
Kalamu House
June 20, 2025 at 01:32 PM
```SIMULIZI: MALAIKA 2```
```SEHEMU: YA TANO```
Upepo mwanana ulimpuliza akivuta pumzi na kuiona siku njema machoni pake. Anga likifunguka na kuangaza vyema mwanga wa jua bila kuwepo mawingu ya kukinga miwayale ile kwenye uso wa Dunia.
Akiwa baraza ile nje ya chumba chake, aliangaza kilichopo mbele yake akiona barabara na mara kusikia sauti kutoka chini, sauti zaidi ya moja ambazo hakuzitambua na kumfanya asogee kwenye ukingo wa ubaraza ule na kutazama chini na kuwaona mafundi wakiwa na Angelina akiwa ndiye aliyewapokea.
Aliwapeleka lilipo gari na kuwakabidhi funguo ya gari lile huku likitolewa turubai lililotumika kufunika gari lile.
Akiwa tayari amesogea kurudi chumbani kwake, alisita baada ya kuhisi utofauti katika gari lile lililokuwa limefunikwa na kumfanya arudi kuangalia; akiwa hana uhakika kama ni gari lake lile aliloliacha.
Turubai lilitolewa lote na machoni pake aliliona gari aina ya Maserati Levante Trofeo akibaki kama aliyezuzuka baada ya kuliona akishindwa kuamini anachokiona.
Ni gari la ndoto zake na hakutegemea kuliona pale akibaki kukosa majibu na kujikuta akitoka chumbani kwake mbio na kuteremka ngazi zile mpaka chini.
Alifika chini na kusogea dirishani akilitazama kwa uzuri zaidi huku akitabasamu usoni mwake kuonesha furaha iliyomjaa moyoni.
Aliona mafundi wakilitazama na kumwaga sifa za uzuri na ubora wake na Angelina akiwaacha wenyewe na yeye kurudi ndani akiendelea na kazi zake.
“Za Asubuhi!” Malaika alimsalimia baada ya Angelina kuingia ndani.
“Nzuri, umeamkaje!?” alijibu Angelina akimtazama Malaika aliyeonekana kuwa na furaha.
“Salama, sijui wewe!?”
“Niko salama!”
“Lile gari ni la…!” alisita kujua namna ya kuuliza swali hilo ambalo lilimtoka tu mdomoni mwake.
“Ndio lakwako!” alijibu Angelina akiwa amemuelewa hata pasipo swali kumalizika.
“Oooh…!” furaha aliyonayo katika kuthibitisha jambo hilo, alikosa la kuongea zaidi akitamani kumuona baba yake na kumshukuru sana.
Alilichungulia dirishani pale akiona rangi yake ya kijivu namna ilivyo ng’aa, hakika lilikuwa gari la hadhi ya juu na kifahari hata bila kuuliza gharama zake.
Alibaki dirishani pale kwa zaidi ya dakika ishirini kabla ya kuamua kuondoka kurudi chumbani kwake kwenda kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo ikiwa hata maswaki hajapiga wala mavazi ya kulalia kubadilisha.
Baada ya kumaliza kujiandaa, alitoka chumbani na katika meza ya kulia chakula iliyo ghorofani huko, chai iliandaliwa. Alisogea mpaka mezani pale akiona kila kitu kimewekwa tayari, ilikuwa ni wazi kwa ajili yake lakini bado alihitaji uhakika na kuamua kuteremka chini mpaka jikoni alipo Angelina.
“Chai tayari, nimekuwekea meza ya ghorofani!” Angelina alimueleza mara tu baada ya kumuona.
“Na wewe?” alimdadisi.
“Nitakunywa nikimaliza hapa!” alijibu Angelina akiendelea kusafisha vyombo alivyotumia kuandaa kifungua kinywa.
“Unakuja ghorofani?” Malaika alimuuliza tena.
“Hapana, nitakula tu hapa hapa!” alijibu Angelina.
“Hapana; nakusubiria juu!” Malaika alimpinga akisisitiza kupata wote chai.
“Aah… mimi nitakuchelewesha!” alijitahidi kujitetea.
“Sahani na kikombe ndio hivi eeh, natangulia navyo!” Malaika alichukua vyombo alivyoona vikiwa pembeni kwenye meza ya jikoni pale.
“Usihangaike!” alijitahidi kumzuia.
“Nakusubiri!” alisisitiza Malaika akitoka jikoni mule kupandisha ghorofani.
Angelina alibaki akiona aibu, hakujua nini cha kufanya mbele ya Malaika; hakuwa amezoeana nae na akiwa wenye asili ya upole.
Hakuwa na namna, alimaliza kusafisha vyombo vile na kupanda ghorofani alipomkuta Malaika akitazama runinga sebuleni. Alipomuona, alinyanyuka kutoka sebuleni pale na kuelekea mezani kwenda kupata kifungua kinywa pamoja.
Malaika alikuwa na mengi ya kumuuliza Angelina lakini hakuwa na ujasiri au namna ya kuyauliza maswali hayo, njia pekee aliyokuwa nayo ni kutengeneza ukaribu na Angelina ili kupata kujua majibu yake ikiwezekana pasipo kuuliza, zaidi kama kuthibitisha mawazo aliyokuwa nayo.
Walikunywa chai bila kuzungumza lolote, Angelina alionekana kuwa mtaratibu sana na asiyependa kusema, muda mwingi akizungumza kwa kujibu alichoulizwa au kueleza jambo muhimu, hakuwa mzungumzaji na hilo lilimfanya Malaika kuona ugumu uliokuwa mbele yake.
Wakiwa wanamaliza kupata kifungua kinywa, walisikia mafundi wakiongea kuonesha kama wamemaliza na mlango mkubwa wa chini kugongwa. Angelina aliteremka mara moja akishuka na vyombo vyake alivyokuwa akitumia kwakuwa tayari alimaliza na kuvipeleka jikoni kabla ya kwenda kuwasikiliza wakimkabidhi ufunguo na kumueleza kuwa wamemaliza kazi iliyowaleta, gari likiwa tayari kutembelewa bila tatizo lolote na ikitokea kuna shida basi waelezwe na wao watashughulikia mara moja.
Aliipokea funguo ya gari lile na kurudi juu alikomuacha Malaika akiendelea kuoata kifungua kinywa chake.
“Wamemaliza, funguo hii hapa, gari lipo tayari!” alimueleza akimkabidhi funguo ile mezani pale.
“Lipo tayari, kila kitu kiko sawa, naweza kutembelea!?” alimuuliza maswali bila kituo kuonesha furaha aliyokuwa nayo.
“Ndio!” alijibu Angelina akitabasamu.
“Uuuuhh….!!” Mara moja kusikia jibu la Angelina, Malaika alinyanyuka kwenye kiti alichokuwa amekalia na kuondoka mezani pale.
“Ahsante; sana!” alimshukuru akiichukua funguo ile na kuteremka ngazi upesi akimuacha Angelina akimtazama na kucheka.
