
Bank of Tanzania
June 16, 2025 at 07:19 PM
SERIKALI YASAINI MIKATABA YA UNUNUZI NA USAFISHAJI DHAHABU
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesaini mikataba ya ununuzi na usafishaji dhahabu na kampuni za uchimbaji madini pamoja na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita (GGR).
Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imefanyika leo, tarehe 16 Juni 2025, katika Ukumbi wa Kambarage uliopo Wizara ya Fedha jijini Dodoma, na kushuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, pamoja na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde.
Dkt. Nchemba alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini, kinachowataka wachimbaji kuuza asilimia 20 ya uzalishaji kwenye masoko ya ndani, ikiwemo Benki Kuu yenye haki ya kwanza ya ununuzi wa dhahabu. Alisema hatua hiyo itaongeza akiba ya fedha za kigeni na kusaidia viwanda vya usafishaji dhahabu nchini kupata ithibati ya kimataifa ya LBMA.
Alibainisha kuwa hadi sasa BoT imenunua tani 5 za dhahabu zenye thamani ya dola milioni 554, zaidi ya lengo la dola milioni 350 kwa mwaka 2024/25. “Hii ni hatua ya kihistoria kwa sababu inahakikisha dhahabu inasafishwa hapa nchini na kutunzwa kama sehemu ya akiba ya taifa,” alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa lengo la BoT ni kununua tani 6 kwa mwaka wa fedha 2024/25, huku akitoa wito wa kuendeleza mkakati huu wa kitaifa kwa kuwa bei ya dhahabu imeendelea kupanda kimataifa.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, alisema mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 9.0 mwaka 2015 hadi 10.1 mwaka 2024/25. Mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali yameongezeka kutoka Sh. bilioni 162 hadi Sh. bilioni 753, lengo likiwa ni kufikia Sh. trilioni 1.
Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema mpango wa ununuzi wa dhahabu ulianza mwaka wa fedha 2022/23 ili kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje na kuongeza akiba ya nchi ya fedha za kigeni.
Makampuni ya Shanta Mining, Buckreef, Geita Gold Mining na Kiwanda cha Usafishaji Dhahabu cha Geita (GGR) yamesaini mikataba hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na serikali katika kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini.
https://www.instagram.com/p/DK-H2dWIYlM/?igsh=MXFodXplaXZwcjBpOQ==
👍
❤️
😂
😢
🙏
❤
👎
💃
🤝
32