TRA TANZANIA

TRA TANZANIA

317.1K subscribers

Verified Channel
TRA TANZANIA
TRA TANZANIA
June 20, 2025 at 11:46 AM
MENEJIMENTI YA TRA YAKUTANA KUJADILI BAJETI NA LENGO LA MAKUSANYO KWA MWAKA WA FEDHA 2025/26 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya kikao cha siku tatu kuanzia tarehe 18 hadi 20 Juni 2025, chini ya uongozi wa Kamishna Mkuu, Bw. Yusuph Juma Mwenda, kujadili bajeti ya taasisi hiyo pamoja na lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/26. Kikao hicho, kilichofanyika katika ukumbi wa GerWill Hotel jijini Dodoma, kililenga kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa malengo ya makusanyo yaliyowekwa na Serikali ya Tsh Trilioni 34.93 kwa TRA kwa mwaka wa fedha 2025/26 yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa. Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kamishna Mkuu Bw. Mwenda alisisitiza umuhimu wa watumishi wote wa TRA kuelewa kwa kina lengo la makusanyo ya mapato lililowekwa na Serikali kwa mwaka ujao wa fedha. Alisema kuwa kufanikisha lengo hilo kunahitaji juhudi za pamoja, bidii, na uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwa kila mtumishi wa TRA. “Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa tunachangia kikamilifu katika kufikia malengo ya makusanyo ya mapato. Hili ni jukumu letu la msingi kama TRA, na tunapaswa kulifanya kwa weledi na kujitolea,” alisema Bw. Mwenda. Aidha, katika kikao hicho, menejimenti ya TRA ilifanya mgawanyo wa malengo ya makusanyo kwa Idara za makusanyo pamoja na mikoa yote nchini. Mgawanyo huo ulilenga kuhakikisha kwamba kila idara na mkoa unapewa wajibu wa wazi wa kufikia sehemu yake ya mapato, kwa kuzingatia uwezo wake wa kiuchumi na mazingira ya biashara. Bw. Mwenda alieleza kuwa mgawanyo huo umefanyika kwa uwazi, ili kuhakikisha kuwa kila kitengo na mkoa kinachangia ipasavyo katika lengo la jumla la makusanyo. Kikao hicho kilishirikisha wakuu wa idara, mameneja wa mikoa na vitengo pamoja na wataalamu wa masuala ya bajeti na uchumi kutoka TRA. Mamlaka ya Mapato Tanzania ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa inakusanya Shilingi za kitanzania Trilioni 36.07 kabla ya marejesho na Trilioni 34.93 baada ya marejesho ya mapato ya kodi kwa walipakodi. Mapato yanayokusanywa na TRA yanahitajika kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo na huduma za umma. Kwa mwaka wa fedha 2025/26, TRA imepangiwa lengo la makusanyo ambalo linatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika bajeti ya Taifa. Ili kufikia lengo hilo, taasisi hiyo imejipanga kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sekta binafsi, taasisi za fedha, na walipa kodi ili kuhakikisha mazingira wezeshi ya ukusanyaji wa mapato. Kikao cha menejimenti ya TRA kimechukuliwa kama hatua muhimu katika kuweka msingi thabiti wa kufanikisha malengo ya mwaka ujao wa fedha. Kikao hicho kimehitimishwa kwa ahadi ya pamoja ya kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kufikia lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2025/26. Mwisho.
Image from TRA TANZANIA: MENEJIMENTI YA TRA YAKUTANA KUJADILI BAJETI NA LENGO LA MAKUSANYO KWA ...
👍 🙏 ❤️ 9

Comments