
Dr. BUDODI
June 15, 2025 at 09:12 AM
KUGAWANYIKA KWA KIZAZI HUSABABISHA UTASA
Changamoto za kimaumbile mbali mbali zinazotekea ndani ya mji wa mimba husababisha utasa. Kugawanyika kwa kizazi(Bicornuate/ Septate Uterus) inaathiri ~2-5% ya wanawake wenye utasa.Hali hii hufanya iwe vigumu kwa wanawake hawa kupata mimba bila matibabu.
*KUGAWANYIKA KWA KIZAZI NI NINI?*
Mji wa mimba huota nyama(tishu) ambayo huugawanya katika sehemu mbili tofauti(Septate Uterus)na katika hali nyingine, mji wa mimba hugawanyika kuanzia nje na kutengeneza pande mbili tofauti. Hali hizi ni za kuzaliwa nazo(congenital anomalies) huathiri moja kwa moja utendaji kazi wa mji wa mimba kama kuweza kuhifadhi mimba na hata kuruhusu mbegu na yai kukutana. Hali hizi zinaweza rithishwa kati ya wanafamilia lakini matumizi ya kemikali kama diethylstilbestrol (DES) wakati wa ujauzito huongeza hatari ya changamoto hizi. Dalili zinaweza kujumuisha kuharibika kwa mimba mara kwa mara, hedhi zenye maumivu makali, maumivu ya nyonga, lakini wanawake wengi hawaonyeshi dalili hadi pale wanaposhindwa kupata ujauzito. Kasoro hizi za kimaumbile hugunduliwa kwa ultrasound, MRI, au hysteroscopy.
*INASABABISHAJE UTASA?*
Mgawanyiko wa kizazi hutengeneza mazingira magumu kwa mimba kutunga na pia huathiri ubora wa kuta za mji wa mimba kwa kupunguza mzunguko wa damu kwenye kizazi. Mimba hupandikizwa kwenye kuta zisizo na ubora hali ambayo huongeza hatari ya kuharibika kwa mimba kwa ~30-50% pia inasababisha mwanamke kujifungua kabla ya muda kwa.
*NJIA SALAMA ZA KUBEBA UJAAUZITO.*
* _Hysteroscopic Septum Resection(upasuaji):_ Njia hii ya upasuaji husaidia kurekebisha maumbile yasiyo sahihi. Inaweza tumika pekeake ambapo mwanamke ataweza kubeba mimba kwa njia za kawaida au inaweza tumika kabla ya IVF ili kuongeza ufanisi wa njia hizi za upandikizaji
* _In Vitro Fertilization (IVF):_ Baada ya upasuaji njia hii ya upandikizaji hutumika kuhakikisha mwanamke huyu anabeba mimba. Mayai huvunwa kutoka kwa mwanamke na urutubishaji utafanyika maabara na watoto watakaopatikana hupandikizwa kwenye kuta za mji wa mimba na mwanamke huyu hubeba ujaauzito.
*USHAURI WA KITAALAMU*
Ikiwa una historia ya kuharibika kwa mimba mara kwa mara, hedhi zenye maumivu makali, au unashindwa kupata ujauzito kabisa. wasiliana na daktari ambapo atapendekeza vipimo kama ultrasound, MRI, au hysteroscopy ili kugundua kasoro za kizazi kugawanyika. Hysteroscopic resection ni hatua ya kwanza katika kutibu Septate Uterus, na inaweza kurejesha uwezo wa mwanamke kubeba mimba kawaida au kuboresha IVF. Usichelewe, kwani umri zaidi ya 35 hupunguza ufanisi wa njia za upandikizaji. Epuka dawa au kemikali zinazoweza kuathiri homoni zako. Daktari atakupa ushauri wa kisaikolojia utakaokusaidia kukabiliana na msongo wa mawazo kipindi cha matibabu, hasa ikiwa mimba zimeharibika mara kadhaa. Kula chakula chenye vitamini D na omega-3 ili kuimarisha afya ya mji wa mimba. Zingatia haya kwa usahihi na utaitwa mama!.