
Aviation Tanzania 🇹🇿
June 13, 2025 at 06:07 AM
https://www.instagram.com/p/DK1IbDKttU8/?igsh=MXFiZG5rMjc0cGR3dA==
*Abiria mmoja anusurika katika ajali ya Air India, asimulia hali ilivyokuwa**
Wakati dunia ikiomboleza ajali mbaya ya ndege ya Air India iliyotokea mchana wa Alhamisi Juni 12,2025 na kusababisha vifo vya mamia ya watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo, taarifa mpya zimetolewa na kuvunja hali ya ukimya zinazothibitisha kuwa abiria mmoja pekee amepatikana hai.
Vishwash Kumar Ramesh, raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 40, alipatikana akiwa hai katikati ya miili ya marehemu katika eneo la ajali, saa chache baada ya polisi kuthibitisha kuwa hakuna mtu aliyenusurika.
Alikimbizwa Hospitali ya Serikali ya Asarwa, Ahmedabad, ambako kwa sasa amelazwa katika wodi ya kawaida, akiwa na majeraha ya kifua, macho na miguu.
Vishwash alisimulia kuwa muda mfupi tu baada ya ndege hiyo kupaa, alisikia mlio mkubwa kisha ndege ikaanguka ghafla. Alisema tukio hilo lilitokea kwa kasi ya kushangaza kiasi kwamba hakuwa na muda wa kuelewa kilichotokea. Alipoamka, alijikuta akiwa katikati ya miili ya watu waliopoteza maisha. Alieleza kuwa alikuwa na hofu kubwa na alipoona anaweza kusimama, alikimbia kutoka eneo hilo huku akizungukwa na mabaki ya ndege. Mtu mmoja alimtokea na kumsaidia kumpakia kwenye ambulensi, na ndipo akafikishwa hospitalini.
Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Gatwick, Uingereza, ilibeba watu 242 wakiwemo wafanyakazi wa ndege. Air India imethibitisha kuwa kati ya abiria 230, 169 walikuwa raia wa India, 53 Waingereza, 7 kutoka Ureno, na 1 kutoka Kanada. Vishwash alikuwa akirejea London pamoja na kaka yake, Ajay Kumar Ramesh, mwenye umri wa miaka 45, baada ya kutembelea familia yao nchini India.
Alieleza kuwa yeye na kaka yake walikuwa wametoka kutembelea mji wa Diu, lakini walikuwa wamekaa katika mistari tofauti ndani ya ndege. Aliongeza kuwa hadi sasa hajui aliko kaka yake na anaendelea kumtafuta, akitumai bado yuko hai.
Katika hospitali hiyo hiyo, mamia ya ndugu na jamaa wa abiria waliokuwemo kwenye ndege hiyo wanaendelea kufuatilia taarifa, huku wengine wakitafuta wapendwa wao ambao bado hawajapatikana.
Taarifa hizi zimetolewa baada ya Kamishna wa Polisi wa Ahmedabad, G.S. Malik, awali kusema kuwa hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo, kutokana na mlipuko mkubwa ulioharibu kabisa sehemu ya ndege na kusababisha vifo vingi papo hapo, wakiwemo wanafunzi waliokuwa kwenye bweni la Chuo Kikuu cha Tiba cha B.J. ambako ndege hiyo iliangukia.