
Aviation Tanzania 🇹🇿
May 26, 2025 at 05:48 PM
https://www.instagram.com/p/DKIC32nsera/?igsh=NHp6N2dlMnJmaWs3
*Abiria atakayeinuka kabla ya ndege kusimama atatozwa faini ya Dola 70*
Mamlaka ya usafiri wa anga ya Uturuki imeweka sheria mpya inayowataka abiria wote kubaki wamekaa hadi ndege itakapokuwa imesimama kikamilifu kwenye eneo la kupaki,na Kwa abiria atakayekiuka sheria hiyo atatozwa faini ya dola 70 za Kimarekani.
Sheria hiyo inalenga kukomesha tabia ya abiria kuamka mapema na kuanza kupanga foleni kwenye korido mara tu ndege inapotua, kabla hata ya ndege kufika kwenye kituo cha kupaki. Mamlaka hiyo inasema hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa wasafiri na wafanyakazi wa ndege, na tayari mashirika ya ndege yameelekezwa kutoa maelekezo ya wazi kwa abiria kuhusu kutii agizo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la DPA kutoka Ujerumani, mashirika ya ndege yamepewa jukumu la kuwakumbusha abiria kufunga mikanda wakati wote wa kutua hadi ndege itakapopaki, na kwamba yeyote atakayekiuka agizo hilo ataripotiwa katika mamlaka na kutozwa faini.
Abiria wengi wamekuwa wakionekana wakifungua mikanda yao mara tu ndege inapotua na kuamka kuelekea mlangoni kwa lengo la kuwa wa kwanza kushuka au kuchukua mizigo yao, jambo linaloonekana kuhatarisha usalama na kuvuruga taratibu za kushuka kwa mpangilio.
Turkish Airlines, shirika la taifa la Uturuki ambalo linatoa huduma ya usafiri katika nchi zaidi ya 130, tayari limeanza kutekeleza sheria hiyo. Mashirika mengine ya kimataifa kama Emirates na Qatar Airways yanaripotiwa pia kuzingatia kuanzisha utaratibu huo.
#airline #turkishairlines #airlinepassengers #aviationtanzania✈ #aviationtanzaniaupdates #aviata #aviataupdates