
Radio Maria Tanzania
June 18, 2025 at 05:10 AM
MASOMO NA TAFAKARI SIKU YA JUMATANO - 18 JUNI 2025
Mtakatifu Juliana Falkonieri, Bikira.
Somo la Kwanza: 2 Kor 9:6-11
Injili: Mathayo 6:1-6, 16-18.
*Si kwa huzuni, wala si kwa lazima*
Paulo anaendeleza mada juu ya ukarimu na leo anatupa namna *ukarimu unavyotakiwa kuwa.* Anatupa mambo mawili ambayo ni si kwa huzuni na si kwa lazima.
1. Huzuni: katika utoaji hasa katika ukarimu, *huzuni huja kama hisia ya hasara na kupoteza.* Kwamba umetwanga maji kwenye kinu, umempigia mbuzi gitaa, umeenda mrama na *hivyo kujuta au hata kukasirika kwa utoaji.*
Ndugu wapendwa, *ukarimu ni uwekezaji na wema ni mtaji.* Tukumbuke maneno ya Bwana Yesu jinsi alivyosema mwenyewe, ni heri kutoa kuliko kupokea (Matendo 20:35) kwani wapendwa, *amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, Naye atamlipa kwa tendo lake jema* (Mithali 19:17). Tusichukulie ukarimu kama kamari kwamba unahuzunika ukikosa, *ukarimu unaakisi wema wa Mungu kwetu* (Yohane 3:16).
2. Lazima: *Matendo yanayofanyika kwa kulazimishwa mara nyingi hukosa kibali* kwa Mungu hata kwa wanadamu; kubaka, kuiba, ujambazi, hata ndoa hubatilishwa pindi inapogundulika mmoja wa wanandoa alilazimishwa, hakua na hiari yake kuingia katika ndoa. *Maana yake tunakosa baraka kama tunajikuta tunalazimika kufanya jambo flani.*
Kama ilivyo katika mambo mengine, *kulazimishwa kuwa mkarimu au kutoa msaada hakutuletei baraka wala furaha katika utoaji.* Tujifunze kutoa kwa upendo tukiamini kuwa Mungu ndiye mpaji wa vyote. Tukumbuke kwamba, tunavyotumia rasilimali zetu kunaonesha nia na madhumuni ya mioyo yetu zaidi ya maneno kwa kuwa *”pale akiba yako ilipo ndipo moyo wako utakapokuwa”* (Mathayo 6:21).
*Matokeo ya huzuni na ulazima katika utoaji ni kutaka kuonekana kwa watu ili kuhisi kuwa hujapoteza* na kuonekana hujalazimishwa, kwa ufupi matokeo ya hayo ni unafiki. Basi *”kila mtu atende kama alivyokusudia moyoni mwake”* 1Kor 9:7.
Mtakatifu Juliana Falkonieri, Bikira; Utuombee.
Padre Ignatius Kangwele - Jimbo Katoliki Tanga
www.radiomaria.co.tz
#katekisimukatolikishirikishi
#radiomariatanzaniamiaka20
#mariathon2025mamawatumaini

🙏
❤️
👍
❤
👏
🥰
55