
TRA TANZANIA
June 17, 2025 at 05:19 PM
CG MWENDA AONGOZA KAMPENI YA ELIMU NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIPAKODI
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda tarehe 16 Juni 2025 ameongoza kampeni ya elimu na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara mkoani Simiyu.
Akizungumza wakati wa mkutano na wafanyabiashara mkoani Simiyu, Kamishna Mkuu Mwenda aliwapongeza kwa jitihada zao za kulipa kodi kwa hiari, jambo ambalo amesema linachangia katika maendeleo ya Taifa.
“Nawashukuru sana wafanyabiashara wa Simiyu kwa kuonyesha utamaduni wa kulipa kodi bila kulazimishwa, hii ni ishara ya uzalendo na dhamira ya kujenga Taifa letu,” alisema Mwenda.
Aidha, aliwahimiza wafanyabiashara hao kuendelea na utamaduni huo wa kulipa kodi kwa wakati na kwa hiari ili kusaidia serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kamishna Mkuu Mwenda pia aliwaasa wafanyabiashara hao kutoogopa kufika katika ofisi za TRA iwapo watakumbana na changamoto zozote zinazohusiana na ulipaji wa kodi.
Alisisitiza kuwa TRA iko tayari kusikiliza na kutoa ufumbuzi wa haraka kwa changamoto hizo ili kuondoa migogoro na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara.
“Ofisi zetu ziko wazi kwa wote. Msikate tamaa au kusita kufika kwetu pale mnapokumbana na changamoto za kikodi. Lengo letu ni kuwasaidia na kuhakikisha mazingira ya Biashara yanakuwa rahisi na ya kirafiki,” aliongeza Mwenda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Chama cha Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani Simiyu, Bw. John Bahame Sabu, ameipongeza TRA kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa wafanyabiashara na kuwapa nafasi ya kuuliza maswali na kufikisha changamoto zao.
Alisema kuwa utamaduni huu wa TRA wa kushirikiana na wafanyabiashara umesaidia kupunguza migogoro ambayo hapo awali ilikuwa ikitokea mara kwa mara kati ya wafanyabiashara na mamlaka hiyo.
“TRA imefanya kazi ya kipekee kwa kuwajengea wafanyabiashara uelewa kuhusu kodi na pia kuwasikiliza. Hili limepunguza sana migogoro na kufanya Biashara iwe rahisi zaidi,” alisema Bw. Sabu.
Aidha, Bw. Sabu aliwahimiza wafanyabiashara wenzake kutumia fursa zinazotolewa na TRA kupata elimu zaidi kuhusu mifumo ya kodi na taratibu za ulipaji ili kuepuka makosa yanayoweza kusababisha adhabu au riba kwa wafanyabiashara.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wafanyabiashara na TRA ili kuhakikisha mazingira ya Biashara yanabaki kuwa endelevu na yenye tija kwa Taifa.
Kampeni hiyo inayoendeshwa na TRA kwa mwezi Juni 2025 inalenga kuelimisha wafanyabiashara kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na kuwapa fursa ya kufikisha kero zao moja kwa moja kwa TRA.
Mwisho.

👍
🙏
❤️
😮
😢
29