
Bank of Tanzania
June 18, 2025 at 06:06 PM
DKT. NCHEMBA AIPONGEZA BENKI KUU KWA USIMAMIZI MAHIRI WA UCHUMI
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mchango wake mkubwa katika kusimamia kwa ufanisi uchumi wa taifa na kuchochea ukuaji endelevu wa maendeleo.
Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo tarehe 18 Juni 2025 jijini Dodoma, alipokutana na Bodi ya Wakurugenzi ya BoT, inayoongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Nchemba alisema licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikumba dunia, Tanzania imeendelea kustawi kiuchumi, hali ambayo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na usimamizi madhubuti na utendaji bora wa Benki Kuu. Alieleza kuwa ufanisi huo umechangia kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha uthabiti wa kiuchumi.
Aidha, aliipongeza Benki Kuu kwa mafanikio katika kusimamia sekta ya fedha, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa fedha za kigeni pamoja na kushughulikia kwa ufanisi malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za kifedha, hususan mikopo inayotolewa na taasisi za huduma ndogo za fedha.
Vilevile, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki Kuu kwa mchango wake mkubwa katika jitihada za kuiondoa Tanzania kwenye orodha ya nchi zenye mapungufu ya kimkakati katika udhibiti wa utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi (Grey List), hatua ambayo ni ushahidi wa uimara wa mifumo ya udhibiti wa fedha nchini.
Aliitaka BoT kuendeleza weledi katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akiahidi kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana kwa karibu na Benki Kuu ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, alieleza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa umahiri mkubwa, kwa lengo la kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, kukuza uchumi na kuchangia ustawi wa taifa kwa ujumla.
https://www.instagram.com/p/DLDRx2GIvYI/?img_index=4&igsh=cXR2dDllMWcxZzVh
👍
😂
❤️
🇹🇿
🌹
👏
🖕
😢
🙏
31