
Dr. BUDODI
June 13, 2025 at 09:11 PM
*UTE HUHUSIKA VIPI KWENYE UJAA UZITO?*
Mlango wa kizazi hutengeneza ute(cervical Mucus) kwaajili ya kulinda kizazi lakini pia kwaajili ya kusaidia mbegu za mwanaume kusafiri kwenda kwenye yai na kutungisha mimba. Ute huu ukiwa mzito zaidi ya kawaida, ukiwa na hali ya asidi, au ukiwa na seli za kinga ya mwili ambazo hushambulia mbegu za kiume ute huathiri uwezo wa mbegu kusafiri na hata kuzishambulia na kuziua kabla hazijaingia kwenye kizazi. Mwanamke anaweza kuwa na hali hii sababu ya changamoto za homoni (mf, viwango vya chini vya estrogen au viwango vya juu vya Progesterone), maambukizi kwenye kizazi, matumizi ya dawa kama clomiphene, au magonjwa kama polycystic ovarian syndrome (PCOs). Ute usiofaa hupunguza uwezo wa mbegu kuishi hadi chini ya saa moja badala ya siku 3-5. Dalili zinaweza kujumuisha ukavu ukeni, maumivu wakati wa tendo au hedhi zisizo za kawaida. Mara nyingi hugunduliwa kwa kipimo cha ute baada ya tendo(postcoital test). Kwa upande mwingine kujifunga kwa mlango wa kizazi(Cervical Stenosis), hutokea wakati njia ya mlango wa kizazi inapokuwa nyembamba sana au kujifunga kabisa kutokana na makovu ya upasuaji au vipimo vya kutoa nyama kwenye Cervix (mf. LEEP au cone biopsy). Maambukizi ya mara kwa mara, au matibabu ya mionzi baada ya kuugua kansa ya mlango wa kizazi pia husababisha. Mambo haya huzuia mbegu za kiume kuingia au ute kufanya kazi vizuri, na kuongeza utengenezwaji wa ute usiofaa. Dalili zinaweza kujumuisha maumivu makali wakati wa hedhi au kupata damu kidogo, lakini mara nyingi hazionekani hadi utakapofanyiwa vipimo.
*INASABABISHAJE UTASA?*
Ute usiofaa unazuia mbegu za kiume kufika kwenye yai kwa kuziua au kuzifanya zipoteze nguvu, ikifanya urutubishwaji wa yai kwa njia za kawaida kuwa mgumu. Hata kama mbegu chache zinafika, hatari ya kuharibika kwa mimba huongezeka kwa ~10-15% kutokana na mazingira yasiyo rafiki. Kujifunga kwa mlango wa kizazi huongeza tatizo kwa kuzuia mbegu za kiume kuingia kabisa au kuharibu ubora wa ute, ikipunguza nafasi za ujauzito na kupunguza ufanisi wa njia za upandikizaji kwa ~5-10%.
*NJIA SALAAMA NA SAHIHI YA KUPATA MTOTO.*
Njia za upandikizaji husaidia wanawake wenye changamoto hizi kupata watoto.
* _Intrauterine Insemination (IUI):_ Kwa njia hii mbegu za kiume huwekwa moja kwa moja kwenye mji wa mimba au mirija ya uzazi kipindi cha ovulation, ikiepuka changamoto ya ute usiofaa na mlango wa kizazi uliojifunga.
* _Cervical Dilation:_ Njia hii ya upasuaji inafungua mlango wa kizazi uliojifunga na kuruhusu IUI au IVF kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
* _In Vitro Fertilization (IVF):_ kwa njia hii mayai huvunwa kutoka kwa mwanamke kipindi cha ovulation na kuyarutubisha kwenye maabara, na mtoto aliepatikana hupandikizwa kwenye kizazi. Njia hii huepuka changamoto zote za mlango wa kizazi na hata zile za mirija ya uzazi.
*USHAURI WA KITAALAMU.*
Ikiwa una uke mkavu, hedhi zisizo eleweka, au historia ya upasuaji wa mlango wa kizazi, wasiliana na daktari mapema ambapo atapendekeza kipimo cha ute baada ya tendo (postcoital test) na hysteroscopy ili kugundua ute usiofaa na mlango wa kizazi kujifunga. IUI ni njia nzuri zaidi kwa wagonjwa wa tatizo hili, na cervical dilation inaweza kusaidia ikiwa mlango wa kizazi umejifunga. Usichelewe, kwani umri zaidi ya miaka 35 hupunguza ufanisi wa njia za upandikizaji. Jikinge na maambukizi ya mara kwa mara kwenye kizazi kwa kufanya ngono salama na kupata matibabu haraka ukiugua pia epuka matumizi ya hovyo ya clomiphene. Daktari atakupa msaada wa kisaikolojia utakaokusaidia kukabiliana na msongo wa mawazo kipindi cha matibabu. Kula chakula chenye vitamini E kwa wingi na kunywa maji mengi ili kuboresha afya ya ute wako. Kwa kuzingatia haya utaitwa mama.