
Aviation Tanzania 🇹🇿
June 9, 2025 at 10:51 AM
https://www.instagram.com/p/DKrUuZ9t2ms/?igsh=bW1pY2NoamRmdGdl
*Delta yaonya kusitisha agizo la ndege mpya za Airbus kutokana na ushuru wa Marekani*
The Kampuni ya ndege ya Delta Air Lines imesema kuwa ikiwa serikali ya Marekani itaweka ushuru mpya kwa ndege na vipuri vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi, kampuni hiyo inaweza kuacha kununua ndege kutoka nje na pia kufuta baadhi ya safari zake za kimataifa, hatua inaweza kuathiri zaidi ya abiria milioni 10 ambao husafiri kwa kutumia ndege za kampuni hiyo kwa mwaka.
Delta ilitoa taarifa hiyo katika Wizara ya Biashara ya Marekani wiki iliyopita, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa serikali kuhusu usalama wa taifa unaohusiana na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje Uchunguzi unaoweza kusababisha serikali kuongeza ushuru wa ndege, injini na vipuri vya ndege kutoka nje.
Kampuni hiyo imesema kuwa ikiwa ushuru huo utaanza kutekelezwa bila kampuni kupewa muda wa kujiandaa, utaathiri uwezo wa Marekani kutengeneza ndege, na pia utaifanya Delta ishindwe kununua ndege mpya – iwe kutoka ndani ya Marekani au kutoka nje.
Katika miaka ya 2023 na 2024, Delta ilinunua ndege 47 aina ya Airbus kutoka Canada, Ujerumani na Ufaransa. Delta imesema kuwa kama ushuru huo ungekuwepo wakati huo, kampuni hiyo isingeweza kuendelea na safari zake za kuhudumia abiria milioni 10 kwa mwaka. Pia wamesema kuwa hali kama hiyo inaweza kujitokeza tena endapo ushuru mpya utaanza kutumika.
Delta inaweza kulazimika kufuta mikataba ya ununuzi wa ndege ambayo tayari imeingia, na kuacha mipango ya manunuzi mpya ya ndege, jambo ambalo litaathiri kampuni zinazotengeneza ndege nchini Marekani kama vile Boeing na Airbus, kwa sababu baadhi ya ndege hizo hutengenezwa sehemu mbalimbali duniani kwa kushirikiana.
Mnamo mwezi Aprili, serikali ya Trump ilitangaza ushuru wa asilimia 10 kwa karibu ndege zote na vipuri vinavyotoka nje ya nchi. Ikiwa ushuru huo utaongezwa zaidi, Delta imesema inaweza kuahirisha au kufuta maagizo ya ndege mpya.
Wizara ya Biashara ya Marekani, kupitia waziri wake Howard Lutnick, imesema inatarajia kukamilisha uchunguzi huu mwishoni mwa mwezi Juni na baadaye kutoa mapendekezo kwa Rais Trump ili afanye uamuzi wa mwisho.
Wadau wengine wakubwa wa biashara, kama vile Chama cha Biashara cha Marekani na Business Roundtable (jumuia ya wakurugenzi wakuu wa mashirika makubwa), pia wameonya kuwa ushuru huo unaweza kudhoofisha sekta ya anga, kupunguza usalama, na kuharibu mnyororo wa usambazaji wa vipuri.
Makampuni ya ndege na viwanda vya kutengeneza ndege sasa yanaiomba serikali ya Marekani irejee kwenye makubaliano ya kimataifa ya mwaka 1979 ambayo yaliruhusu biashara ya ndege kufanyika bila ushuru. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, sekta ya anga ya Marekani ilikuwa inapata faida ya hadi dola bilioni 75 kwa mwaka.