MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶
June 11, 2025 at 10:08 AM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel* WhatsApp; 0763204351 ----------------- SEHEMU YA KUMI NA TATU *Katu usijidharau na wala usiwadharau wengine.* *Huenda wewe ni daraja la mafanikio ya mtu mwingine, yupo mahala fulani na mtakutana katika namna ya kushangaza.* *Ama neema ya mafanikio yako imebebwa na mtu fulani aliye mbali ama huyuhuyu aliye karibu yako.* *Ulimwengu wetu umeumbwa kwa kanuni ya ajabu sana...* *Tunaishi kwa kutegemeana.* *Karibu kwenye sehemu ya kumi na tatu.* Kila kitu kilikuwa kama mchezo wa sinema. Ndani ya siku moja tu...kila mtu alikuwa amebadilisha historia ya maisha yake. Sio Bebe, sio J4 na pia sahau kuhusu Chief Didas, kama alivyozoea kuitwa na Bebe. Kila mtu kwa nafasi yake, aliyapokea mabadiliko japokuwa katika namna tofauti. Haswaa, Bwana Didas, alilazimishwa kulivujisha pakacha lake. Bebe na J4, wakafurahia nafuu hii ya kuwa wachukuzi. Bwana Didas alikuwa bado haamini kama ameokoka kwenye hatari kama hii. Hatari ya jina lake kupakwa matope mbele ya Watanzania wanaomheshimu. Na zaidi ya yote, wanazipenda bidhaa za kampuni yake. Akashusha pumzi ndefu kujiweka sawa. Ni kama punguani aliyeiokoa kete yake ya mwisho kwenye mchezo wa kamari ambao alikuwa na kila dalili ya kupoteza. Hofu ya kuaibika bado ilizidi kuutafuna ujasiri wake. "Hivi huyu jamaa hajapost kweli?!" Ni swali pekee alilozidi kujiuliza akiwa anaendesha gari lake kuelekea nyumbani. Ameshapiga simu mara kadhaa kwa mkewe, akimuuliza endapo kuna taarifa yoyote ile mpya iliyogonga hodi. "Mh Baba Junior, umekuwaje mme wangu? Hii ni mara ya nne. Mara ya nne unaniuliza kama kuna jipya. Vipi, kwema huko? Ama kuna msiba?" Sauti bembelezi ya kujali, lakini yenye kujiamini ikahitaji majibu. "Aaam...hapana laazizi. Nakujulia tu hali mke wangu. Hehehe wala hamna shida." Didas anamjibu huku akijichekesha kwa aibu. Siku hii anamuita mkewe kwa jina *Laazizi* , haikuzoeleka hivi. Hatulii anabadili upepo angani, atapiga simu kwa baadhi ya vigogo na viongozi wakubwa wa serikali anaofahamiana nao. Hawa atawauliza juu ya kile kinachoendelea Ikulu. Didas atasimamisha gari lake kando kidogo. Anapoongea na watu wenye nyadhifa kama hizi, kelele hazihitajiki. Badala yake ataiinamia simu yake na kulitega sikio lake kwa adabu zote, kusikia litakalosemwa. Hataambulia kitu zaidi ya malalamiko ya viongozi hawa juu ya kero za wananchi na ugumu wa majukumu yao. Ni saa tatu na robo usiku, Didas Kilonzo Ambrozi anarudi nyumbani baada ya siku ndefu sana. Ama siku hii gari la *faza hausi* limerudi nyumbani mapema kuliko siku za nyuma. Tazama, hii ni siku ya tofauti kabisa kwa familia hii tangu asubuhi. Labda ni siku nzuri kwa mama Junior na wanae, lakini kwa Didas ni ya kipekee. Anakuja kupokelewa na bintiye mdogo wa kike katika namna ya *Baba huyo*...anaigiza tabasamu, nalo linamgomea kuigizwa. Anamkwapua na kumuinua juu kiasi lakini hambebi, anamrejesha upya sakafuni baada ya kugundua kuwa amechafuka! Suti yake nyeusi nadhifu aliyoandaliwa na mkewe asubuhi ya siku hii, imepakwa rangi mpya ya vumbi. Tai yenye nembo ya bendera ya taifa, haipo tena shingoni mwake. Ukosi wa shati lake nao ni kama umepata muundo mpya shingoni mwake. Didas anaiburuza miguu yake na kuingia nyumbani mwake akiwa amechoka mwili na akili. Hataki usumbufu wala mazozano na mkewe, ambaye anamshushia mvua ya maswali juu ya muonekano wake. Huyooo Didas anajisogeza bafuni ili akakoge. Lakini hapigi hatua zaidi ya tano kabla hajahisi kuongezeka kwa gramu kadhaa za uzito wa kichwa ni chake. Anayumba na kuisalimia ardhi kwa kuanguka chini kama mzigo. Hii nayo ina maswali ya kumuuliza. Hana majibu...anakoroma tu, anaona giza! Giza linamfumba macho yake. Kinachofuata ni hekaheka za mama Junior na wanae kumpepea kabla hawajaomba msaada wa wafanyakazi wa nyumba ile. ******* "Mic check, mic check...one two, one two!" Sauti nzito changamfu iliendelea kurindima ndani ya Studio kubwa. Ilikuwa sauti ya bwana mmoja mnene wa umbo, aliyeyafunika masikio yake yote mawili kwa kifaa cha kidigitali, maalumu kwa ajili ya kusikiliza muziki, headphones! Fulana yake pana ya kijivu, imelowa jasho na kuchora mfano wa ramani kwenye kifua na mgongo wake. Mbele yake ni meza iliyochafuka kwa vifaa lukuki vya kieletroniki. Vifaa vinavyomweka kwa rangi mchanganyiko. Rangi zinazompa mzuka wa kufanya hiki anachokifanya. Atagusa hapa na pale, atabonyeza kitufe hiki na kile, huku atasugua sugua kisha kile atakizungusha. Ili mradi tu, aukoroge mchanganyiko wa sauti na azalishe mziki bora. Hii nd'o kazi yake.Yeye ni producer (mzalishaji) wa muziki. Pia ni mkufunzi wa wasanii wa muziki wa kizazi kipya. Na siku hii alikuwa akimpika kijana mpya pale pale kwenye studio yake. Kichwa chake kinapanda juu na chini, kikifuatisha miondoko ya mdundo wa muziki anaousikia yeye peke yake. Kisha anatoa ishara ya kidole gumba kwa kijana nyuma ya kinasa sauti, aliye ndani ya chumba maalumu kilichomtenganisha naye kwa kioo kipana kinachoruhusu waonane. Kijana yule anaiweka sawa sauti yake, anayafumba macho yake kiasi kwa hisia kali na kuanza kuimba yale anayoyasoma kwenye karatasi mbele yake, japo kwa kuibiaibia. Hamalizi hata mshororo mmoja wa beti lake, "Hajwaa! Hajwaaa!" Sauti inapazwa, haisikiki. "Dogo achaa! Acha nakwambia! Hii mbovu, mbovu sana!" Bwana yule mnene amechachamaa, anasimama kwa hasira na kufoka. Kitambi chake kinatikisika, ndita zimeweka kambi usoni mwake. "Nimeshakwambia, usiimbie kooni my boy! Sauti itoke kwenye tumbo! Tumboni nimesema! Haya shime..." Anarejea kwenye kiti chake, uso wake mnene bado una ramani za ndita. Ni kama aliyekunywa dawa chungu. Kijana ndani ya chumba, anajiweka sawa kwa mara nyingine. Naye, anavaa kifaa kilekile masikioni. Safari hii anajitahidi kuimba kama alivyoelekezwa. Anaibia mashairi kwenye karatasi mbele yake, kisha anapepesa macho kumsanifu bwana yule mnene, ambaye bado amemkazia macho kwa hasira. Mara ghafla, bwana yule mnene anakitoa kifaa kile masikioni. Anasimama kwa pupa, akimtazama kijana yule. Pumzi zinapishana kwa kasi puani mwake, ni kama mbogo mwenye hasira. "Dogo! Hivi nikueleze mara ngapi? Umekuja kuimba au kunipotezea muda?Mh? Sema!" Akiwa kwenye mahojiano haya na kijana huyu ambaye anaonekana kuipoteza hali yake ya kujiamini. Mara unafunguliwa mlango wa studio hii na kinaingia kikundi cha wanaume watano, kikiongozwa na kijana mmoja aliyevalia mavazi ya kisasa. Nyuma yake ni wenzie wawili wanaoonekana kufanana naye kimavazi, pamoja na watu wawili wa miraba minne, waliovimba kwa mazoezi. Ujio huu unabadilisha hali ya hewa ndani ya studio hii na kusababisha uchangamfu wa ghafla. "Alaaaa! Kenzy kama Kenzy! Finally, you are here my boy!" Bwana mnene anakurupuka na kumkumbatia kijana huyu. "Eeeeh BIG kama BIG!" Kijana yule akamchangamkia. Wanakumbatiana kwa furaha huku kicheko cha ushindi kikikatiza baina yao. "Aiseee...kitambo sana ticha!" Kenzy akatamka kwa bashasha. "Haswaa naona umenitupa mwanangu...mara ya mwisho, lini ilikuwa?...show yako ya pale Mbeya! Tangu hapo!" Bwana mnene, aliyetambulishwa kwa jina la BIG akatamka huku anakielekea kiti chake. "Nimeimiss sana hii studio ticha!" Kenzy anagundua kuwa kuna kijana ndani ya chumba cha mazoezi. "Nani huyu? Chipukizi eeh?" "Yeah...niko namchonga kijana. Sema huyu boga sana aisee...doh!" BIG akatamka huku akilipangusa jasho lake kwa kitambaa kipana. Kenzy akamfanyia ishara kijana yule asogee pale walipokuwa wao. Kijana anasogea akiwa anatetemeka. Haamini kama ni yeye leo hii anaonana na mwanamuziki mashuhuri nchini uso kwa uso. Msanii nyota, ambaye anatamani siku moja aje kuwa kama yeye. "Mambo vipi?!" Kenzy akamuuliza kwa uchangamfu. "Sa..sa-lama bro! Ke- Kenzy. Shkamoo!" Anajiumauma. "N'do nakwambia boy! Mimi nimewaandaa wasanii wakubwa! Huyu hapa Kenzy, nimemchonga mimi. Alikuwa anafuata maelekezo. Anatoa sauti! Kutoka tumboni...haibanii. Wewe sasa!" BIG akatamka kwa kisirani huku akisonya. Wale wapambe waliokuja na Kenzy wakacheka kwa sauti baada ya kuyasikia maneno ya BIG. Kijana akatazama chini kwa aibu. "Unaitwa nani mdogo wangu?" Kenzy amemshika begani kijana huyu, katika namna ya kumfariji. "Jackson" "Hili ni jina lako la kisanii?" "J-la...J-love nd'o jina langu la kisanii" "Safi sana...haya sasa nenda katuoneshe ulichonacho. Jiamini!" Kenzy anampiga begani, kijana anarejea ndani ya chumba. Anavaa kifaa kile masikioni, anashusha pumzi kwa nguvu. BIG anamtazama kwa pembe za macho yake katika namna ya *ole wako na hii uharibu*. Unawashwa muziki na kijana anaanza kutembea na mapigo yake akiimba. Ama! Ni kama mashetani yake yalikuwa yanasubiri ujio wa Kenzy, ndipo yampande kichwani. Sauti yake ikapita kwa adabu kwenye vifaa hivi vya kielektroniki. Ikawa sasa, ni kama mapigo ya muziki ule yanamtii yeye na kuifuata sauti yake badala ya yeye kuyafuata mapigo. Jackson, J-love akamaliza ubeti wake wa mwisho kwa kufumbua macho yake. Akakuta watu wote ndani ya studio hii, vinywa wazi. Makofi! Wote wakampigia makofi! Wote isipokuwa BIG. "Hebuu kwanza!" Bado haamini kama kweli Jackson ameimba namna ile. "Nipe stanza ya mwisho..." Akamsihi huku akicheza na vifaa vyake. J-love akaiimba beti ile kwa ubora zaidi ya mara ya kwanza. Aliyepiga makofi safari hii alikuwa ni BIG peke yake. "Unaishi wapi aisee!" Kenzy akamuuliza akiwa na shauku. "Msasani bro." Akajibu kwa adabu. "Unaimba vizuri sana mdogo wangu. Ukiendelea hivi, nitatoa ngoma moja na wewe siku si nyingi!" Kauli hii ikafufua tabasamu usoni mwa Jackson. "Sauti yako ina kitu mdogo wangu...ina raw energy ambayo wasanii wengi wanaikosa. Usiache, push harder! Na ukiweza kupata mentor kama BIG hapa, usimuachie." Kenzy akaongeza. Wakabadilishana nambari za mawasiliano na kupiga picha ya pamoja. Hili likawa kama kombe la ushindi kwa Jackson. Achana na kupiga picha na staa, hilo si suala. Suala kubwa ni kumiliki namba zake za mawasiliano. "Karibuni aisee wanangu! Sie tupo." BIG akarejea kuutambua ugeni wa Kenzy na wenzie. Ni yeye aliyemtengeneza Kenzy tangu alipokuwa chipukizi mpaka hivi sasa alivyo. Nyota wa muziki wa kizazi kipya. "Naam faza! Nilikuwa nakatiza, nikaona si vyema nipite kwenye mtaa ulionilea halafu nisipite hapa mgodini pasi na kutoa hata salamu!" "Oooh safi sana...walau hata umelikumbuka hilo. Nyie mkitoka huwa mnatusahau. Tumeshawazoea, na wala sishangai!" Producer BIG anajibu kwa kujiamini bado kitambaa chake kipana cha jasho kipo mkononi mwake, kinafanya kazi yake kwa uaminifu. "Walaa mimi siwezi kukusahau anko wangu, BIG mzazi! Tena..." Kenzy anasita kisha mkono wake unazama mfukoni na kuibuka na noti nyekundu kadhaa. "Nadhani hii ya maji itakufaa!" Anampatia BIG kiasi kile. BIG haonekani kushtuka. Anaipokea na kuisweka kwenye mfuko wa suruali lake bila hata kuihesabu. "Mafao yetu ya uzeeni haya!" Anatoa kijembe. Wote wanacheka kidogo. Anamkazia macho Jackson kisha na yeye anazama mfukoni na kumpatia noti ya rangi tofauti na zile alizopewa. "Haya dogo! Changanya mbaliga zako, kaniletee maji makubwa. Chenji inayobaki chukua!" Jackson anaipokea noti ile na kuondoka ndani mule kwa bashasha. "Enhe vipi umefikia wapi na ile project yako mpya? " BIG anamuuliza Kenzy. "Ipi hiyo?" "Video ya lile jiwe lako, ME AND YOU!" Anaweka wazi swali lake. Kenzy anachangamka, "Aaaah ME AND YOU....naelekea kushoot wiki ijayo mzazi. Kila kitu kipo tayari so far! Na pia kuna surprise hapo!" Kenzy anatulia na kuiacha sentensi yake ielee hewani ili auvute usikivu wa BIG. "Surprise gani tena?" "Unajua ni video vixen gani nitakuwa naye?" Akauliza tena kwa bashasha. Lengo lake ni lilelile, amshangaze BIG. "Ni nani?" "Queen Frola!" Akatamka kwa kushtukiza, akitabasamu kwa shauku. Na kweli BIG akashangaa. "Unamaanisha? Huyu huyu mrembo ninayemuona kila siku kwenye matangazo au?" "Eeh huyu huyo. Na mimi nitakuwa msanii wa kwanza kufanya naye kazi hapa nchini!" "Duh hongera bwana. Lakini mbona ni kama ni wa bei ghali sana yule. Utamudu kum-" "Nitamlipa. Pesa sio tatizo. Uzuri ni kwamba nikifanya naye video moja. Itakimbiza sana mitandaoni, faida itakuja kwa kasi!" Kenzy akajipeperusha. "Mh sawa! Utakuwa umepiga hatua kubwa sana aisee. Maana industry haicheki na mtu sasa hivi." BIG akatamka bila kumuangalia Kenzy usoni. "Tena jioni hii nina appoitment naye, tutakutana tuongee." Kenzy akaweka nukta. Baada ya dakika kadhaa za maongezi mafupi hususani ya kisanaa, Kenzy na jopo lake waliondoka na kuacha ahadi nyingine lukuki za kurejea tena. Ahadi ambazo masikioni mwa BIG zilikuwa sawa na baba anayemuhaidi peremende mwanae mdogo ma asimletee. Alishawazoea hawa wasanii! Anawachonga mpaka wanafanikiwa na kupenya kwenye tasnia, wakishapata mafanikio wanamsahau. Ama kweli, Tenda wema nenda zako! Anakunywa mafunda makubwa ya maji na kurejea upya katika darasa lake na kijana Jackson J-love. "Sikiliza, mgema aliwahi kusifiwa sana kuwa anatengeneza pombe aina ya Tembo kwa ustadi wa hali ya juu pengine kupita wagema wote. Unajua ni nini alifanya baadae?" Akamtupia swali Jackson. "Alilitia maji!" Akajibu upesi kwa kujiamini. "Unajibu kwa kuwa umekaririshwa hivyo au unaelewa?" "Naelewa!" Jackson akamjibu. "Haya vaa Headphones tuendelee. Kanuni ni ileile, toa sauti tumboni...imba kwa kujiachia. Usibane sauti! Haya sasa...One! two! three!....twende!" ******* Kipande cha kitu mfano wa kalamu ya rangi kinapitishwa kwa adabu kwenye papi za midomo yake. Anaifumba na kuigusanisha katika namna ya kuikausha rangi ile. Lipstick! Hii ni baada ya uso wake kurembwa kwa vipodozi na kuufanya ung'ae na kumeremeta. Sijaongelea kope zake ndefu ambazo sio za bandia. Ni kope ambazo zikipepesa tu, zinatamfanya mtu anayetazamana naye aimbe pambio kumsifu Mungu. Alikuwa na silaha zote za maangamizi. Kama hatakuua kwa sura yake iliyovimbiwa urembo, basi umbo lake na ngozi yenye nuru havitakuacha salama. Basi tuseme wewe ni mgumu sana. Utapona kwenye haya, lakini chunga sana masikio yako. Labda yafunike kwa pamba usiisikie sauti yake inayoweza kuwatorosha malaika mbinguni. Basi tuseme wewe ni kiziwi japo kwa mkopo. Chunga sana, usimsogelee karibu. Huyu hapa! Anajipulizia manukato yake ya bei mbaya. Manukato yenye harufu tamu, inayodai kumbato zito la mtu atakayepishana naye karibu. Eeh unashangaa?! Inabidi uwe na mkusanyiko wa vilema vitatu mpaka vinne vinavyohusisha milango ya fahamu. Uwe kipofu, macho yako simuone Uwe kiziwi, masikio yako yasimsikie Uwe toinyo, harufu yake ikupite kando. Na katu, ngozi yako isimguse kumhisi...utapagawishwa na wororo wa ile ya kwake. Ulimi hauna mfupa! Hii dhambi sitaki kushiriki. Hamna namna yoyote ile utakayokwepa kukiri kuwa Bebe ni malikia wa uzuri. Hasa jioni hii anayojiandaa kwenda kukutana na Kenzy. Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania. Bongo Fleva! Anasimama mbele ya kioo chake kipana. Anajitazama. Anajigeuza huku na huku, anajibinua kidogo. Kisha anazunguka nyuzi mia tatu sitini kwa madaha. Anafurahi namna nywele zake zinavyoufuatisha mzunguko ule. Ni huu urembo wake uliomtajirisha siku mbili zilizopita. Anatabasamu anapolifikiria hilo. Upesi anaitwaa simu yake, simu janja. Akachukua picha mbili tatu mbele ya kioo kile. Anamtazama yule Bebe mwingine wa ndani ya kioo. Ni kama anaweza kuzungumza naye, anampa uhai, "Enhe una nini sasa? Ulidhani nitakuwa mtumwa daima? Tazama! Mwili wangu unanilipa...tabia ile chafu, uliyokuwa ukinishutumu kwayo, inaeleka kunitajirisha. Upo hapo?!" Anatamka akitazamana na taswira ile. Safari hii huyu Bebe wa kwenye kioo hamjibu na wala habadiliki katika namna yoyote ile. Bali anafanya kile anachokifanya kwa kuigiza. Akicheka naye anacheka, akiruka anaruka. Bebe akatoka ndani ya chumba hiki akiwa na pochi yake ndogo. Anatoka nje akipewa salamu lukuki na vijakazi wake. Anazipokea kishingo upande kana kwamba hazistahili. Na kweli hazistahili! Anajua fika kuwa ima fa ima, muda wowote ule atanyang'anywa mji huu. Anaitazama nyumba hii kwa nje, kisha analigeukia gari lake na kulitazama kwa macho ya aibu. Dhamiri yake inamsuta kwa kutumia kisicho chake. Ilikuwa wazi sasa kuwa ameachana na kampuni ya Bwana Didas. Anaachana na mawazo haya baada ya kukumbuka kuwa hana muda wa kuwaza yaliyopita. Bado kitambo kidogo, atamiliki majumba makubwa hata kumi ya kifahari. Wasiwasi wa nini? Ofa mbalimbali za matangazo bado zimepanga foleni kuhitaji saini yake. Hata jioni hii anaenda kuongelea dili linalohusisha pesa. Ana shida gani sasa? Na zaidi ya yote, amefahamiana na J4. Ambaye ana madili ya maana zaidi yanayohusisha fedha nyingi chekwachekwa. Analiondoa gari lake taratibu na kuanza safari ya kuelekea walikopanga kukutana na msanii Kenzy. "Nipo njiani!" "Ooh okey, mi nimeshafika mama. Nakungoja wewe tu." Ni sauti ya Kenzy ndani ya simu ya Bebe. "Santeeee!" "Take care." Simu inakatwa. Kabla hajaitua chini, inaingia simu nyingine ambayo inaanza kuzungumza papo hapo bila yeye kuiruhusu. "Mlimbwende! Hakikisha anajaa kwenye mfumo huyo msanii. Naona ameshaanza kulainika." Bebe anashtuka. Ni sauti ya J4. "Wewe ina maana umeidukua simu yangu ama?" Anauliza akiwa na hamaniko. "Usiwe na hofu bibiye...mimi nimekutafuta tu kwa muda huu, na kwa bahati nikakuta unaongea na nyama mpya. Nilitaka kukusalimia tu." "Mh kwa nini lakini? Biashara gani hizo unaleta sasa? Masuala ya kudukuana mi staki." "Alaa basi sawa, nitakutafuta usiku." Simu ile ikakatwa. Kukatwa kwa simu hii, kukaambatana na Bebe kupokea ujumbe wa kutoka kwa namba hii ngeni. Ujumbe uliokuwa na ile picha yake nzuri aliyojipiga kwenye kioo chumbani mwake! Maneno chini yameandikwa, *What a beautiful lady!* Imemfikiaje huyu? Hajui. Na wala hata hajaitundika mitandaoni. Bebe akakosa la kufanya, akatabasamu na kuendelea na safari yake. J4 mdukuaji kwenye ubora wake. ---------------- Aisee 🥱, Tukiwa bado tunakitafuta kiini cha riwaya yetu ya *KIBIRITINGOMA*, Fanani wenu ninafurahishwa sana na juhudi zenu za kuisambaza link ya chaneli yetu. Hakika mnastahili kila kilicho bora! Msiache kushare link ya chaneli, acha reaction na toa maoni yako kwenye 0763204351. Mtunzi anapokea yote! Riwaya hii inaendelea...
Image from MAJIVU YA FASIHI. 📖🪶: RIWAYA; *KIBIRITINGOMA* MTUNZI; *GODLOVE KABATI* KWENDA KWA; *MAJIVU Y...
❤️ 👍 ❤‍🔥 🔥 🫂 8

Comments