
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
June 2, 2025 at 08:56 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA*
MTUNZI; *GODLOVE KABATI*
KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel*
WhatsApp; 0763204351
-----------------
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
*Mwanaume mnyime ugali...atakula hata viazi.*
*Mnyime kanzu, atavaa hata kaniki mbovu ama gunia*
*Mnyime salamu, hii ataipata popote pale kwingineko kama sio kwako.*
*Lakini chondechonde, katu usimnyime heshima yake.*
*Na hii ni sehemu ya kumi na moja.*
Siku yake iliyoanza kwa bashasha sasa ilikuwa imegeuka siku mbaya.
"Siku ya shetani hii!" Nafsi yake ilimshtakia,
kila alipolinganisha vibwanga na vibweka vyote vilivyomuandama siku hii.
Didas Ambrozi alikuwa njiani kuelekea asikokujua.
Alikuwa amechanganyikiwa haswaa. Mikono yake ilioshikilia usukani ilikuwa bado inamtetemeka kwa hasira.
Kila mara jina la Bebe likimjia kichwani ana sonya na kutukana kimoyomoyo. Mara nyingine anapiga honi hovyohovyo kwa kuupiga kwa nguvu usukani.
"Nimeyaona macho yake yule mnafiki. Changudoa mkubwa na tapeli kutoka kuzimu. Nimeyaona macho yake, yalikuwa makavu kabisaaa. Malaya yule!" Hatimaye akatamka kwa sauti akilalamika. Sentensi zake zikafuatiwa na honi iliyomkurupua mwendesha baiskeli ambaye aliponea chupuchupu kupitiwa na gari lile lililokuwa kasi.
Didas amechachamaa!
"Machozi yake ni ya kinafiki! Machozi ya wizi kabisa. Nimemuona usoni! Msaliti...mpumbavu." Didas akazidi kulalamika, akatema mate kwa hasira, amesahau kuwa yu ndani ya gari lake zuri la kifahari.
"Yaani jitu pumbavu pumbavu litoke huko kusikojulikana, lile magimbi na ugali lisishibe...halafu liniamrishe eti ooh, nipe milioni mia halafu sitisha mkataba! Mimi huyooo?! Yeye kama nani kwanza."
Didas yu peke yake garini, bado analalamika.
Safari hii ghafla akashika breki zake kwa nguvu almanusura amgonge mlemavu aliyekuwa anavuka barabara kwenye alama za pundamilia.
Nje ya gari, aliweza kuwatazama watembea kwa miguu waliokuwa wamecharuka kwa hasira, ndita zimechoreka kwenye nyuso zao, midomo na vinywa vyao vikionekana kumnenea maneno ya hasira kwa kuaalamika. Vidole vyao vya shahada vikilinyookea gari lake la kifahari lililomficha kwa vioo vyeusi vyenye sifa ya 'Wa ndani anamuona wa nje, lakini huyu wa nje katu, hawezi kuona kilicho ndani.'
Yeye hakuwasikia na akamshukuru sana yule mtu mwerevu aliyebuni vioo vya namna ile. Mzee yule mlemavu alipovuka salama, akachochea upya gari lake na kufyatuka eneo lile.
Baada ya kilomita chache akagundua kuwa anakosa umakini kwenye kuendesha gari. Akaliegesha gari lake kando ya barabara na kutulia akijipa dakika chache ili afanye tafakuri.
Bado mawazo yake yanashindwa kuamini kuwa huenda Bebe amemzunguka na kumchezea shere tena katika namna ya kitapeli.
"Au namsingizia?" Akajihoji.
"Hapana simsingizii!" Akajijibu.
"Hawa malaya wana mambo mengi sana ya ovyo! Wana mitandao yao ya siri ya kufanya uhalifu na dhambi zote zimchukizazo muumba." Sasa Didas akaikumbuka kofia yake ya uzee wa kanisa.
"Yaani afanye uzinifu na uasherati huko halafu nimpe-"
Mawazo yake yakavurugwa na mlio wa simu yake iliyoita kwa ghafla.
Akaitazama kwa hofu, nambari iliyokuwa imempigia wakati huu ilionyesha kuwa ya tofauti kidogo.
Akaitazama kwa sekunde chache. Kumbukumbu zake zikamkumbusha kuwa aliwahi kuziona mahali.
Namba za namna hii hutumiwa na watu wachache sana hasa wale walio kwenye sekta nyeti za kiserikali kama mawaziri au usalama wa taifa.
"Atakuwa nani huyu ambaye sijamsevu?" Didas akaingiwa na hofu akiinua simu yake tayari kwa kuipokea. Alikuwa akifahamiana na viongozi wengi tu wakubwa wa kiserikali, lakini wote alikuwa na mawasiliano nao. Ni kwa namna gani simu hii mpya imjie tena kwenye nyakati kama hizi ambazo anaandamwa na hofu?
"Video zimewafikia!!" Kengele ya hatari ikalia kwenye ubongo wake.
Akaketi vizuri na kujikohoza ili kuweka sawa sauti yake kisha akaipokea simu ile kwa nidhamu na unyenyekevu mkubwa.
"Ha...haloo!"
"Naongea na Didas Kilonzo Ambrozi!" Sauti nzito changamfu iliyoonekana kuwa na haraka ilipepea kutoka kwa mpigaji.
Didas akagutuka.
Kutajwa kwa majina yake matatu kama yalivyo kwenye vyeti vyake vya elimu, kukamshtua. Tena wakati huu hakuitwa bwana au muheshimiwa.
Hakika alikuwa anaongea na mtu mkubwa.
"Naam ni..ni mimi!" Akajibu kwa kigugumizi.
"Unaongea na Special agent YW536 kutoka kitengo cha kiintelijensia na usalama wa mitandao Tanzania." Utambulisho huu ukamfanya Didas apate tumbo la kuhara. Akajishikilia kwa nguvu ili kujizuia.
Mfano wa vitu kama vipepeo, vinapepea tumboni mwake.
"Kwa nini unafanya mambo ya aibu ndugu yangu?" Swali jepesi la kiungwana lakini linalotatanisha likaachika kutoka kwa mpigaji yule.
Mfumo wa upumuaji wa Didas ukabadilika. Pumzi zikaanza kupishana kwa kasi puani mwake, hakujua ajibu nini. Maadamu anayeongea naye ni mtu wa ndani ya mfumo, basi kuna uhakika wa asilimia zote kuwa ameziona video zake.
Hakuwa na sababu yoyote ya kupoteza muda kuuliza mambo gani ya aibu aliyoyafanya.
Aulize ili atumbuliwe?
"Nisaidie ndugu yangu!" Kauli hii ikamtoka kwa uchungu huku akiikumbatia simu ile kwa mikono yote miwili sikioni mwake.
Alikuwa anazungumza na masihi wake.
"Hapa nakusaidiaje Didas? Enhe?
Yaani ungejua namna unavyoheshimika huku lkulu, sidhani kama ungefanya huu upuuzi wa kujirekodi ukifanya uchafu.
Huu ni upuuzi aisee! Akiona mheshimiwa Raisi itakuweje?
Kwenye mitambo hapa inaonesha bado nusu saa, video zote ishirini zitakuwa mitandaoni!
Na mtandao wa kwanza kufikiwa na huu upuuzi ni ule unaotumiwa na serikali."
Sauti ya mpigaji ikapandwa na jazba, bado kasi yake ni ya haraka na haina mahusiano na utani wa aina yoyote ile. Yalipotajwa maneno kama *Raisi* na *serikali* , ushuzi ulimponyoka Didas kwa mafungu.
"Bwana mkubwa! Bwana mkubwa! Naomba unisaidie kaka.
Ni wahuni tu wamenifanyia mchezo mchafu. Nimeangushiwa jumba bovu ndugu yangu!" Ni Didas kwenyw harakati za kuutafuta wokovu wake.
"Mimi sio ndugu yako! Na wala usiniite kaka.
Sina undugu na wazee wazinifu wasio na uaminifu kwa wake zao.
Wewe mzee hauna maadili kabisa!" Sauti ile inaonekana kama haitaki kupoteza muda, ni nzito, sauti ya mamlaka.
"Kesi za maudhui ya namna hii hutufikia siye kabla ya kuingia mitandaoni. Yapo yanayofutika na yapo maudhui kama haya tusiyoweza kuyafuta kutokana na umahiri na ujanja wa mdukuzi anayeyapakia kwenye system.
Na mimi siko tayari kuona huu uchafu unaingia kwenye rada za serikali yetu tukufu ya Jamhuri.
Kwanza ni bahati sana nimeipata namba yako na nikakupigia. Nimekuheshimu sana kwa vile mimi ni mpenzi wa bidhaa za kampuni yako.
Kimsingi sina cha kukusaidia,
Lakini kama kuna mtu unayedaiana naye kwa namna yoyote ile, mlipe kabla ya nusu saa...
Ama sivyo,
Mzee wangu...jiandae kisaikolojia!
Adui yako anaijua teknolojia vyema kuliko kitu chochote kile!"
Simu ikakatwa.
Upesi!
Didas hakuwa na muda wa kujiuliza mara mbili. Akaliwasha gari lake na kuugeuza usukani. Gari likachomoka kwa kasi kuelekea eneo lolote lile ambalo alifahamu kuwa kuna jengo linaloitwa benki.
Kiburi na majivuno yake yote akaamua avitie mfukoni kwa muda.
Shilingi yake ya ukombozi ilikuwa ikinesanesa kiganjani mwake karibu na tundu la choo, hakutaka kuipoteza!
Potelea mbali kama Bebe ni msaliti, mnafiki ama malaika mtoa roho. Akampigia simu mara moja kutaka kukutana naye ofisini mwake.
Alikuwa ni kama aliyepewa mzani achague ni kipi chenye uzito kati ya utajiri na heshima yake alivyovihangaikia tangu zamani akiwa kijana, ama msichana changudoa aliyekutana naye ukubwani na kuamua kumsaidia.
Wakati huu akaipa heshima yake uzito wa jiwe la fatuma mbele ya Bebe mwenye uzito wa unyoya.
********
"Saini hapa na hapa!" Didas anaitazama saa yake, upara wake unavuja jasho.
Anamtazama Bebe ambaye naye ni kama haelewi ni nini kinachoendelea.
"Nisaini nini tena mbona sielewi?" Bebe anauliza.
"Usinichanganye! We saini hapa... sina muda wa kupoteza. Mengine utayajua mbele ya safari." Didas anabwata, matone kadhaa ya mate yakimtoka kinywani.
Tai yake shingoni imegeuka nyuma. Ina maana kifua chake kimehamia mgongoni?Hatujui. Anajua yeye.
Bebe akakamata kalamu ile ya wino na kuanza kusoma karatasi ile kabla hajasaini.
"Come on! Unasoma nini tena?"
"Unataka nisaini kitu ambacho sikijui? Kama unataka kuniuza?" Bebe akauliza kwa kujiamini.
Didas akashusha pumzi kwa nguvu.
"Sikia Frola!" Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu akamtaja kwa jina lake halisi.
"Hapa tunaongelea uhai na kifo! Heshima yangu na familia yangu niliyo nayo ni maisha yangu Frola.
Huu ni mkataba wa kusitisha kazi yako wewe na kampuni yetu kama anavyohitaji huyo mwenzio...Ahhh (Anabadili) huyo jamaa aliyeturekodi.
Umenielewa?!" Uso wake umetota kwa jasho anamtazama Bebe.
"Ina maana naacha kazi?"
"Yeah! Haya saini hapa."
"Kwa nini lakini?"
"Bebe...hayo masuala mengine tutajua baadae. Tazama! Tuna dakika kumi na moja tu hapa."
Bebe akaiinamia karatasi ile na kuanza kuchonga herufi zake. Didas anamtazama kwa shauku, bado anaona Bebe kama anaandika taratibu.
Bebe akamaliza kutia saini yake. Didas akaikwapua bahasha kubwa ya kaki iliyosheni fedha kutoka kwenye begi dogo na kumkabidhi Bebe.
"Haya mama! Mpelekee huyu jamaa hivi vitu haraka kwenye eneo nililokuelekeza. Fanya upesi." Didas akamsurutisha Bebe.
"Lakini-"
"We nenda, hili likiisha hayo mengine tutayaongea!" Didas akamkatisha.
Bebe akaondoka kishingo upande kutoka ofisini mwa Didas na kutoka nje.
Huku nyuma akamuacha Didas aliyechanganyikiwa, anaitazama saa yake kila baada ya sekunde kadhaa.
Baada ya takribani dakika ishirini simu yake ikaita. Akakurupuka kuipokea baada ya kugundua kuwa mpigaji ni huyu huyu aliyepelekewa mahitaji yake.
Didas akapongezwa kwa juhudi zake alizozifanya kukamilisha kile alichoagizwa.
"Makubaliano yetu ni kutoziachia video mitandaoni. Kwa hio ziko salama kabisa! Hutozikuta kwenye mtandao wowote ule kiongozi wala usiwe na wasiwasi.
Na hakuna mtu awaye yote anayeweza kuzipata." Sauti ya kijana mchangamfu asiyejulikana ikamtoa hofu.
"Naweza nikaongeza kiasi zaidi ili zifutwe kabisa kama inawezekana? Samahani lakini."
Didas anauliza kwa saut ya nidhamu.
"Ninayo furaha kukuambia kuwa hilo haliwezekani mzee wangu!" Sauti changamfu akamjibu.
Anayo furaha? Kivipi?
"Kwa nini haiwezekani?" Didas akauliza.
"Siku yoyote ile utakapolitamka jina la Frola, ama kukutana naye, ama kumuhusisha kwenye mduara wa maisha yako, basi video hizi zitakuwa kama wa muhtasari wa taarifa za habari kwenye televisheni kubwa hapa nchini. Nina uhakika sishindwi kufanya hilo jambo!" Sauti changamfu akaweka kituo kisha akaendelea.
"Kiufupi kuanzia muda huu, nataka uachane na Frola moja kwa moja. Huyu nd'o anguko lako! Muone kama ukoma.
Kaa mbali naye kabisa. Hapo utakuwa salama." Akamaliza na simj ikakatwa.
Didas akachoka.
*******
"Kiufupi kuanzia muda huu, nataka uachane na Frola moja kwa moja. Huyu nd'o anguko lako! Muone kama ukoma.
Kaa mbali naye kabisa. Hapo utakuwa salama." Yalikuwa ni maneno ya mwisho kutoka kinywani mwa J4 akiwasiliana na mtu kwenye simu.
Kando yake ameketi Bebe akiburudika kwa kinywaji chepesi kulipasha tumbo lake kwa ajili ya maandalizi ya mlo mzito uliokuwa ukisubiri hukumu yake pale mezani.
J4 akakata simu ile na kumtazama Bebe aliyekuwa anatabasamu kwa madaha.
Cheko fupi likawavamia wote kisha wakahamia mezani pale na kuanza kula.
"Unawezaje kuyafanya haya yote?" Bebe akamuuliza huku akitafuna paja nono la kuku wa kukaanga.
"Ni njaa tu!" J4 akamjibu kwa kifupi.
"Njaa? Kivipi."
"Njaa amekuwa mwalimu wangu mzuri. Kama hujanielewa endelea kula, ukishiba utanielewa vizuri." J4 akatamka kwa mzaha akiwa na uso unaowaka tabasamu.
-------------------
Mambo yamekuwa mambo!
Bwana Didas Kilonzo Ambrozi anashambuliwa kutoka kila pande. Ile Utatoa sitoi, utatoa sitoi...Anajikuta anaachia tonge.
Anapewa vitisho vikali kutoka kwa mtu asiyemfahamu.
Je, huu ni mwisho wa Bebe kukutana na Didas?
Ana lengo gani na Bebe huyu J4? Halafu ni kama wana jambo lao hawa...kulikoni?
Kazi yetu sisi ni kushare link ya chaneli, kureact na kutoa maoni kwa mwandishi kupitia 0763205351.
Riwaya hii tamu Inaendelea...

👍
🔥
❤🔥
👏
🙏
7