Wizara ya Afya Tanzania

Wizara ya Afya Tanzania

231.4K subscribers

Verified Channel
Wizara ya Afya Tanzania
Wizara ya Afya Tanzania
June 10, 2025 at 07:30 AM
MADAKTARI BINGWA WA SAMIA WATAKIWA KUHAMASISHA JAMII KUJENGA UTAMADUNI KUPIMA AFYA MARA KWA MARA Na WAF - MOROGORO Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Bw. Herman Tesha, amewasisitiza Madaktari Bingwa wa Rais Samia kutoa hamasa kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali za afya zao kwani itasaidia wananchi kujitambua mapema hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Mhe. Tesha amesema hayo Juni 9, 2025 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati akizungumza na Madaktari Bingwa wa Rais Samia watakaotoa huduma za kibingwa na bobezi katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema kambi hiyo pia italenga zaidi kuwajengea uwezo wataalam wa afya waliopo katika hospitali zilizopo katika halmashauri hizo. "Nawashukuru sana madaktari bingwa, pamoja na Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaleta katika awamu nyengine mkoani kwetu, kwani huduma ya afya mtakayokwenda kutoa kwenye halmashauri zetu ni muhimu sana kwa jamii nendeni mkawasaidie wananchi," amesema Bw.Tesha. Kwa upande wa Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa Mkoa wa Morogoro, Bi.Jackline Ndanshau, amesema kambi hiyo ina jumla ya madaktari bingwa 49 ambao watatoa huduma hizo za kitabibu katika mkoa wa Morogoro kwa siku nane (8) na wananchi zaidi ya 3000 watanufaika na kambi hiyo. Bi. Ndanshau, amesema kambi hiyo ya madaktari bingwa italenga zaidi pia kutoa uzoefu kwa jumla ya wataalam wa afya 200 kwa upande wa magonjwa ya akina mama, watoto, ukunga, pamoja na huduma za upasuaji. Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Best Magoma, amesema wamepokea ugeni huo na watatoa ushirikiano wa hali ya juu ili azma ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma bora kwa wananchi ikamilike. Dkt. Magoma pia amewataka wataalam wa afya katika halmashauri ambazo zitakuwa na madaktari bingwa kutumia fursa hiyo kujiongezea uzoefu wa kitabibu.
👍 😮 🙏 ❤️ 9

Comments