
MAJIVU YA FASIHI 📖🪶
June 16, 2025 at 10:35 PM
RIWAYA; *KIBIRITINGOMA*
MTUNZI; *GODLOVE KABATI*
KWENDA KWA; *MAJIVU YA FASIHI channel*
WhatsApp; 0763204351
-----------------
*Sikia,*
*Tafsiri sahihi ya wewe kuwa na umaarufu, ni kujulikana na watu wengi ambao wewe huwajui.*
*Haijalishi wanakujua kwa mema ama mabaya. Lakini daima tambua kuwa, kwenye wengi kuna mengi.*
*Zichunge sana nyendo zako ewe supastaa mwenzangu.*
*Ni kosa moja tu linaweza kuyafuta mema tisini na tisa uliyoyafanya.*
*Nakuandikia haya katika sehemu hii ya kumi na nne.*
Siku zilitembea kwa kasi sana kama mshale hewani. Ndani ya wiki moja baada ya makubaliano ya ana kwa ana baina ya Bebe na msanii Kenzy, hatimaye mtandaoni lilitupwa jiwe jipya lenye mshindo mkuu, ulioyatikisa masikio ya watanzania.
FROLA ATAKUWEPO KWENYE NGOMA MPYA YA KENZY FLAVOUR!
Hii haikuwa taarifa rasmi, bali zilikuwa tetesi tu. Tetesi hizi zikatambaa kwa kasi kama moto mkubwa nyikani. Macho na masikio ya watanzania wote wapenzi wa Bongo fleva vikakaa chonjo kusubiri.
"Acha utani bwana!! Kwamba Frola huyuhuyu, atakuwa video queen kwenye ngoma mpya ya Kenzy?"
"Sa' hapo unabisha nini mzee? Unaambiwa Kenzy flavour amemwaga mpunga wa kutosha kaka. Majuzi tu kamera zimewanasa pale Sheraton wanashoot! We unacheza na media nini?"
Yalikuwa ni maongezi ya vijana wawili wa rika moja, wakipata mlo wa mchana kwenye moja kati ya migahawa, uliokuwa karibu na chuo chao.
Wanakula chakula, vidole vya mikono yao ya kuume vikikamata vijiko kupambana na punje tamu za wali mweupe. Huku vile vya mikono yao ya kushoto vikipapasa vioo vya simu zao. Macho yao yanazidi kupepesa wakikagua kinachojiri kwenye kurasa mbalimbali za mitandao.
"Kama ni kweli, basi hili dude litakuwa na bonge moja la video aisee!"
"Ooh ooh, Bro! Hii *Me and you* itakuwa ni dunia nyingine."
Wakamaliza kupashana habari na kuendelea kuufaidi uhondo wa kile kilichoko kwenye sahani mbele yao.
Dunia ya muziki, ikaisubiri kwa hamu kubwa ile tarehe ya kuachiwa kwa video ya wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour.
Kuhusu ubora wa uimbaji wake, hilo halikuwa suala la kushangaza. Tayari alishafanikiwa kuziteka nyoyo za mashabiki wake wengi tangu walipompa masikio yake. Suala kubwa muda huu lilikuwa ni kuitazama video ya wimbo huu ambao ilisemekana kuwa yule mrembo maarufu nchini Tanzania, yumo ndani.
Mrembo ambaye anajulikana mpaka na watoto wadogo kila wanapoyaona makopo ya *icecream* yaliyopambwa na sura yake.
Siku ya siku ikawadia.
Lile jiwe la kimondo cha *Me and you* lililohaidiwa, likatupwa mitandaoni. Safari hii haikuwa tetesi tena na hakuna aliyetaka kusimuliwa.
Mitandao ya kijamii ikafurika. Watu wakateketeza masalio ya vifurushi vyao vya intaneti ili tu kutazama kunani?
Maajabu,
Ndani ya lisaa limoja tu, takribani watu milioni moja na ushee walikuwa wamezipepesa mboni za macho yao kwenye ukurasa wa msanii Kenzy. Rekodi mpya ikaandikwa nchini Tanzania katika mtandao wa *Youtube* . Msanii wa kwanza Afrika mashariki, kupata watazamaji wengi ndani ya muda mfupi.
Mafanikio!
"Bro siamini macho yangu aisee!" Kenzy flavour alikuwa wima, mikono yake inamtetemeka viganja vyake vinamiliki simu yake. Anachokiona haamini kama ni kweli kinatokea. Amewahi kupandisha video za kutosha, tena zenye mawe ya maana kwelikweli. Lakini hii ilikuwa ni kubwa kuliko.
Haelewi afanye nini. Ni kama anayetaka kupaa na kukimbia kwa wakati mmoja. Anazunguka huku na kule kwenye sebule yake ya kifahari. Mara anaitupa simu ile na kumrukia rafiki yake aliyekuwa karibu kwa shangwe.
Ni furaha tupu! Haya ni mafanikio makubwa kwake katika tasnia hii. Yupo kwenye kilele cha furaha yake.
Upesi anawasiliana na Bebe, na kumshirikisha juu ya hili.
Ni furaha na burudani mara mbili kwa wale wanaosimuliana hadithi za urembo na madaha ya Bebe kwenye video ya wimbo huu. Wimbo wenye mashairi matamu ya mapenzi yenye mchanganyiko wa kiingereza na kiswahili.
Anga la nchi ya Tanzania, likahanikizwa kwa mrindimo wa sauti za wimbo huu.
Umaarufu wake ukatishia kuuweka kwenye daraja moja na wimbo wa taifa.
LE CLUB GRANDE, ukapigwa usiku na mchana. Ukamfikia mpaka Madam Sally na mabinti zake ambao waliufurahia japo kwa matamanio makubwa ya kuipata nafasi kama ile aliyo nayo Bebe.
Mitandao haifichi kitu, wimbo ukapigwa mpaka kwenye vipindi mbalimbali vya runinga. Ukaifikia familia ya Bwana Didas. Watoto wake wakaufurahia, wakajitahidi kuyakariri mashairi yake, mke wake akayatumia mashairi haya kumliwaza mmewe.
Lakini yeye bwana Didas aliutazama wimbo huu kwa uchungu, roho yake imechafuka kwa kisirani, wivu na hasira.
* * * * * *
Jukumu la mashabiki siku zote ni moja tu. Ama ni mawili kwa hakika. Kusifia na kupiga makofi pale panapostahili pongezi vilevile kukosoa na kukemea pale panapohitaji kukosolewa.
Baada ya makofi mengi kupigwa na sifa kedekede kujazwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii kuhusu wimbo huu mpya wa msanii Kenzy Flavour, ghafla likaibuka kundi la wale mashabiki wenye macho ya mwewe yanayotazama na kufanya uchambuzi wa umakini zaidi.
Hawa wakayafuatilia kwa umakini zaidi yale makumbato, ile mipapaso na miguso kwenye video hii...kisha wakarejea na mawazo mapya ambayo abadani hayakutegemewa.
Mawazo haya yaliyobeba hoja mbalimbali, yakaibua mijadala kwenye makundi mbalimbali ya udaku kwenye mitandao ya kijamii.
Wimbi kubwa la wale wanaokesha kujadili maisha ya wasanii, wakaipenda mada iliyosogezwa mezani.
Vikao visivyo rasmi vikaanzishwa.
:Sanaa imeingiliwa!
:Kenzy hakufanya makosa kabisa, alihakikisha hela yake haiendi burebure.
:Alimkamatilia kwelikweli aisee.
:Duh! Kwa namna alivyokuwa anampiga tachi, sidhani kama yule manzi alitoka salama.
Mijadala hii ikaibua hoja ambazo ni kama zilikuwa zinasubiriwa kwa hamu na kiumbe fulani aliyekuwa nyuma ya kioo cha kompyuta yake, ndani ya chumba chake chenye giza la wastani.
Kiumbe huyu akatabasamu kisha kwa utulivu mkubwa, akaendelea kunukuu machache kwenye kitabu chake kidogo chakavu kilichokuwa kando.
Akaendelea kusoma yanayoendelea huko mitandaoni.
:Aaaah wasanii hawa kawaida yao hawa! Tumeshawazoea!
:Kwanza huyo Frola si inasemekana aliwahi kufanya kazi pale LE CLUB GRANDE? Au kumbukumbu zangu haziko sawa?
:Uko sawa mkuu, miaka ya nyuma aliwahi kufanya kazi pale.
:Kwa hio flavour kapita naye? Ila wabongo, hampoi
:Naipenda nchi yangu, kila siku skendo mpya.
:Huenda hii nchi ni chaneli ya vichekesho huko mbinguni.
Maoni haya lukuki yakazidi kuipeleka mada hii kwenye uelekeo ule ule, aliokuwa anautaka.
Kiumbe huyu alikuwa mtandaoni muda huu pia, japo kwa akaunti isiyo rasmi. Kwa maana hiyo, isingekuwa rahisi kujulikana na vyombo vya usalama. Kwa kujiamini akavielekeza vidole vyake juu ya kompyuta ile na kuzicharaza herufi,
:Kwani bado tu hamjaona koneksheni yao?
Akauliza swali lililozua kizaazaa.
Neno koneksheni, kama lilivyotumika mitandaoni kumaanisha video chafu za ngono zinazorekodiwa kwa makusudi ama kimakosa.
Watu waliomuelewa wakamshukia kwa maombi na vingi viulizo, ikiwa ni kweli kitu kama hicho kipo.
:Mnadhani natania? Haya huyu nani?
Akatuma picha, ambayo iliwashangaza wengi. Ni Bebe akiwa na Kenzy, miili yao ikiwa ndani ya mavazi mepesi ya kulalia. Wamekumbatiana na tabasamu zito la huba likitalii nyusoni mwao.
Picha hii inaelezea kila dalili ya wawili hawa kuwa ndani ya chumba kimoja, hotelini.
Baada ya sekunde sitini akaifuta picha hii.
Ilikuwa picha ya kipekee, picha ambayo kila aliyejaribu kuipakua alishindwa. Waliofanikiwa kuiona upesi wakawaka kwa shauku ya kutaka kuiona tena. Lakini isivyo bahati, ilionwa na wachache.
Wakamlalamikia kwa kitendo chake cha kikatili kwa kutundika picha na kuifuta upesi.
:Mnadhani ni nini kiliendelea baada ya hapo?
Akatupa swali jingine.
Watu wakazidi kumshambulia kwa maswali na kudai udhibitisho wa ziada ambao hakuutoa. Wengine wakaifatilia akaunti yake kumchunguza. Mtu huyu ni nani?
Hakuwa wafuasi wengi mtandaoni. Lakini kitendo chake alichokifanya dakika kadhaa nyuma, kikampatia umaarufu wa ghafla.
Naam, jina la ukurasa wake aliouita kwa jina la MUTU MWEUSI ukawa gumzo kwenye mtandao huu.
Mafuriko ya jumbe nyingi kutoka kwa watu mbalimbali yakammiminikia, wakimsihi awatumie picha na video hizo kwenye akaunti zao binafsi, kama ikiwa ni kweli anazo.
Kiumbe huyu, akatabasamu baada ya kuiona fursa.
Namna ambavyo wanadamu wanalalamika kutaka kuziona tupu za wanadamu wenzao wakifanya zinaa.
Wana nini watu hawa?
Tamaa! Tamaa ya ngono.
Macho yao yenye tamaa yanang'aa kwa uchu yakidai shibe kwa kuangalia video hizi chafu zinazojulikana kama *koneksheni* huko mitandaoni.
Watu hawa wanaabudu fedheha kuliko utu.
Kiumbe huyu, J4 akashusha pumzi na kuchepuka kutoka mtandao ule, akaunti yake feki ikayeyuka na kusinzia ghafla. Akaifunga kompyuta yake na yeye akakisogelea kitanda kuutafuta usingizi wake.
Mtego wake umenasa tayari.
Mwanzo wa usingizi wake mtamu, ukawa ndio kengele ya kuwaamsha wale wanaokesha mitandaoni usiku kucha. Linalotafutwa ni jina moja, ama mawili hakika lakini ya mtu mmoja.
Mtu mwenye *koneksheni* ya Kenzy na mrembo Frola. Kampuni za mitandao zikapata wateja lukuki mida hii. Wateja wanaomtafuta mtu mmoja tu.
*MUTU MWEUSI* !!!
*******
Baada ya kazi ngumu ya kurekodi na mahangaiko ya uandaaji wa video ya wimbo huu, kila mtu alikuwa tepetepe kwa uchovu.
Bajeti iliyotengwa kando na Kenzy, ilitosha kabisa kukodi vyumba kadhaa vya hoteli kubwa kwa ajili ya mapumziko ya kundi lote linalohusika na uandaaji wa kazi hii.
Ni katika namna ambayo hakuelewa ilikuwaje, na wala hakukumbuka alifanya nini.
Lakini alijikuta yeye na Bebe, wameamua kupumzika kwenye chumba kimoja. Achana na chumba, hebu tuongeze ukali wa maneno kidogo. Walipumzika kwenye kitanda kimoja.
Yumkini kwa Bebe hili lilikuwa ni pumziko la kawaida. Lakini kwa Kenzy hii ilikuwa ni kama nafasi moja ya kipekee inayojitokeza kila baada ya miaka elfu.
Nafasi ya dhahabu! Nafasi ambayo hakutaka kuipoteza kabisa.
Kulala na mrembo kama huyu kwenye kitanda kimoja? Maajabu!
Pumziko hili likaanza kupata uhai baada ya ngozi za miili yao kugusana. Kila mmoja akalihisi joto la mwenzie. Wakabadilishana joto hili na damu kwenye mishipa yao ikaanza kuchemka. Hisia kali ikasafiri kwenye mishipa hii kwa kasi.
Yule Frola, akabadilika ghafla na kuwa Bebe tuanyemfahamu sisi. Bebe aliyehitimu chuo cha Profesa madam Sally.
Na sasa huyu hapa yuko kazini.
Masomo kwa vitendo bwana!
Ghafla wakachangamkiana.
Wakausahau ule uchovu wa siku nzima uliowafanya wapumzike.
Haoooo, kukurukakara, vuta n'kuvute, wakatapatapa huku na kule.
Dakika thelathini za mahangaiko zikahitimishwa kwa usingizi mzito wa Kenzy Flavour, msanii wa kizazi kipya anayetegemea kuachia ngoma yake hivi karibuni. Huku Bebe akiwa nd'o kwanza amechangamka.
Hii michezo ana uzoefu nayo. Na hapa alikuwa uwanja wa nyumbani.
Mashahidi wa tukio hili walikuwa na ahadi moja tu. Kubaki kimya milele. Japo sio wote ambao wangeitimiza ahadi hii. Wapo waliokataa katakata kubaki kimya. Na ni hawa ambao walimfanya Bebe asipate usingizi.
Binti akasimama baada ya kuhakikisha kuwa Kenzy amelala usingizi wa pono. Akanyata taratibu mpaka kwenye pembe kadhaa za chumba kile na kunasua vipande vidogo vya kamera kwa uangalifu.
Akavitunza mahali salama na kisha akaikota simu yake kufanya mawasiliano na namba ambayo alijua tu kuwa iko hewani kusubiria majibu.
DEAL DONE, akaandika.
BRAVO, akajibiwa.
Akazima simu yake na kurejea kitandani kuubembeleza usingizi. Roho yake ina amani na anauona ushindi mkubwa mbele yake. Mtego umenasa!
_____________________
Aiseeee 😀,
Mitego imenasa! Mitandao imechafuka.
Ngoma ya *ME AND YOU* inazua taharuki ambayo sidhani kama itamuacha mtu salama.
Ni hekaheka!
Tumekuwa familia kubwa sasa, watu Alfu si haba. Haya sasa raection zenu zimwagike hapa.
Nahitaji thelathini tu, tuendelee Alhamisi hii.
Riwaya ya bure hii jama...
30 kati ya 1000. Na hapa mshindwe kweli? 🥱

👍
❤️
🔥
❤
🎬
🤝
16