Tanzanian Catholics Online
Tanzanian Catholics Online
June 1, 2025 at 06:38 AM
NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TATU, JUMAPILI Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina WIMBO WA ROHO MTAKATIFU Uje Roho (Sekwensia) 1. Uje Roho Mtakatifu, tuangaze toka mbingu, roho zetu kwa mwangao 2. Uje Baba wa maskini, uje mtoa wa vipaji, uje mwanga wa mioyo 3. Ee Mfariji mwema sana, ee Rafiki Mwanana, ewe raha mustarehe. 4. Kwenye kazi u pumziko, kwenye joto burudisho, u mfutaji wa machozi. 5. Ewe mwanga wenye heri, uwajaze waamini, neema yako mioyoni 6. Bila nguvu yako Wewe, mwanadamu hana kitu, kwake yote yana kosa 7. Osha machafuko yetu, panyeshee pakavu petu na kuponya majeraha 8. Ulegeze ukaidi, pasha moto ubaridi, nyosha upotovu wote 9. Wape waamini wako, wenye tumaini kwako, paji zako zote saba 10. Wape tuzo ya fadhila, wape mwisho bila hila, wape heri ya Milele. ROHO MTAKATIFU ANATUFANYA KUWA MITUME Bwana alisema kwa kinywa cha nabii Yoeli; “Katika siku zile za mwisho asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, waume kwa wake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.... hata watumishi wenu watamiminiwa Roho wangu katika siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu." (Rejea Mdo.2:17-21) Siku ile ya Pentekoste, bada ya Roho Mtakatifu kulishukia Kanisa, mitume waliwakumbusha watu maneno haya ya nabii Yoeli na miaka mingi baadae, Petro aliwaandikia barua Wakristo wa kwanza akawaambia; kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile wakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumikia anapaswa kutumikia kwa nguvu aliyojaliwa na Mungu ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele (Rejea. Pet 4;10-11). Mtaguso wa Pili wa Vatikano ulitukumbusha jambo hilo hilo uliposema; “Roho Mtakatifu anayetakasa taifa la Mungu kwa njia ya Sakramenti amewapa waamini mapaji ya pekee na kumjalia kila mmoja kadiri apendavyo. Kwa hiyo kila mmoja amgawie mwenzake kadiri ya vipawa alivyopewa, awe mgawaji mwaminifu wa neema ya Mungu, alijenge kanisa zima katika upendo. Tunao wajibu wa kutumia vipawa tulivyojaliwa na Roho Mtakatifu kwa manufaa ya Kanisa zima na kwa faida ya watu wote. Tuunganike sote pamoja na wachungaji wote katika kazi hiyo ya utume. Tumuombe basi Roho Mtakatifu atusaidie kutumia vema vipawa vyake alivyotujalia. 1. Ewe Roho Mtakatifu uwape wakristo neema na nguvu za kutumia vema vipaji ulivyowajalia kwa ajili ya kujenga Kanisa lako popote duniani, kwa ajili ya wokovu wa watu wote. W. Twakuomba utusikie 2. Utujalie sisi sote mapaji yako saba, tupate kukutumikia kwa uchaji W. Twakuomba utusikie 3. Utujalie tuwe mitume wa kweli wa wenzetu, tushirikiane na wachungaji wetu katika huduma za kuwaongoza watu wote na kuwafikisha mbinguni W. Twakuomba utusikie. 4. Utujalie hekima na nguvu za kuwahudumia watu wote kwa mapendo ya kweli yasiyo na kinyume W. Twakuomba utusikie 5. Utujalie neema ya kumpenda Mungu kwa moyo wote na kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda wenyewe W. Twakuomba utusikie 6. Utupe neema ya kulisikia neno lako na kulifuata, nayo mawazo yetu na matendo yetu yafuate daima mwongozo wako Mtakatifu W. Twakuomba utusikie 7. Uwazidishie mapaji yako wale wote wanaotumia vema vipawa vyao, uwarudishe na wale wanaotumia vibaya rehema zako W. Twakuomba utusikie TUOMBE; Ewe Roho Mungu ndiwe uliyewapa waamini vipawa vyako kwa kadiri unavyotaka. Utujalie tuyapokee na kuyatumia vema mapaji yako mengi kwa ajili ya utukufu wa Jina lako na kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. W. Amina LITANIA YA ROHO MTAKATIFU.
Image from Tanzanian Catholics Online: NOVENA YA ROHO MTAKATIFU SIKU YA TATU, JUMAPILI  Kwa jina la Baba na l...
🙏 1

Comments