
MAJIVU YA FASIHI 📖🪶
June 15, 2025 at 07:28 PM
*PAZIA LA FILAMU* 📽🎬
*`IO CAPITANO`* (2023)
Ni kweli kuwa njia ya kuyafikia malengo na kuzitimiza ndoto zetu imejaa miiba, suluba na mateso ambayo hatuna budi kuyavumilia.
Pia ingawa ni mara chache sana njia za mkato hujitokeza, sio salama kuzitumia ili kufikia kile tunachokilenga.
Haya yote yalizingatiwa kwa moyo na vijana wawili, Seydou na Moussa. Vijana waliokulia katika familia zilizoendelea kusota na kuwa mateka wa umasikini wa kudumu.
Walikuwa masikini lakini walikuwa na furaha. Furaha ambayo ilidumisha upendo na amani kwenye maskani yao.
Walijiona matajiri kila walipokaa pamoja, kula, kunywa na kucheza ngoma za kiasili pamoja. Umoja wao ukaipiga teke fikra ya umaskini kwenye bongo zao.
Wengine wote waliridhika...wote, isipokuwa Seydou na Moussa binamu yake.
Kutoridhika kwao, ndiko kunaifanya filamu hii iwe moja kati ya zile *bora za muda wote*. Kulikoni? Songa nami 👇🏼.
Ni ubora wao tu, katika kutunga na kuimba mashairi ya nyimbo mbalimbali. Ama kwa lugha rahisi waweza kuwasifu kuwa walikuwa na kipaji.
Naam, walikuwa na talanta ya kuimba.
Kipaji chao kikawaaminisha kuwa, wanaweza kuyaandika majina yao kwa wino wa dhahabu kwenye mioyo ya kila sikio la shabiki atakayesikiliza nyimbo zao.
Sio hapa Afrika tu...hata Ulaya!
Eeh hata Ulaya! Wakaamini kuwa hata wazungu watapanga foleni kuzililia saini zao. Vipaji vyao vikawaaminisha hivyo.
Wakaendelea kuvinoa.
Kwa desturi, kipaji humtesa sana mwenye nacho. Huwaka na kuteketea nafsini mwake kama moto mkali. Humfanya mtu ajihisi kama mwenye deni kubwa maishani mwake.
Naam,
Talanta yao, ikawafanya Seydou na Moussa wasilale usiku na mchana.
Ikawafanya wasote na kupitia suluba, kufanya kazi na kutunza fedha kwa muda wa miezi sita. Lengo lao?
Wapate fedha itakayowatosheleza kwa safari yao kutoka Senegal mpaka Ulaya.
Wakiwa chini ya ule umri wenye ruksa ya kutumia vileo, wakaweka nia ya kusafiri kwenda Ulaya kwa njia haramu.
Hawakutaka kumuaga yeyote maana kwa hakika wasingeruhusiwa na wazazi wao.
Na hawakutaka kitu chochote kiwazuie.
Wakakwepa baraka za wazazi na walezi wao na badala yake wakazikimbilia baraka za Sangoma. Mganga ambaye alipeperusha usinga wake huku na huko, akinena maneno ya kilugha yasiyoeleweka. Kisha akaibariki safari yao.
Seydou na Moussa wakatoroka nyumbani kwao wakiwa na matumaini na heri nyingi ya kule waendako.
Taratibu, wakaanza kuipasua ramani kutoka Dakar, Senegal kuelekea Kaskazini.
Njia za magendo na usafirishaji haramu wenye unafuu wa nauli na uhakika wa kufika kule wanakoelekea, vikazidi kuwaaminisha kuwa safari yao bado ni salama. Ni noti kadhaa tu zilizotosha kuvifunga vinywa vya askari wa mipakani waliodai rushwa. Ama la uende kuozea jela. Nani anataka jela?
Wanatoa noti kadhaa na kubaki salama kuendelea na safari yao. Usalama huu mpya, katika nchi za kigeni ukaungana na shetani kama abiria mpya kwenye safari yao.
Barabara kwa barabara, mipaka kwa mipaka, kituo kwa kituo. Hatimaye wakapata usafiri wa bei cheee, utakaowafikisha Tripoli, mji mkuu wa Libya. Usafiri ambao utawaepusha na manyanyaso ya jangwa la Sahara.
Ni hapa mambo yalipoanza kubadilika. Shetani akachanua makucha yake, na matumaini yao yakaanza kuyeyushwa na lile joto kali na jua lililokasirika la jangwa la Sahara.
Askari jeshi, walinzi wa jangwa wakauvamia msafara wao haramu. Wakadai fedha na mali zao, huku wakiitanguliza sheria mbele kama kitisho cha kuwasweka jela.
Seydou akapona..lakini Moussa akakamatwa kupelekwa jela.
Dhuluma hii iliyofanana na haki, ikawatenganisha ndugu hawa wawili waliokuwa safarini.
Yumkini Seydou aliwahi kusoma kuhusu historia na hadithi za enzi za utumwa darasani. Yale yalikuwa ni nadharia tu, na sasa alikuwa kwenye mafunzo kwa vitendo. Alianza kama msafiri jangwani, ghafla shilingi ikageuka, akawa mtumwa.
Macho yake yakashuhudia hatua zote anazopitia mtu, anapoelekea kukata roho. Ukatili unaofanywa na mwanadamu juu ya ngozi yenye madonda ya mwanadamu mwenzake.
Aliona, aliogopa, alitishika!
Ali-ililia chai na sasa ilikuwa inamchoma kwa joto lake. Seydou kwenye gereza la siri, katikati ya jangwa la Sahara Libya.
Aliyafumba macho yake, akaikumbuka amani aliyokuwa nayo kwenye udongo wa nyumbani kwao. Ni kama malaika mtoa roho alikuwa anarandaranda karibu yake, kumsubiri amalize mkataba wake wa maisha na dunia.
Akatamani walau aombe msamaha kwa mama yake, kabla hajaiaga dunia.
Labda ndotoni pekee, huko ndiko angewasiliana na mamaye.
Kijana wa miaka kumi na sita tu kwenye uso wa dunia, akakomazwa na maisha.
Akautafuta ukombozi katika nchi za kigeni.
Baada ya kubahatika kuukwepa moto wa mchanga jangwani...anakutana na mawimbi ya mauti yanayoelea kwenye mdomo mpana wa bahari ya Mediterranean.
Ni filamu ambayo itakupa kila sababu ya kukijali ulicho nacho, na kukuasa kuepuka tamaa mbaya. Huku, ukipata ufahamu juu ya ukatili wa usafirishaji haramu wa binadamu. Inaitwa *Io Capitano* ya mwaka 2023.
Hii nd'o maana halisi ya bonge la filamu.
Imeandikwa na Godlove Kabati ✍🏼

❤️
❤
👍
4