Radio Maria Tanzania

Radio Maria Tanzania

350.5K subscribers

Verified Channel
Radio Maria Tanzania
Radio Maria Tanzania
June 22, 2025 at 02:56 AM
SHEREHE YA EKARISTI JUNI 22, 2025 - PADRE BONAVENTURE MARO C.PP.S leo ni Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo, sherehe ijulikanayo kama 'Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi'. Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii inatutafakarisha kuwa, “EKARISTI TAKATIFU NI ISHARA YA UPENDO NA UKARIMU WA KIMUNGU” Sherehe hii huadhimishwa Alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu, lakini kwa sababu za kichungaji, katika majimbo mbalimbali huadhimishwa Dominika baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa ameamua hivyo ili kuwapa Watoto wake nafasi ya kufurahia, kumsifu, kumwabudu na kumpa Mungu heshima ya pekee katika fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa maandamano yanayofanyika baada ya Misa Takatifu ili kuliishi, kulitafakari, kulishuhudia na kuonesha umuhimu na uhitaji wa Fumbo hili Takatifu katika Maisha yetu ya kiroho. Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, akatwaa mwili na kukaa kati yetu, akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu. CHIMBUKO LA SHEREHE YA MWILI NA DAMU TAKATIFU YA BWANA WETU YESU KRISTO. Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo ilianzishwa rasmi katika Kanisa, kutokana na uwepo na kusambaa kwa ibada mbalimbali kwa heshima ya Ekaristi Takatifu, uwepo halisi wa Mungu katika maumbo ya mkate na divai mapema katika karne ya 13AD. Kwa kusaidiwa na wanateolojia mbalimbali na viongozi wa Kanisa kwa wakati huo, Sherehe hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1246 katika Jimbo la Liége huko Ubelgiji ikijulikana kama 'Corpus Christi', yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo. Mwaka 1264 Baba Mtakatifu Urbano IV aliidhinisha Sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa kote ulimwenguni. Alimwomba Mtakatifu Tomasi wa Aquino kuandika nyimbo na machapisho mbalimbali ya kiliturjia kwa ajili ya sherehe hii kama vile Pange Lingua, Tantum Ergo na Adore te. Mwaka 1263, uliotokea muujiza wa Ekaristi Takatifu huko Bolsena Italia ambapo Hostia Takatifu ilivuja damu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu wakati ambapo Padre aliyeadhimisha alikua na mashaka juu ya uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Muujiza huu ulipeleka kukua na kusambaa kwa haraka kwa ibada kwa Ekaristi Takatifu na kwa namna ya pekee Sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Baadaye Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) walifundisha kuwa, “Tunapaswa kumpa heshima Bwana wetu Yesu katika Ekaristi Takatifu hadharani ili wale wanaotazama Imani ya Wakristo Wakatoliki waweze kuvutwa na Yesu Ekaristi Takatifu, na kuweza kuamini katika Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai na mzima katika Fumbo Takatifu sana la Ekaristi Takatifu” Hii ilitokana na kuwepo kwa mafundisho mbalimbali ya uzushi juu ya Ekaristi Takatifu juu ya uwepo halisi wa Kristo (Real Präsenz) katika maumbo ya Mkate na divai, kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Ibada ya Misa Takatifu na maandamano ya Ekaristi Takatifu. Katika majiundo ya mtaguso wa pili wa Vatikano 1962-1965, Sherehe hii iliunganishwa na Sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu ambayo huadhimishwa tarehe 1 Julai, ili kusisitiza teolojia ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo jina lilibadilika kutoka 'Corpus Christi' yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo na kuitwa 'Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi', yaani Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo na ndivyo inavyojulikana hata sasa. MSINGI KATIKA MAANDIKO MATAKATIFU. Imani yetu katika uwepo halisi na kweli wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai upo katika maandiko Matakatifu ambapo ni Kristo mwenyewe alitoka mwili wake kama Chakula na Damu yake kama kinywaji kwa ajili yetu na akawapa Mitume wake mamlaka ya kuadhimisha fumbo hilo Takatifu kwa ukumbusho wake mpaka atakaporudi tena (Mt 26:26-29; Mk 14:22-25; Lk 22:14-20; 1 Kor 11:23-26 na Injili ya Yohane sura ya 6). Ndilo Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu tunaloadhimisha kila siku, ukumbusho wa sadaka ya Kristo pale msalabani. Nini kinatokea katika mageuzo wakati wa ibada ya misa Takatifu? Katika ibada ya Misa Takatifu, mkate hugeuzwa kuwa mwili wa Kristo na Divai kuwa Damu ya Kristo, mabadiliko yajulikanayo kama Transubstantiation. Ndugu wapendwa, mababa wa mtaguso wa Trento wanasema hivi, “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba huu ndio mwili wangu, akautoa mwenyewe kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai. Hivyo kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake”. Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai huanza katika mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo. Hivyo, Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao. Kwa jinsi hii, kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo. Uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika hata katika kila tone la damu yake, uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (KKK 1376-1377). Inaendeleaaaaaa.... Tunakutakia Tafakari njema mpendwa. #radiomariatanzania #mahujajikatikamatumaini #mariathon2025mamawamatumaini
Image from Radio Maria Tanzania: SHEREHE YA EKARISTI JUNI 22, 2025 - PADRE BONAVENTURE MARO C.PP.S  leo...
🙏 ❤️ 🤲 32

Comments