
DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
June 12, 2025 at 06:28 PM
*MASOMO YA MISA, JUNI 13 2025.*
*IJUMAA YA JUMA LA KUMI, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA C(I).*
*KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU ANTONI WA PADUA, Padre na Mwalimu wa Kanisa.*
*RANGI YA KILITURJIA: NYEUPE 🤍*
*SOMO LA KWANZA*
*Somo katika barua ya pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (2 WAKORINTHO 4: 7 — 15)*
Yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka pamoja namyi mbele yake. Ndugu: Tunayo hazina hii [ya utume] katika vyombo vya udongo ili ionekane ya kuwa uwezo huu mkubwa mno unatoka kwa Mungu, si kwetu. Tunasongwa toka pande zote, lakini hatugandamizwi chini. Twahangaika, lakini hatukati tamaa. Tunadhulumiwa, lakini hatuachwi bila msaada. Tunaangushwa lakini hatuangamii. Kila wakati tunayachukua maumivu ya kifo cha Yesu miilini mwetu, ili uzima wake Yesu ufafanuke pia katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio wazima tunatolewa daima tufe kwa ajili ya Yesu ili uzima wake Yesu ufafanuke pia katika miili yetu inayokumbwa na kifo. Kwa hiyo ndani yetu sisi kinatendeka kifo, ndani yenu ninyi uzima. Lakini roho ya imani tuliyo nayo ni sawa kwetu na kwenu kama ilivyoandikwa: Nilisadiki, kwa hiyo nimesema." Nasi tunasadiki tukisema. Tunajua ya kuwa yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka pamoja nanyi mbele yake. Hayo yote nayavumilia kwa ajili yenu, ili kwa shukrani ya wengi zaidi neema iongezeke na kumtukuza Mungu zaidi.
*Neno la Bwana.....*
*Tumshukuru Mungu.*
*ZABURI YA KUITIKIZANA*
Zaburi 116: 10 — 11, 15 — 16, 17 — 18 (K.) 17a
*K. Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru, ee Bwana.*
Nilitumaini hata niliposema,
"Mimi nimetaabika sana,"
nami nilisema katika mshtuko wangu,
"Watu hawa wote ni waongo." *K.*
Kina thamani kubwa machoni pa Bwana
kifo cha wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
mimi ni mtumishi wako, nwana wa mjakazi wako;
umevifungua vifungo vyangu. *K.*
Nitakutolea dhabihu ya shukrani,
na kulita jina la Bwana.
Nitamtimizia Bwana nadhiri zangu
mbele ya watu wake wote. *K.*
*SHANGILIO LA INJILI*
Wafilipi 2: 15d, 16a
*K. Aleluya. W. Aleluya.*
K. Mtang'aa kama mianga katika ulimwengu, mkilishikilia neno la uzima.
*W. Aleluya.*
*INJILI*
Kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye.
*† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo (MATHAYO 5: 27 — 32)*
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Mmesikia kwamba imenenwa: Usizini.' Nami nawaambieni, kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kulia likikukosesha, uling'oe na kulitupilia mbali, kwa maana yakufaa zaidi kupotewa na kiungo kimoja kuliko kutupwa mwili wako mzima Jehanamu. Na mkono wako wa kulia ukikukosesha, uukate na kuutupilia mbali. Afadhali upotewe na kíungo kimoja kuliko kutupwa mwili wako mzima Jehanamu. Tena imenenwa, Mtu anayemwacha mke wake, ampe hati ya talaka." Mimi lakini nawaambieni, kila anayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu va ndoa ya maharimu anamtia katika hali ya uzinzi; kadhalika mtu akimwoa mwanamke aliyeachwa, anazini."
*Injili ya Bwana......*
*Sifa Kwako Ee Kristo.*
