha. Alitamani siku moja akutane na binti mrembo. Amuoneshe namna sahihi ya kulitumikia neno *Nakupenda*. Wapendane kwa damu na nyama, roho na mwili. Wafunge ndoa na wajenge familia bora. Hili kwake lilikuwa ni deni kubwa ambalo nafsi yake ilimdai usiku na mchana. Alikosa furaha na amani. Katika umri wake huu wa miaka takribani 30, hakuwahi kujihusisha na mahusiano katika namna yoyote ile. Sahau kuhusu mazoea na wasichana, Freddy alijawa na aibu kila linapofika suala la wasichana. Akajitahidi kutafuta wachumba wa mtandaoni lakini nao hakuwavutia kutokana na aibu yake na mtindo wake wa maisha. Akaamua kuisubiri bahati yake popote pale ambapo itamdondokea. Ni siku moja tu iliyotosha kumbadilisha Freddy. Naam, siku hii akiwa na bibi yake kwenye sherehe fulani, macho yake yakagota moja kwa moja kwa msichana mrembo wa kike aliyekuwa kwenye hafla ile. Angefanya nini sasa badala ya kumtazama tu? Huu nd'o ujasiri pekee aliokuwa nao dhidi ya wanawake. "Mjukuu wangu, ni lini utakuwa na mke?" Lilikuwa swali kutoka kinywani mwa bibi yake lililogeuka mkuki wa sumu masikioni mwa Freddy. Aibu imemjaa, anatetemeka, hajui amjibu nini bibi yake. Familia yake inamtazama kama mtu wa ajabu. "Haya kuna mrembo yule pale, na anaonekana yuko peke yake. Kamchangamkie upesi, huwezi jua. Nenda usiogope wanawake!" Bibi yake akamsurutisha. Freddy akaenda kuijaribu bahati yake. Huenda ni siku hii bahati imemwangukia, yeye alienda kujaribu tu. Akajikuta ameangukia kwa mke wa mtu. Mrembo Kainaaz! Na ni hapa alipokutana na binti Kainaaz kwa mara ya kwanza. Binti ambaye aliuteka moyo wake, nao ukatii bila shuruti. Akaufunga kwenye gereza la mapenzi. Freddy akawa mtumwa wa mapenzi kwa Kainaaz. Huyu ni msichana pekee aliyempokea na kumsikiliza kwa upole kuliko wale wengine wa mitandaoni. Kwa mara ya kwanza Freddy akajihisi amekamilika. Akabadili mtindo wa nywele zake, akanunua nguo mpya, akabadili mpaka mwondoko! Si amepata mpenzi bhana! Kwa nini asing'ae? Akapenda, akafa, akaoza! Zawadi kemkem hazikukatika kwa Kainaaz. Hakujali kuwa huyu ni mke wa mtu au la. E bwana eee, Freddy amependa tayari. Freedy akiwa anapambana kumfanya Kainaaz aifurahie kila dakika anayoiishi hapa duniani, akagundua kuwa binti huyu anapitia mateso makali. Vipigo na manyanyaso vya kila mara kutoka kwa mume wake vilikuwa kama wimbo wa taifa kwake. Alikuwa amevizoea. Freedy alipoligundua hili, akahaidi kumsaidia. "Niambie ukweli unampenda huyu mumeo?" Akamuuliza kwa moyo uliojaa wivu na kisasi. "Japokuwa ananitesa, bado nampenda. Yeye ni mtu mzuri na mwema sana!" Kainaaz akamtetea. "Namna gani anakupiga kila siku na bado unampenda huyu mtu katili? Haya sikia, ninao mpango hapa...em sogea!" Akamnong'oneza mpango wa siri ambao ungekuwa msaada wa moja kwa moja kwake. Msaada ambao ulipakwa rangi zote za dhambi ya mauti. Mapenzi yale yale yaliyosababisha Ngoswe apoteze nyaraka muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi, yakamfanya Freddy abadilike na kuwa kiumbe katili. Ama mapenzi yana nguvu sana jama. Akamvizia mume wa Kainaaz usiku usiku katika mida yake ya kufanya mazoezi ya viungo. Akamuua! Akapambana kuuficha na kuufuta ushahidi, akakamilisha uovu wake. Kwake hili lilikuwa ni jambo la kijasiri zaidi kulifanya tangu azaliwe. Alikuwa analipambania penzi lake kwa Kainaaz. Moyo wake ukiwa na ushindi uliosindikizwa na amani na salama, akarejea kwa Kainaaz akiwa na maua mkononi. Hamadi! Hakuamini kile ambacho macho yake yalikishuhudia. Kainaaz alikuwa na mwanaume mwingine. Mwanaume ambaye alitambulishwa kwa jina la mpenzi. Maajabu! Kainaaz alimtumia Freddy kufanya mauaji haya ili tu apate umiliki wa mali za mumewe na awe huru. Shoti ilitambaa kwenye mwili wa Freddy, hakuamini kile alichoambiwa. Akajaribu kumkumbusha Kainaaz ahadi zao na maneno yote matamu walizowahi kupeana. Jambo pekee aliloambulia ni kufukuzwa kama mbwa. Kitendo alichokifanya akikusudia kihesabike kama upendo, kikawa kama pingu za chuma kwake. "Ukiendelea kunifuatilia...nitakushtaki kuwa umemuua mume wangu!" Hakuamini. Ni mapenzi tu. Ni mapenzi ambayo yalimfanya amuuwe mtu asiye kuwa na hatia ili yule ampendaye aishi kwa amani mbali na mateso. Kumbe alikuwa amempenda nyoka mwenye sumu kali. Sumu ambayo inamtambaa kwenye mishipa ya damu yake na kuisuta nafsi yake juu ya dhambi aliyoifanya. Alipenda vibaya, na sasa upendo unampiga visu vya kifua. Freddy Ginwala, Akauzika ule upole na hulka yake ya utulivu. Akavaa kofia mpya ya ukatili. Sasa akawa muwindaji aliye tayari kulipa kisasi katika namna ya kisayansi zaidi. Daktari wa meno akapiga hatua moja kubwa. Simulizi ikageukia upande wa pili. Sasa sio mapenzi tena ni hekaheka na visasi. Ni filamu ya kusisimua yenye mseto mtamu wa hadithi kama asali. Ndani yake kuna mapenzi, visasi na upelelezi wa kisaikolojia. Hutabandua macho yako mara tu utakapoanza kuitazama. Inaitwa FREDDY imetoka mwaka 2022. Imeandikwa na Godlove Kabati ✍🏼
Image from MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶: *`PAZIA LA FILAMU`* 📽🎬   *FREDDY*  (2022)   Mungu alimbariki sana Fr...
❤️ 👍 3

Comments