
DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
June 19, 2025 at 07:55 PM
*MASOMO YA MISA, JUNI 20 2025.*
*IJUMAA YA JUMA LA KUMI NA MOJA, KIPINDI CHA KAWAIDA, MWAKA C(I).*
*RANGI YA KILITURJIA: KIJANI KIBICHI💚*
*SOMO LA KWANZA*
"Na juu ya hayo yote, mambo yanayonisonga siku kwa siku, yaani uchungaji wa makanisa yote."
*Somo katika barua ya pili ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (2 WAKORINTHO 11: 18, 21b — 30)*
Ndugu: Kwa kuwa wengi wanajisifia kwa mambo ya kimwili, nami nitajisifu. Chochote kile ambacho mtu angethubutu kujivunia — ninajisemea kama ujinga — nami ninathubutu kujisifia. Je, wao ni Waebrania? Nami pia. Je, wao ni Waisraeli? Nami pia. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Nami pia. Je, wao ni watumishi wa Kristo? Nasema kiwazimu, mimi ni mtumishi wa Kristo kupita wao, maana nilivumilia taabu nyingi zaidi, nilitupwa gerezani mara nyingi zaidi, nilipigwa kupita kiasi, nilikuwa katika hatari ya kufa mara nyingi. Mara tano nilichapwa kwa Wayahudi mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nilipigwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe. Mara tatu nilivunjikiwa meli, nikashinda baharini usiku na mchana. Mara nyingi nilikuwa safarini, katika hatari ya mito, hatari za wanyang'anyi, katika hatari zilizotoka kwa jamaa, hatari zilizonipata kwa watu wa mataifa, hatari za mjini, hatari za jangwani, hatari za baharini, hatari kwa ndugu wa uwongo; katika taabu na masambufu, katika mikesha mingi, katika njaa na kiu, kwa kufunga mara nyingi, katika baridi bila nguo. Na juu ya hayo yote, mambo yanayonisonga siku kwa siku, yaani uchungaji wa makanisa yote. Nani atapatwa na udhaifu, nisipatwe na udhaifu nami? Nani anakwazwa, nisipate hasira mimi? Ikitakiwa kijisifu, haya nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.
*Neno la Bwana...*
*Tumshukuru Mungu.*
*ZABURI YA KUITIKIZANA*
Zaburi 34: 2 — 3, 4 — 5, 6 — 7 (K.) 18b
*K. Bwana huwaokoa wanyofu katika taabu zao zote.*
Nitamtukuza Bwana kila wakati,
sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Nafsi yangu itajisifu katika Bwana;
wanyonge wasikie na kufurahi. *K.*
Mtukuzeni Bwana pamoja nami;
tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nilimtafuta Bwana, akanijibu;
akaniokoa katika hofu zangu zote. *K.*
Mtazameni Mungu mkang'are;
na nyuso zenu zisihuzunike.
Mnyonge huyu aliita,
naye Bwana akamsikiliza,
akamwokoa na shida zake zote. *K.*
*SHANGILIO LA INJILI*
Mathayo 5: 3
*K. Aleluya. W. Aleluya.*
K. Heri walio maskini rohoni, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
*W. Aleluya.*
*INJILI*
"Penye hazina yako, ndipo moyo wako ulipo."
*† Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Mathayo (MATHAYO 6: 19 — 23)*
Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, "Msijiwekee hazina duniani wanapozitafuna nondo na mchwa, na wawezapo kuingia wezi na kuziiba. Bali jiwekeeni hazina mbinguni, wasikozitafuna nondo na mchwa, wala wasikoweza kuingia wezi na kuziiba. Kwa maana penye hazina yako, ndipo ulipo moyo wako. Taa ya mwili ni jicho. Basi, jicho lako likiwa zima, mwili wako wote utakuwa mwangavu; na jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa gizani. Basi, kama mwanga wako wa ndani ni giza, litakuwa giza la ajabu hilo!"
*Injili ya Bwana........*
*Sifa Kwako Ee Kristo.*
