
Aviation Tanzania 🇹🇿
June 15, 2025 at 06:16 AM
https://www.instagram.com/p/DK6TbhyNW8z/?igsh=MXhxbGh2ZTc5N2ZubA==
*Wote walinusurika Wakiwa Kwenye siti namba 11A: Mwanamuziki wa Thailand na Manusura wa ajali ya Air India.*
Msanii maarufu wa muziki nchini Thailand, Ruangsak Loychusak, ameibua hisia mpya za majonzi na mshangao baada ya kusimulia kuwa aliwahi kunusurika katika ajali mbaya ya ndege ya Thai Airways mwaka 1998 akiwa amekaa kwenye siti namba 11A – sehemu ileile ambayo Bw.Vishwash Kumar Ramesh, manusura pekee wa ajali ya ndege ya Air India, iliyotokea hivi karibuni, alikuwa ameketi.
Ruangsak, ambaye alipata umaarufu mkubwa miaka ya 90 kwa jina la utani “Iron Bones”, alinusurika ajali ya ndege ya Thai Airways TG261 iliyotokea mnamo Disemba 11, 1998, wakati ndege aina ya Airbus ilipoanguka kwenye shamba la mpira huko Surat Thani, na kusababisha vifo vya watu 101. Akiwa ameketi katika kiti namba 11A, alinusurika kwa miujiza lakini aliishi na hofu ya kutumia usafiri wa anga kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi.
Ruangsak alipata mshtuko baada ya kusikia kuwa Vishwash Kumar Ramesh, manusura pekee wa ajali ya ndege ya Air India, Boeing 787 Dreamliner iliyotokea tarehe 12 Juni 2025 huko Ahmedabad, India, naye alikuwa ameketi kwenye kiti namba 11A kabla ya ndege hiyo kuanguka katika bweni la chuo kikuu na kuua watu wote waliokuwemo isipokuwa yeye.
Kupitia chapisho lake la hisia mitandaoni, Ruangsak alieleza kuwa taarifa hiyo ilimpa msisimko usio wa kawaida na kumfanya atafakari kwa kina namna maisha yalivyojawa na miujiza.
Aidha, alitoa salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali ya Air India, akisema kuwa kiti namba 11A sasa ni zaidi ya namba – ni alama ya matumaini na ushuhuda wa uhai katika mazingira ya maafa.
#planecrash #survivor #planecrashsurvivor #airindia #boeing787dreamliner #aviationtanzania✈ #aviationtanzaniaupdates #aviata #aviataupdates