DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS
June 22, 2025 at 12:39 AM
*MASOMO YA MISA YA JUMAPILI, JUNI 22 2025.* *DOMINIKA YA SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU SANA YA KRISTO, MWAKA C.* *RANGI YA LITURUJIA: NYEUPE 🤍* *MADA YA SIKUKUU:* ```CHUKUA NA ULE!``` *_Masomo matatu leo yanatualika kutafakari maana ya Ekaristi. Ekaristi ni lishe. Sio kama dawa ambayo hufanya kitu kiatomati, lazima ipokewe na imani, mtu akiwajibika kwa kile kitendo cha kula na kunywa mwili na damu ya Kristu kinachomaanishwa. Masomo yote matatu yanasisitiza juu ya kiunga cha karibu kati ya Ekaristi na maisha, kati ya mkate ambao ni Kristo na mkate ambao unalisha mwili. Hatuwezi kuwa katika ushirika na mwili wa Bwana bila kushirikishana kile tulicho acho. Tunaona hili katika somo la kwanza na Injili. Somo la pili linasisitiza jinsi pasiwepo na uwiano kati ya "kuumega mkate" na misuguano na migawanyo katika jumuiya._* *ANTIFONA YA KUINGIA:* Zaburi 81: 17 Mungu ametulisha kwa ngano bora, ametushibisha asali itokayo mwambani. *KOLEKTA* ```Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika Sakramenti ya ajabu; tunakuomba utujalie kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya Mwili na Damu yako, tupate kuona daima ndani yetu tunda la ukombozi wako. Unayeishi na kutawala pamoja na Mungu Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu...``` *SOMO LA KWANZA* Alileta mkate na divai. *Somo katika kitabu cha Mwanzo (MWANZO 14: 18 - 20)* Siku zile: Melkisedeki, mfalme wa Salemu, alileta mkate na divai; yeye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu. Akambariki Abramu akisema, "Abramu abarikiwe na Mungu Aliye Juu, Muumba wa mbingu na dunia. Atukuzwe Mungu Aliye Juu, aliyewatoa maadui wako mikononi mwako." Naye Abramu akamtolea sehemu yu kumi ya mateka yote. *Neno la Bwana......* *Tumshukuru Mungu.* *ZABURI YA KUITIKIZANA* Zaburi 110: 1, 2, 3, 4 (K.) 4bc *K. Ndiwe kuhani hata milele, kwa utaratibu wa Melkisedeki.* Bwana amemwambia Bwana wangu: keti mkono wangu wa kuume, mpaka niwafanyapo adui zako, kibao cha kuwekea miguu yako. *K.* Fimbo ya enzi yako Bwana atainyosha kutoka Sioni. Bwana asema: Tawala adui zako! *K.* Watu wako watakujia / kwa hiari siku ya vita vyako. Kwa fahari ya utakatifu tangu tumbo la mapambazuko kama umande nalikupata. *K.* Bwana ameapa wala hataghairi: "Ndiwe kuhani hata milele kwa utaratibu wa Melkisedeki." *K.* *SOMO LA PILI* Kila mnapoula mkate huo na kukinywea kikombe, mnatangaza kifo cha Bwana. *Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho (1 WAKORINTHO 11: 23 - 26)* Ndugu zangu: Niliyowakabidhi ninyi ndiyo niliyoyapokea mimi kwa Bwana, yaani usiku ule aliposalitiwa, Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega, akasema, "Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu: fanyeni hivi katika ukumbusho wangu." Kadhalika akatwaa kikombe baada ya kula, akasema, "Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu. Kila mnapokinywea fanyeni hivi katika ukumbusho wangu." Maana kila mmapoula mkate huo na kukinywea kikombe, mnatangaza kifo cha Bwana hata atakapokuja. *Neno la Bwana.....* *Tumshukuru Mungu.* *SHANGILIO LA INJILI* Yohane 6: 51 *K. Aleluya. W. Aleluya.* Mimi ndimi mkate wa uzima ulioshuka toka mbinguni, asema Bwana; aulaye mkate huu ataishi milele. *Aleluya.* *INJILI* Wote walikula, wakashiba. *Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Luka (LUKA 9: 11b - 17)* Wakati ule: Yesu alisema na watu juu ya ufalme wa Mungu, na akawaponya waliohitaji kuponywa. Kulipokuchwa, wale Kumi na Wawili wakamwendea, wakamwambia, "Waage watu waende katika vijiji vya jirani na kwa wakulima wa mashambani wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni mahali pa ukiwa." [Yesu] akawaambia, "Wapeni ninyi chakula." Wakajibu, "Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, labda twende kuwanunulia watu hawa wote chakula." Sasa wanaume peke yao walikuwa kadiri ya elfu tano. Kisha akawambia wafuasi wake, Waketisheni watu vikundi vya hamsini hamsini." Wakafanya hivyo wakawaketisha wote. Akaitwaa mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akaibariki, akaimega, akawapa wafuasi wake wawaandalie watu wa umati. Wote wakala wakashiba. Na vipande walivyoviokota vilijaza vikapu kumi na viwili. *Injili ya Bwana.......* *Sifa Kwako Ee Kristo.*
Image from DIVINE RETREAT UPDATES AND PRAYERS: *MASOMO YA MISA YA JUMAPILI, JUNI 22 2025.*   *DOMINIKA YA SHEREHE YA ...

Comments