MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
June 7, 2025 at 04:35 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA KUMI NA MBILI *Kwa kuwa bado tunaishi ndani ya hii dunia..* *Hakika ipo siku moja isiyo jina, utakutana na mtu ama atakuja mtu mpya maishani mwako.* *Huyu ataubadilisha mwelekeo wa maisha yako...atakupa elimu mpya na changamoto ambazo hukuwahi kamwe kukutana nazo.* *Omba sana, mtu huyu mpya asilipeleke motoni jahazi la maisha yako...* *Hii ni sehemu ya kumi na mbili!* Zilipotea takribani dakika thelathini na tano, mpaka walipoukamilisha mlo wao katika hoteli hio kubwa waliokutana. Wakaziteketeza dakika nyingine ishirini kwenye mazungumzo ya hapa na pale huku wakiyasindikiza maongezi haya kwa vinywaji laini. Matumbo na nafsi zao zilipotosheka, ukawadia muda maalumu ambao uliwaweka katika hoteli hii mpaka muda huu. Bebe akaangaza macho yake huku na kule kuhakikisha usalama ambao tayari ulikuwepo. Kisha taratibu bila papara akainama na kuibuka na begi dogo mfano wa briefcase kutoka chini ya meza hii. Sanduku lililoonekana kuwa na uzito baada ya kujazwa vitu fulani fulani, akalitua juu ya meza ile, na meza ikaitika kwa kutoa mlio *TIIII!!* Naam, lilikuwa na uzito usiokuwa wa kawaida. Ni uzito ambao unahitaji dakika moja tu ya maajabu kumbadilisha mtu anayeonekana kama mwehu, aanze kuitwa chifu. Uzito wa fedha! Akalisukuma katika namna ya kuteleza kuelekea kwa J4. J4 ambaye alikuwa na mshawasha wa kuziona hizo milioni mia zilizomo. Akajisogeza karibu zaidi, uso wake ukiwa na shauku. "Mzigo huu hapo, ufungue!" J4 akasita na kumtazama Bebe usoni kwa macho ambayo ni kama yanamuuliza, "Una uhakika kuwa humu ndani kuna milioni mia?" Bila kutamka neno lolote, akayerejesha tena macho yake juu ya sanduku lile. Huenda huu nd'o muda pekee ambao J4 alihitaji kuwa mtulivu. Milango yake yote mitano ya fahamu ikaanza kufanya kazi sawasawa. Akainyoosha mikono yake tayari kwa ajili ya kulifungua. Akili yake ilikuwa tayari imelifungua sanduku hili na kukisia juu ya wingi wa mabunda makubwa ya fedha uliomo ndani yake. Na sasa alikuwa akienda kuyahakiki yale aliyokuwa akiyadhahania akilini mwake mubashara kabisa. Milioni mia! Alaaa, hii ilikuwa fedha ambayo hakika asingewahi kuimiliki mpaka atakapozama futi sita ardhini. Mikono inamtetemeka, J4 akavibetua vyuma vilivyolikaza sanduku lile. Kisha kama anayefungua mlango hivi, akalifungua sanduku. Hamadi! Pua zake zikapokelewa na harufu ya kipekee. Harufu halisi ya fedha kutoka sandukuni. Mboni za macho yake zikapanuka, macho yake yakaona, Safu za mabunda ya noti mpya nyekundu zilizonyooka zilijipanga vyema kama zimepigwa pasi. Bado haamini, mkono wake hakukutaka kubaki nyuma. Akaamua kuzigusa. Mkono wake ukatambaa na kuteleza juu ya noti hizi. Vidole vikakana kuwa havijawahi katu kuzigusa milioni mia moja. Akafanya kama anayechimba, akaibuka na bunda moja la noti zilizoviringwa ndani ya mpira mdogo. Akalitikisatikisa kama anayepima uzito wake. Akazichezesha noti kwenye ncha za vidole vyake kama anayezihesabu hivi. Ni noti mpya kabisa ambazo hazijapita kwenye mikono ya watu wengi. Uso wake ukawa wa mwisho kudhibitisha kuwa amefurahishwa sana na kile alichokikamilisha. Tabasamu likawaka usoni mwake, akamtazama Bebe usoni. Akaufungua mpira ule uliozidhibiti noti za bunda lile, zikawa huru. Akazitupa juu ya meza kumwelekea Bebe. Noti zikateleza mezani katika mfumo wa kusambaa. "Unajua tunaziitaje hizo?" J4 akauliza akiwa wima. "Zinaitwa hela!" Bene akamjibu kwa bashasha. "Lipe neno uzito...sema fedha! Kama wasemavyo wao." J4 akarejea kwenye kiti. Akauinua mguu wake wa kulia na kuubebanisha juu ya paja la ule wa kushoto, akakaa kwa kuchonga namba nne. "Ni burudani sana kutazamana na utajiri uso kwa uso. Na leo nimepata bahati ya kuipata burudani hii bure kabisa. Kwa nini nisiburudike?" J4 akatamka huku akilifunga upya briefcase lile. Bebe akacheka kidogo huku akiuziba mdomo wake kwa aibu. "Haya nd'o maisha tunayotakiwa kuyaishi Bebe!" J4 amemaliza kulifunga sanduku lile na sasa anafanya jitihada ya kuzikusanya fedha zile alizozitawanya mezani pale kwa mbwembwe. "Hii ndio namna tutakavyo-yanyanyasa maisha. Mpaka yapige magoti yakisota na kuomboleza chini ya nyayo zetu. Hivi hivi...mimi na wewe!" Sauti yake imejaa unabii, J4 anatamka akiwa ametazamana na Bebe uso kwa uso. Wote wakatabasamu wakitazamana. Tabasamu lao lilinena lugha moja. Lugha ambayo waliielewa wao tu. Sio lugha ya mapenzi asilani. Ilikuwa lugha ya ajabu ambayo Bebe aliitafuta kwa muda mrefu sana bila mafanikio. Lugha ya ukombozi! Ni lugha hii hii iliomfanya akutane na J4 na kumkabidhi uaminifu wake wote. Hakuwahi kumuamini mwanaume yeyote yule lakini kwa J4 ilikuwa tofauti. "Tutakuwa huru...tutakuwa matajiri! Ni haya haya maisha yaliyotufikisha hapa tulipo. Mimi na wewe tunajua ni nini tunakihitaji." Ni maneno ya J4 yaliyogeuka kuwa asali masikioni mwa Bebe. Maneno ambayo baadae yalimfikisha Bebe kwenye anga ambazo hakuwahi kutarajia kufika. Anga zinazoifanya simulizi hii iwe hii. ******* Ilikuwaje mpaka wawili hawa wakakutana? Ni swali ambalo hakika linakufanya unishutumu mimi ninayekusimulia. Ilikuwa hivi... Jumanne Maliki, ama J4 kama mlivomzoea ndiye alikuwa mchoraji wa hii ramani yote. Mpango wake aliusuka kwa ustadi na hakutaka kupoteza muda kabisa. Hapo awali, Akiwa katika harakati za ujana maji ya baridi na swahibu yake Dotto, alipagawa alipoitia sura ya Bebe kwa mara ya kwanza kwenye mboni za macho yake. "Hii pisi kwelikweli aisee, imenyooka sana hii!" Dotto aliinadi picha ile kwenyw simu yake. "Anaishi wapi huyu? Mbona sijawahi kumuona hapa mtaani." J4 akahoji. "Aaa wewe...unadhani hiki kiwango ni cha kucheza kwenye viwanja vya chandimu? Hiki ni kiwango cha kimataifa kaka. Class A kabisa! Wa watu wazito hawa!" D akaanza mbwembwe zake zilezile za udalali. J4 akampokonya simu yake na kuitazama picha ile kwa umakini zaidi. Akakitikisa kichwa chake kukubaliana na alichokiona. "Mali iko Sinza hii mzee baba. Inapiga ukaunta pale GRANDE!" Dotto akaendelea kuipamba picha yake. "Ni baamedi eh?" "Itakuwa...lakini ninasikia, japo sina uhakika...kuwa ni dada poa!" D akanong'ona. Hili la mrembo huyu kuitwa dada poa, likazitia doa kubwa jeusi sifa zote nyeupe zilizokuwa zikipepea kwenye akili ya J4. "Kwamba anajiuza au?" "Nasikia hivyo...maana yule bimdashi mmiliki wa klabu, nasikia nd'o mishe zake hizi pande zile." "Duh anaitwa nani aisee?!" "Nani? Huyo bimkubwa au-" "Huyu demu" "Be-Bebe! Anaitwa Bebe!" Anaitwa Bebe! Nd'o ikawa sentensi ya kwanza kukisumbua kichwa chake. Akamhimiza rafiki yake himahima ampeleke pale kwenye klabu ambayo mrembo huyu anafanya kazi. Siku ya kwanza, wakafukuzwa na walinzi baada ya mavazi yao kuwatambulisha kama vijana mabarobaro waliokuja kutalii na kuondoka tu. Hawakujipanga, bali walikurupuka tu. LE CLUB GRANDE sio mahala pa wanaoulizia bei. Wakajipanga vyema siku ya pili, lakini haikuwa bahati yao. Hawakumkuta! Baada ya J4 kubembeleza sanaa, Wakajaribu tena siku nyingine. Safari hii wakaenda usiku. Na kweli, akamuona Bebe kwa mara ya kwanza. Moyo wake ukamuuma sana! Ni heri asingemuona kabisa labda angeweza kujiepusha na yote. Kwamba hii sanaa bora ya uumbaji inayopumua ni kahaba? Alikataa kuamini. Moyo wake ukataka kufanya kosa la kumfumba macho na kumtupa kwenye shimo la huba. Lakini akili yake ikawahi upesi na kuikamata miguu yake, ikamrudisha kwenye njia sahihi. Kwamba azame penzini na kahaba? Akili yake ikamshutumu na kumfanya ajidharau. Lakini moyo uliougua gonjwa la mapenzi unatibika kwa namna ya kipekee sana. Na tiba yake ya kweli ni muda! Naam, kama ambavyo alimpenda taratibu. Ni hivyo hivyo alijifunza kumsahau taratibu. Na katika darasa hilo la kujifunza kumsahau, akadurusu somo ambalo alitaka limpe sababu zenye mashiko, ni kwa nini asimpende kahaba. Hapa akaiacha nadharia, akajifunza kwa vitendo. Akaanza kumfuatilia Bebe nyendo zake zote alizotegemea ziwe chafu machoni mwake. Yeye alikuwa na lengo moja tu. Kujifunza kumsahau. Hilo tu. Lakini macho yake kijana huyu mhitimu wa uhandisi wa umeme na masomo ya kompyuta, yakaiona fursa! Fursa ambayo labda aliwahi kuiona na kuipuuza. Lakini sasa anapata kila sababu ya ni kwa nini anahitaji sana fursa hii. Akazidi kuzama darasani! Aliyaona macho ya wanaume wenye tamaa, yanavyolitazama umbo la Bebe na kummezea mate. Aliyaona macho yao yanavyoweweseka baada ya kutazamana na ile sura yake jamali. Tazama wanaume hawa wanavyomwaga fulusi za kutosha ili tu wampate Bebe kwa ajili ya kuiridhisha miili yao. Tazama namna wanavyoteketeza fedha ambazo labda zingetosha kabisa kubadilisha maisha ya J4 na wazazi wake kule Ushirombo. Wanaume hawa ndimi zao zinaning'inia nje wakitokwa na mate kwa uchu wa ngono. Macho yao yanawaka tamaa wakimtazama Bebe. Tazama! J4 akafumba macho yake na kuzikumbuka nyakati na maisha yote magumu, yaliyogubikwa na umasikini aliyoyapitia tangu akiwa chuoni hasa baada ya kukosa mkopo wa serikali. Akalazimika kukitumia kipaji chake akidukua vyanzo mbalimbali vya mitandao na kuuza intaneti kwa wanafunzi wenzake ambao nao walimlipa kwa rasharasha. Mara kadhaa akakoswakoswa kudakwa na vyombo vya usalama kama mhaini na tapeli wa mitandao. Yote haya aliyafanya ili tu apate fedha ya kujikimu. Leo hii yupo mtaani, anatumia kipaji chake kama silaha ya kuiwinda fedha. Lakini hapa anaona fedha ile inamwagwa na matajiri kwenye uasherati. Ajabu! Vita yake ya kuitafuta fedha ikamdai silaha ya ziada. Hapa akamtazama Bebe kama silaha yake mpya ya maangamizi. Alikuwa amemfatilia kwa muda mrefu. Mpaka Bebe anapata umaarufu, J4 alikuwa kimya nyuma ya skrini za kompyuta akiandaa mitego yake ambayo aliiamini sana. Na alihitaji nyakati moja pekee ya kuitega mitego hii. Ndipo ikafika hii siku ambayo aliwafuata Bebe na Didas hotelini kwa usiri. Akalazimisha kumpiga Bebe kikumbo mpaka vitu vyake vilivyokuwa ndani ya mkoba legevu vikaanguka chini. Katika kumsaidia kuviokota, mikono yake ikafanya kazi kwa kasi ya ajabu na kubandika vinasa sauti na kamera ndogo ndogo kwenye baadhi ya vitu vyake. Akiwa na uhakika kuwa ni lazima tu atanasa. Na kweli akanasa! Ilikuwa bahati mbaya sana kwa bwana Didas Kilonzo Ambrozi. Ndani ya muda mchache, tayari J4 alikuwa na vipande vya video kadhaa ambavyo aliviunganisha. Usiku wa siku ile akakutana na Bebe baada ya kumpigia na kumueleza kuwa upo ujumbe wa siri anaotaka kuzungumza na yeye peke yake. Akamuondoa hofu kuwa kwa usalama zaidi, Bebe yeye mwenyewe apange mahala ambapo angependa wakutane. Bebe alipojaribu kuleta maringo, akashtuliwa kwa kipande cha video ile kilichotumwa katika simu yake. Hapo akakurupuka na kukutana na J4. Saa nne usiku, LE CLUB GRANDE! Ni hapa ambapo Bebe alipaona kuwa mahala salama zaidi kutokana na kujulikana kwake mahala pale. Hapo akakutana na J4 kwa mara ya kwanza, wakazungumza. "Wewe ni nani? Hiyo video umeitoa wapi?" Bebe aliuliza akiwa mwingi wa hofu. Licha ya uzoefu wake wa kuwahudumia wanaume kingono, hakuwahi katu kujirekodi au kuruhusu hilo litokee akiwa kazini. "Jina langu utalifahamu mara tu baada ya mimi kukamilisha kile nilichokusudia kukifanya ili wote tufaidike. Namaanisha, nikusaidie wewe na wewe unisaidie mimi." J4 akiwa ndani ya kofia pana na mavazi yaliyojaribu kumfanya aonekane kama jasusi wa kimataifa, akatamka kwa kujiamini. "Unisaidie? Nikusaidie?...wewe unanisaidiaje mimi? Unaweza kunisaidia kwa lipi?" Bebe akaruhusu kiburi kimfanye ajihisi yeye ni jitu la miraba minne na huyu anayeongea naye ni mbilikimo tu. J4 akatabasamu kidogo kisha akaketi vyema. "Sikia Frola!" Kutajwa kwa jina hili kukamfanya Bebe aubadili mkao wake na kukaa chonjo. "Mimi nafahamu fika wewe ni mwanamke wa aina gani. Nafahamu fika kuwa unapenda kuwa huru, ulitoka hapa GRANDE ili uwe huru. Hata huko ulikoenda, unautafuta uhuru! Lakini bado maisha yako, yako ndani ya minyororo ya utumwa. Haujapata kile unachokitafuta." Akatulia na kuyapa nafasi maneno yale yazame kwa Bebe. "Uhuru? Unadhani mi ni mtumwa?" Jazba inaanza kumpanda Bebe. "Hii video hii...inaweza kukupa fedha mara ishirini ya huo mshahara wako wa milioni mbili na nusu unaopata kwa ajili ya tangazo moja unaloigiza! Huwezi kuamini." J4 akatema cheche huku akitikisatikisa simu yake ya kupangusa, iliopasuka kioo chake na kuacha nyufa kadhaa zikitambaa. Bebe akapagawa. Huyu jamaa anajua mpaka mshahara wake! "We..ume..umejuaje mshahara wangu?" Akababaika. "Nataka nifanye kazi na wewe Frola! Kazi yetu tukiwa huru, mimi na wewe. Nakuhaidi tutapata hela nyingi sana! Tutakuwa matajiri." Utajiri? Utajiri gani hasa ambao Bebe alikuwa akihuitaji kutoka kwa huyu kijana mpya machoni mwake? Tayari anao umaarufu mkubwa nchini japokuwa huu haukumfanya awe tajiri moja kwa moja. Hata kama angepata ofa yenye malipo makubwa, bado isingeweza kuzidishwa mara ishirini ya mshahara wake. Akaketi vizuri na kuiegemea meza yake, akajisogeza karibu, tayari kumsikiliza J4. J4 akaachiwa umiliki wa dimba la maongezi. Akauweka mezani mchoro wake mzima wa namna atakavyoikamilisha mipango yake yeye na Bebe. Maneno yake yakawa sumu kali ambayo iliulegeza moyo wa Bebe, supastaa. Bebe akalainika na kukubaliana moja kwa moja na mpango ule wa J4. Mpango ambao ulimhakikishia kuwa siku inayofuata, atakuwa na zaidi ya milioni hamsini kibindoni. Ulikuwa mchezo rahisi sana kwake...ugumu wote uliachwa kwa J4. Ni ndani ya siku mbili tu. Muda huu wanatazamana na kisanduku kilichosheheni fedha. Milioni mia! "Huu ni mwanzo tu! Bado kuna mtu fulani huko ametutunzia hela zetu. Inatakiwa anase kwenye mtego wetu upesi." J4 anayasema haya baada ya mgawo kufanyika kama walivyokubaliana. Na sasa kila mmoja amekifutika kiasi chake anapopafahamu. Wako ndani ya gari la Bebe alilopewa na kampuni ya Bwana Didas. Muda mchache tu ujao, anafahamu kuwa ataachana nalo. "Kituo kinachofuata?" Bebe akamuuliza mikono yake ikiwa kwenye usukani. "Hakuna oda yoyote ile ya mtu binafsi ambayo umeipokea?" J4 akamuuliza. "Ooh yupo, Yule msanii Kenzy. Aliniomba niwe naye kwenye rekodi ya moja kati ya nyimbo zake za hivi karibuni." Bebe akachangamka. "Basi nadhani unajua ni nini unatakiwa kufanya." J4 akanong'ona kisha akatoa cheko la kibabe. Cheko la fedha! Akafungua mlango wa gari hili na kuanza kutoka nje. "Wapi sasa, si ninakupeleka mpaka kwako au?" "Hapana, ukifika wakati wa wewe kupajua kwangu. Nitakuleta mwenyewe. Mahusiano yetu hapa ni ya kibiashara tu na si vinginevyo..." J4 akatamka kwa kujiamini tayari yuko nje ya gari. "Mawasiliano yako ni yalayale ama?" Bebe akapaza sauti. "Hapana hayo yameshapotea, hayapo tena hewani....nitakutafuta kwa namba mpya." J4 akamjibu akitokomea. Hakumng'ang'ania Bebe kwa lolote na wala hakuonesha kumjali. Hili ndilo lililomuacha Bebe njia panda. "Ni mwanaume wa aina gani huyu?" Akajiuliza. Amekutana naye jana usiku tu...lakini tayari amemzoea kama ndugu mapacha wa tumbo moja. Na hajaweza kubabaishwa na urembo wake. Bebe akaliondoa gari lake eneo lile huku akilitafakari ombi la kijana huyu mwenye uelekeo wa hirimu moja na yeye. *Alitaka wawe na mahusiano ya kibiashara!* hivyo tu. Akazikagua noti zile mpya ndani ya mkoba wake, akazikuta bado zinapumua. Akatabasamu. Ama hakika, alikuwa kwenye biashara. ------------------------ Milioni mia kutoka kwenye vibubu vya bwana Didas, imepasuliwa na kutulizwa kwenye mifuko ya Jeifoo na Bebe. Pacha ambayo imetuhaidi kuhusiana kibiashara katika namna ya kushangaza. Wamemtaja Kenzy, msanii wa kizazi kipya ambaye ni maarufu pia nchini. Ni bomu gani limeandaliwa na pacha hii matata? Share link ya chaneli, acha reaction na toa maoni yako kwenye 0763204351. Mtunzi anapokea yote! Riwaya hii inaendelea...
Image from MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶: RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU Y...
❤️ 👍 ❤‍🔥 🔥 13

Comments