
Wizara ya Afya Tanzania
June 14, 2025 at 01:23 PM
WATUMISHI SEKTA YA AFYA WATAKIWA KUVUKA MALENGO KIUTENDAJI
Na WAF - MOROGORO
Waganga wakuu wa mikoa, watalamu, waratibu, watoa huduma na watumishi katika Sekta ya Afya wamepewa rai kuendelea kuona umuhimu wa kuhakikisha kila mtu katika eneo lake la kazi anafikisha na kuvuka malengo ambayo sekta ya afya imejiwekea hususani katika masuala ya chanjo.
RaI hiyo imetolewa leo Juni 13, 2025 mkoani Morogoro na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Dkt. Otilia Gowelle wakati wa akifunga mkutano wa mwaka wa wadau wa chanjo nchini.
“Tumeshinda kwa kishindo mpaka sasa wote tumefikia asilimia 96 kwa uchanjaji lakini tunahitaji kufika asilimia100, na hatuna sababu ya kushindwa maana tumeshajiwekeza katika miundombinu, vifaa tiba, magari ya minyororo baridi na upatikanji wa chanjo, na mchango Serikali na wadau hauwajawahi kukosekana hata siku Moja,” amesema Dkt. Gowelle
Dkt. Gowelle pia ametoa rai kwa wataalam hao kutumia rasilimali kwa uadilifu na mpangilio ili ziwafae na kufikia malengo yaliyowekwa.
Amesema wakati wa utekelezaji wa hayo yote ni vema watoa huduma na watumishi wa umma wakafuata na kuzingatia miongozo ya Serikali iliyopo ili kuhakikisha kazi zinafanywa kwa umakini.
Pia amekazia kuhusu suala la ukusanyaji na utaunzaji wa taarifa ambazo zimekuwa msaada kwa watoa maamuzi linapokuja suala la vipaumbele hususani katika masuala ya takwimu na pale wapatapo changamoto wasisite kuomba msaada ngazi za juu.
Aidha Dkt. Gowele ameziasa timu za afya ngazi ya halmashauri na mikoa kuhakikisha wanajumuisha vifungu vya chanjo katika kila maeneo ya kazi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Georgina Joachim amesema ni mpango wao kuhakikisha wanayasimamia yale yote ambayo bunge la chanjo limeyaazimia katika kuimarisha afua za chanjo nchini kwa ustawi na maendeleo ya taifa.