
Legal Minds Forum ⚖️
June 14, 2025 at 05:11 AM
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania leo imetoa uamuzi katika kesi ya kikatiba ya Rufaa Na. 134 ya Mwaka 2022, iliyofunguliwa na mtetezi wa haki za binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Rufaa hiyo ilisikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa: Jaji Rehema Levira, Jaji Wilfred Rumanyika na Jaji Gerald Ngwembe. Wakili Olengurumwa aliwakilishwa na jopo la mawakili maarufu likiongozwa na Prof. Issa Shivji pamoja na Dkt. Rugemeleza Nshala, Mpale Mpoki na Wakili John Seka.
Kesi hiyo ilihusu kupinga vifungu vya Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya mwaka 2020, vilivyobadili Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Sura ya 3) kwa kuongeza vifungu vya 4(2), 4(3), 4(4), na 4(5). Vifungu hivyo vilionekana kuweka vikwazo katika mashauri ya kikatiba yenye maslahi kwa umma, maarufu kama Public Interest Litigation.
Maelezo ya Vifungu Vilivyolalamikiwa:
Kifungu cha 4(2): Kilihitaji mtu anayetaka kufungua kesi ya kikatiba kuambatanisha kiapo kinachoeleza namna alivyoathirika binafsi na ukiukwaji huo.
Kifungu cha 4(3): Kiliongeza kizuizi kwa mashauri ya maslahi ya umma kwa kutaka mlalamikaji aonyeshe maslahi binafsi sawa na Ibara ya 30(3) ya Katiba.
Kifungu cha 4(4): Kiliweka sharti kuwa kesi dhidi ya viongozi waandamizi serikalini – Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Jaji Mkuu – zifunguliwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali badala ya wahusika hao moja kwa moja.
Kifungu cha 4(5): Kilimtaka mtu anayepanga kufungua kesi kutafuta kwanza nafuu kupitia sheria nyingine zilizopo kabla ya kufungua kesi chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi.
Awali, Mahakama Kuu ya Tanzania iliitupilia mbali kesi hiyo mnamo Februari 15, 2022, kwa maelezo kuwa vifungu hivyo havivunji Katiba wala mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Mahakama Kuu ilisisitiza kuwa vifungu hivyo vinakamilisha Ibara ya 26(2) na 30(3) ya Katiba, na vinaakisi misingi ya utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka, na mfumo wa kimataifa wa haki.
Hata hivyo, Wakili Olengurumwa hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa Mahakama ya Rufaa mwaka huo huo wa 2022.
Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa
Leo Juni 13, 2025, Mahakama ya Rufaa kupitia kwa Naibu Msajili Mhe. Joseph Fovo, imesoma uamuzi huo kwa njia ya mtandao na kubatilisha vifungu vyote vinne vilivyolalamikiwa.
Kwa mujibu wa Mahakama ya Rufaa:
Kifungu cha 4(2) kinavunja dhana ya mashauri ya maslahi kwa umma kwa kuhitaji waathirika binafsi pekee, hali inayokinzana na Ibara ya 26(2) ya Katiba.
Kifungu cha 4(3) ni batili kwa kuwa kinachanganya masharti ya Ibara ya 30(3) (maslahi binafsi) na haki za maslahi kwa umma zinazolindwa chini ya Ibara ya 26(2).
Kifungu cha 4(4) ni batili kwa kuwa Mwanasheria Mkuu hana mamlaka ya kikatiba kuwakilisha mihimili mingine, hasa Mahakama au viongozi wa kisiasa walio huru kikatiba kama Jaji Mkuu.
Kifungu cha 4(5) pia ni batili kwa kuwa hakuna sheria nyingine zinazotoa nafuu ya moja kwa moja kwa mashauri ya maslahi ya umma.
Agizo kwa Bunge
Mahakama ya Rufaa imeagiza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta vifungu hivyo vinne ndani ya kipindi cha miezi 12 kuanzia tarehe ya hukumu. Uamuzi huu umetajwa kuwa ushindi mkubwa kwa wanaharakati wa haki za binadamu na wananchi wanaotetea masuala ya kijamii kupitia Mahakama.
👍
❤️
3