
Wizara ya Afya Tanzania
June 9, 2025 at 06:38 PM
WIZARA YA AFYA, MUHAS KUSHIRIKIANA KUTOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WATAALAM WA MAABARA
NA WAF – DAR ES SALAAM
Wizara ya Afya inaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutoa Mafunzo ya Uongozi kwa Wataalam wa Maabara nchini kwa kutumia mbinu ya Afya Moja.
Akifungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam Juni 09, 2025, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema mpango huo utawasaidia wataalam wa Maabara za Afya ya Binadamu na Mifugo kuwa na ujuzi bora wa kiuongozi.
Dkt. Magembe amesisitiza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo viongozi wa maabara katika kujenga mahusiano, udhibiti wa rasilimali, kuandaa na kutekeleza mipango mikakati, ubora wa huduma za maabara na upimaji wa magonjwa ya mlipuko.
“Hii itatoa fursa kwa washiriki kupata maarifa ya kina ya kiuongozi na mbinu za kisasa za kuboresha huduma za maabara,“ amesema Dkt. Magembe.
Aidha, Dkt. Magembe amesema mafunzo hayo kwa vitendo yatawawezesha washiriki kutumia mbinu bora za utatuzi wa changamoto katika sekta ya maabara na kuboresha utendaji wao kazini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Matengenezo ya Vifaa Tiba, Dkt. Alex Magesa amesema ubora wa huduma za maabara ni nguzo muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa ujumla, hasa katika utambuzi wa magonjwa na ufuatiliaji wa mlipuko.
Amesisitiza kuwa mafunzo haya ya uongozi yataongeza ufanisi wa wataalam wa maabara kwa kuwawezesha kusimamia mifumo ya huduma kwa weledi na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Mafunzo haya yanatarajiwa yatahitimishwa Desemba 12, 2025, ambapo wataalam wa maabara watakuwa wamepata ujuzi wa kutosha wa kiuongozi na mbinu bora za kusimamia mifumo ya maabara nchini.
👍
❤️
🎉
😮
🙏
🤝
11