Samson Ernest
Samson Ernest
May 25, 2025 at 09:12 AM
KIBURI KINATANGULIA KABLA YA ANGUKO BAYA LA MTU Mit 18:12 SUV [12] Kabla ya uharibifu moyo wa mwanadamu hujivuna; Na kabla ya heshima hutangulia unyenyekevu. Sio ajabu kuona mtu aliyefika viwango fulani vya utumishi wake akashuka chini ghafla, yale matendo makuu ya Mungu yaliyokuwa yanajidhihirisha kupitia yeye katika huduma yanakuwa hayaonekani tena. Bora usione matendo makuu ya Mungu kwa muda alafu huyo mtu awe salama kiroho, shida inakuja mtu huyo anapoteana kabisa, kile alichokuwa anakifanya na Mungu anaonekana kinakuwa hakionekani tena. Nini hutokea? Mtu anapofanya jambo la ki-Mungu, matendo makuu ya ki-Mungu yakadhihirika kwa uwazi, wengi huinuka na kuchukua utukufu wa Mungu. Huanza kujiona ni bora kuliko wengine, kile amekifanya na Mungu akaonekana kwa uwazi, badala ya kumtukuza Yesu na kumrudishia utukufu wake, wao hubeba hayo na kujiona wao ndio wamefanya kwa nguvu zao. Ukimsikiliza mtu aliyeinuka kiburi utamwona, vile anaongea anaonyesha wazi yeye ndiye anasababisha hayo mambo makuu ya Mungu yatokee kwa uwezo wao, na mara nyingi huondoa nafasi ya Mungu katika hayo. Ukiona kiburi kimekuwa kikubwa, ujue anguko lipo karibu mno, njia mojawapo ya anguko la mtu ni kiburi kuinuka ndani yake. Yak 4:6 SUV [6] Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu. Ukimwona mwamini yeyote ameinuka kiburi au anaanza kuwa na kiburi mwombee haraka, au mshauri kwa upendo, kwa sababu anguko lake lipo karibu mno, kwa lugha rahisi kushuka kwake chini kupo mlangoni. Ukiona matendo makuu yanatokea kupitia huduma unayofanya, ongeza unyenyekevu mkubwa kwa Mungu, usije ukainua mabega, utashuka mshuko ambao kunyanyuka tena inaweza ikawa historia. Mtu mnyenyekevu ataendelea kula mema ya nchi, Mungu ataendelea kumtumia zaidi, sivyo hivyo tu, ataendelea kuongezeka viwango vya juu zaidi siku kwa siku. Ukitaka kuinuliwa juu na Mungu kwenye eneo lolote lile alilokupa Mungu utumike, liwe la kiroho au kimwili, kuwa mnyenyekevu sana kwa kila hatua unayopiga. Hata kama sasa unaonekana upo chini, kuwa na bidii sana na matokeo mazuri unayopata yasikupe kiburi, endelea kunyenyekea. Luka 14:11 BHN [11] Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa na anayejishusha, atakwezwa.” Maanguko mengi ya watu yanatokana na viburi vyao, wanaweza kukubali au kukataa ila kabla ya kuanguka kiburi kilitangulia, Mungu alivyo mwema aliwaonya kabla ya kuanguka kwao. Jilinde sana na kiburi, ni moja ya sumu mbaya sana kwa maendeleo mazuri ya mwamini, anaweza asifike hatima njema aliyoiweka Mungu katika maisha yake. Na mbolea nzuri ya kustawisha hatua zako ni unyenyekevu. Soma neno ukue kiroho Liwe jua iwe mvua soma Biblia na kutafakari Mungu akubariki sana Samson Ernest
🙏 ❤️ 5

Comments